Majaliwa wapo wengi mtaani, hawaja ajiriwa tu kuonekana

11Nov 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Majaliwa wapo wengi mtaani, hawaja ajiriwa tu kuonekana

Ndege hiyo ilianguka ilipokuwa ikijaribu bila mafanikio kutua kwenye Uwanja wa Ndege, Bukoba mkoani Kagera.

Ajali hiyo ilitokea asubuhi majira ya saa 2:30 asubuhi na kuleta mshituko na simanzi si kwa Watanzania tu, bali hata wananchi wote wa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Ndege hiyo ilianguka ilipokuwa ikijaribu bila mafanikio kutua kwenye Uwanja wa Ndege, Bukoba mkoani Kagera.

Ajali hiyo ilitokea asubuhi majira ya saa 2:30 asubuhi na kuleta mshituko na simanzi si kwa Watanzania tu, bali hata wananchi wote wa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Wakati ikitangazwa idadi ya waliookolewa, ndipo likaja jina la kijana Majaliwa Jackson. Kwa sasa, amekuwa kijana maarufu zaidi nchini Tanzania kutokana na kutangazwa na Mkuu wa mkoa huo, Albert Chalamila na baadaye Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Walimtangaza kuwa ndiye aliyeokoa kiasi cha abiria 24 waliotoka hai ndani ya ndege hiyo. Yeye mwenyewe alisimulia jinsi alivyofanya kila aina ya njia kuhakikisha anawaokoa watu waliokuwa ndani ya ndege hiyo wakihangaika kufungua mlango wa ndege bila ya mafanikio.

Sitaki kurudia kila kitu kilichozungumzwa naye au jinsi alivyowaokoa, kwa sababu kila mtu ameshasikia, kusoma au kuona kwenye televisheni, jinsi alivyotumia njia zake kuokoa watu.

Kifupi tu ni kwamba, kijana huyo ni shujaa. Hakuangalia usalama wake yeye mwenyewe, kwani kuikimbilia ndege ambayo imeanguka nayo inahitaji moyo na ujasiri wa hali juu, kwa sababu inaweza kulipuka.

Alibebwa na ubinadamu zaidi na wala yote yanayotokea yeye hakutegemea wala kudhania kuwa yatamtokea.

Kijana wa kawaida tu, kutoka maisha ya kawaida  mvuvi mdogo, anayetumia mitumbwi hafifu, bila kujali matatizo yote ya nyumbani na ya kimaisha, akabebwa na roho ya huruma kwa binadamu wenzake bila kujali usalama wake, akaokoa roho za binadamu wenzake.

Wala hakutegemea malipo, lakini tayari viongozi wa watu kadhaa wamekuwa wakiahidi kumpa fedha ambazo ukizisikia ni kama ndogo hivi, lakini kwa Majaliwa ni pesa nyingi sana, kwani inawezekana kabisa hakufikiria wala kuota kuzishika kwenye maisha yake.

Kama vile haitoshi, Rais Samia Suluhu Hassan akaagiza kuwa kijana huyo apelekwe kwenye Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Kijana ambaye ndoto zake za kusoma zilikatishwa na umasikini, leo anakwenda kupata mafunzo, lakini bado akiwa na ujuzi wake wa kuvua samaki na kuogelea.

Tutaongea mengi ya kitendo cha kishujaa alichofanya Majaliwa, lakini ninachoweza kusema ni kwamba, kama ajali ya ndege isingetokea hakuna mtu yeyote ambaye angejua kipaji cha kijana huyo.

Kipaji cha kuogelea kwenye maji kwa ufundi wa hali ya juu na kuweza kukaa majini kwa muda mrefu. Hapa Tanzania si Majaliwa tu, kuna vijana wengi sana hasa mitaani wana vipaji vikubwa na vya ajabu, lakini hawajafikiwa au kutokea tukio linaloweza kuwafanya wafahamike au 'wa-trendi' kwa lugha ya kisasa.

Achilia suala la maji kuogelea, wapo vijana wenye uwezo mkubwa wa kuruka sarakasi, ufundi redio, televisheni, ujenzi, michezo na vingine vingi vinavyofanana na hivyo, lakini bado wamekuwa wakiishia mitaani tu.

Nikisema ufundi redio, siyo kwamba anatengeneza redio iliyoharibika, la hasha! Ila anaweza kuchukua nta na mbao, waya na vifaa vingine akatengeneza redio ikavuta mawimbi na kuongea. 

Unashangaa kijana kama huyu akichukuliwa na kuendelezwa kwa mafunzo, anaweza kuwa mtu wa aina gani? Kuna fundi gereji, ambaye akisikia mngurumo tu wa gari anajua lina tatizo gani na haichukui muda mrefu analitengeneza.

Nchi za wenzetu hukusanya kijana wenye vipaji na serikali inaingia gharama ya kuwasomesha wao wenyewe kwa sababu mara nyingi kama ilivyo kwa Majaliwa, wenye vipaji walivyopewa na Mungu kutoka kwenye familia masikini  wanashindwa kusomeshwa na wazazi wao.

Serikali nyingi hasa zilizoendelea zimeshagudua hilo na kufanya utaratibu na kila idara kukusanya vijana wa aina hiyo, wanapowasomesha wanawaletea mafanikio makubwa sana kwenye nchi zao.

Usione nchi zinatengeneza ndege, vipuri, treni, ndege za kivita, silaha za kulinda nchi, majengo makubwa ya kisasa yenye nakshi, wana- michezo mahiri wote wanatokana na mchango wa serikali kutafuta vipaji vilivyojificha na kuvichukua.

Zinafanya kama mtu aliyeokota dhahabu na kwenda kuisafisha. Isingekuwa ajali, tusingejua kipaji cha Majaliwa. Nadhani, sasa tusisubiri kuvipata vipaji vya vijana wa Kitanzania kwa bahati mbaya. 

Rais ameonyesha mfano kwa kutotaka kipaji hicho kipotee, hivyo wenye majukumu hayo kwenye taasisi mbalimbali za serikali sasa, wana dhima ya kuanza kutafuta mazingira ya kusaka vipaji mbalimbali ili vilisaidie taifa. Ili nchi ikue na ipate maendeleo kwa karne ya sasa inahitaji wenye elimu na vipaji pia.