Hongereni Tanzanite kwa mlipofikia, haikuwa riziki

07Feb 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hongereni Tanzanite kwa mlipofikia, haikuwa riziki

IJUMAA iliyopita Watanzania walipatwa na huzuni, baada ya timu yao ya Taifa ya Wanawake chini wa miaka 20, maarufu kama Tanzanite ilipochapwa mabao 2-0 mjini Addis Ababa, Ethiopia na timu ya taifa hilo kwenye mchezo wa raundi ya tatu kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia, zinazotarajiwa ...

kufanyika nchini Costa Rica kuanzia Agosti 10 hadi 28, mwaka huu.

Kwa kipigo hicho cha ugenini, Tanzanite imetolewa kwa jumla ya mabao 2-1, kutokana na mechi ya kwanza hapa nchini kushinda kwa bao 1-0.

Ilibaki hatua moja wasichana hao kuingia kwenye vitabu vya kumbukumbu ya soka la Tanzania kwani ingeweza kuiwakilisha nchi kwenye fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza na ingekuwa ni sifa kwa nchi.

Hata hivyo, ukiangalia timu hiyo ilikotoka hadi ilipofikia kwa ujumla imejitahidi sana na haipaswi kubezwa wala kulaumiwa kwa matokeo hayo.

Kinachotakiwa kwa sasa ni kuwapongeza, na kuwapa moyo kwamba walichokifanya ni sifa kwa taifa, kwani kuna nchi nyingi zimetolewa.

Ikumbukwe kuwa timu hiyo ilianza michuano hiyo kwenye raundi ya pili kwa kucheza dhidi ya Eritrea na kwenda kushinda ugenini mabao 3-0 Septemba na ikashinda mabao 2-0 nyumbani Oktoba mwaka jana. Hii ilikuwa ni raundi ya tatu na hata ukiangalia haijatolewa kwa idadi kubwa ya mabao, badala ni tofauti ya bao moja tu.

Inawezekana kilichowaponza ni kushinda idadi ndogo ya mabao nyumbani. Na hili si tatizo la timu hiyo tu ya wanawake chini ya miaka 20, bali lipo kwa timu zote za Taifa za Tanzania, kuanzia Taifa Stars, ya vijana, hata Wanawake, Twiga Queens.

Kinachotakiwa sasa kwa Shirikisho la Soka nchini (TFF), pamoja na klabu mbalimbali nchini ni kuandaa vijana wengi zaidi kwa ajili ya siku zinazokuja, kwani waliopo inawezekana ikawa ni mwaka wao wa mwisho kucheza michuano hiyo chini ya miaka 20.

Watakwenda kuichezea Twiga Stars na kuongeza kitu huko, lakini tatizo kubwa litakuwa huku chini kupata wachezaji wapya ambao wataibeba tena Tanzania kwenye michuano kama hiyo.

Kuna michuano ya CECAFA, pia Tanzania imekuwa ikialikwa kwenye michuano ya wasichana chini ya miaka 20 kwa Ukanda wa Kusini mwa Afrika (COSAFA) na imekuwa ikifanya vema, pamoja na mashindano mbalimbali ya Afrika.

Klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake zinatakiwa wakati huu ambao Tanzanite wametolewa kusaka vipaji vingine, si kwa ajili ya timu zao tu, bali hata kwa timu ya taifa, kwani TFF inategemea kuteua wachezaji kutoka kwenye klabu hizo na si vinginevyo.

Inaeleweka kuwapata wachezaji wa kike ni ngumu sana tofauti na wanaume, lakini wazazi wamekuwa wagumu kuwaruhusu mabinti zao kucheza mchezo huo.

Ila angalau kwa sasa kutokana na maendeleo ya mchezo huo, kuanzishwa kwa Ligi Kuu, kuanza kuonyeshwa mechi za timu za taifa, pamoja michezo ya Ligi ya Wanawake, kumeanza kulegeza kidogo mitazamo ya wazazi na sasa wameona inawezekana kabisa ikawa njia ya mabinti zao kujipatia ajira, kujikwamua kiuchumi na hata kusaidia familia zao.

Mchezaji wa zamani wa Simba, Mussa Hassan Mgosi, wakati akiwa kocha wa Simba Queens, ameshakaririwa akisema kuwa kuna mabinti ambao wameshajenga nyumba, kukarabati nyumba za wazazi wao kutokana na kucheza soka la wanawake.

Hii inaonyesha kuwa angalau soka la wanawake limeshaanza kulipa, hivyo tunategemea kupata vipaji kutoka chini, na inawezekana kabisa Tanzanite mwakani ikapata wachezaji bora zaidi watakaokuja kuungana na walioko ambao hawajazidi umri wa miaka 20 kwa ajili ya kuanza tena harakati za kusaka tena tiketi ya kucheza fainali za mataifa Afrika na pia Kombe la Dunia ambalo ilikuwa almanusura wasichana waipeleke Tanzania nchini Costa Rica.