Simba, Yanga ziboreshe vikosi vyao kwa michuano ya kimataifa

12Nov 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Simba, Yanga ziboreshe vikosi vyao kwa michuano ya kimataifa

JUMATANO iliyopita Tanzania iliingia kwenye historia ya aina yake baada ya klabu mbili kongwe nchini, Simba na Yanga zote kuingia kwenye hatua za makundi ya michuano ya kimataifa.

Hii ni rekodi ya aina yake kwani mara nyingi timu hizi zimekuwa zikibadilishana tu, Yanga ikitwaa ubingwa Simba inabaki na inakuwa kinyume chake kama Simba ikitwaa ubingwa.

Ni msimu mmoja tu ambao timu za Tanzania zilikuwa kwenye hatua za makundi pamoja msimu wa 2020/21 wakati Namungo ilipotinga hatua hiyo kwenye Kombe la Shirikisho, na Simba ikawa kwenye hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.

Msimu huu tunakwenda kuziona timu kubwa zenye mashabiki wengi nchini zote zikiwa kwenye hatua za makundi, Simba kama kawaida ikiwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Yanga ikitinga Kombe la Shirikisho.

Simba ilitinga hatua hiyo baada ya kuifunga Primeiro de Agosto ya Angola na Jumatano iliyopita Yanga ilifanikiwa kutinga hatua hiyo kwa kuitoa Club Africain ya Tunisia bao 1-0.

Ni hatua ya kupongezwa kwenye soka la Tanzania kwani imeiweka kwenye mazingira mazuri mwakani kuendelea kuwakilishwa na timu nne bila ya kujali kama zitafanya vema kwenye mechi zao au la.

Hata hivyo, pamoja na kupongeza hatua hiyo, lakini nazitahadharisha timu hizo kuwa pamoja na wanachama na mashabiki zao wanafurahia hali hiyo, lakini wanapokwenda ni pagumu zaidi kuliko walikotoka.

Sizitishi na hizi si zama za kuogopa timu, kwani tumeona matokeo ya ajabu na ya kushangaza, ikiwemo kusukumizwa nje ya michuano ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita, RS Berkane ya Morocco, lakini kwa sasa Simba na Yanga zinatakiwa ziboreshe vikosi vyao.

Kwa vikosi vilivyonavyo, ni kweli zinaweza kushinda, lakini zitapata tabu sana.

Kwa upande wa Yanga naona kinachotakiwa kurekebishwa ni sehemu ya ulinzi kwani imekuwa na tatizo. Pamoja na kwamba walicheza vema kwenye mechi dhidi ya Club Africain, lakini timu hiyo ilionekana ina wachezaji wazito, wasio na mbio. Kama Yanga ikipata wapinzani wenye wachezaji wepesi na kasi, huwa inakatika na kufanya makosa mengi.

Msingi na nguvu kubwa ya Yanga ipo kwenye viungo, ina wachezaji viungo wa kukaba wenye uwezo wa hali ya juu ambao wanaifanya beki kutulia na kusawazisha makosa madogo madogo tu.

Mbele inatakiwa itafute mbadala wa Fiston Mayele, kwani amekuwa peke yake ndiyo straika hatari mbele bila msaidizi yeyote wa maana. Michuano ni mirefu na Yanga ina mashindano mengi, Ligi Kuu na Kombe la FA.

Simba ukiitazama kiufundi ina matatizo mengi kuliko Yanga. Haina kiungo wa kukaba wa kiwango cha michuano ya Ligi ya Mabingwa. Inatakiwa isajili kiungo wa uhakika na hawa waliopo sasa Mzamiru Yassin na Sadio Kanoute wawe wanamsaidia. Ikienda huko na kiungo kama Jonas Mkude kwa kiwango chake cha sasa ambacho anaweza asipate namba hata Azam FC, basi wamekwisha.

Simba inatakiwa ipate kiungo mshambuliaji wa kumsaidia Clatous Chama ambaye kama asipokuwepo ni kama tu timu yenyewe haipo. Timu yote ya Simba akikosekana yeye hakuna tena ubunifu, hayo ni makosa makubwa kwa timu inayocheza kimataifa.

Inatakiwa pia kusajili straika mmoja mkubwa mwenye uwezo wa hali ya juu ili kusaidiana na Moses Phiri.

Simba kwa sasa inakosa straika mwenye asili kama Chris Mugalu akiwa kwenye kiwango chake ambaye anaweza kumiliki mipira akiwa na mabeki wa timu pinzani. Mbali na kumiliki, awe pia na uwezo wa kufunga mabao. Inatakiwa pia ipate beki wa pembeni mwenye uwezo wa kucheza namba zote mbili ili kuwafanya wanachama na mashabiki wa Simba akiumia Shomari Kapombe au Mohamed Hussein 'Tshabalala' basi hawana amani.

Kama timu hizo zikifanikiwa kuziba mapengo hayo zinaweza kabisa kushangaza Afrika na Tanzania ikang'aa zaidi.