Tuondoe dhana potofu ili tufanye kilimo chenye tija

09Nov 2022
Golden Kisapile, TUDARCo
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tuondoe dhana potofu ili tufanye kilimo chenye tija

“KILIMO ni uti mgongo wa uchumi wa taifa.” Ni kauli inayoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akihamasisha umma kukipenda kilimo na kujizatiti kwenye uzalishaji mashambani.

Kilimo ni hazina kwa taifa  kwa sababu huchangia kwa kiasi kikubwa mapato, fedha za kigeni kwa mfano kilimo cha korosho kina mchango mkubwa kwenye pato la taifa na uchumi wa nchi hii.

Kuna kilimo cha mwani kinachofanyika Zanzibar na zama hizi kilo moja imefikia Shilingi milioni  1.5. Ni habari njema kwa wakulima.

Kuna mengine mengi kama kahawa, mbaazi, alizeti, ufuta ambayo ni sehemu ya mazao lukuki ya chakula (mafuta) na biashara yanayoongeza mapato ya nchi na ya wakulima.

Tanzania ina ardhi kubwa yenye  rutuba na mabonde yanayoweza kufanikisha kilimo cha umwagiliaji ambayo yanafaa kuzalisha chakula na biashara na mengine mengi kuanzia mtama, mihogo, mpunga, mahindi na ngano wakati ya biashara ni pamoja na  pamba, korosho, kahawa na vanila.

Wizara ya Kilimo inatoa rai kwa Watanzania kujihusisha na kilimo, kwa sababu ni sekta yenye tija kwa taifa tena ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi na kwamba sehemu kubwa ya ardhi takribani asilimia 90 hutumiwa na wakulima wadogo ambao wengi kati yao ni wanawake.

Ni sekta inayotoa ajira kwa asilimia 65.5 na kuchangia kwa asilimia 29.1 ya pato la taifa, aidha asilimia 30 ya soko la nje imejaa mazao yake wakati asilimia 65 ya malighafi za viwanda zinatoka kwenye kilimo.

Suala la ajira linahusisha watu kujiingiza kwenye mnyororo wa thamani kama kulima,  kusafirisha, kuchakata, kufungasha na kuweka kwenye maghala hadi kuwafikishia walaji mezani.

Lakini hapo kuna wazalishaji na wasambaza mbolea, mbegu na viuatilifu kwa wakulima.

Lakini kilimo wengi hawakifurahii. Kumekuwapo na dhana potofu kuhusiana na kilimo kwa hiyo wananchi hawana budi kupiga vita fikra hizo kama vile, ukulima ni kazi ya watu maskini hasa wasiosoma, huenda Watanzania walio wengi hawajishughulishi na kilimo kwa sababu wana taswira hiyo na mitizamo hasi akilini. Wengine wanapenda kukaa kijiweni kuliko kwenda shambani.

Kuendelea kudhani kuwa kilimo ni cha watu maskini kunapunguza mwamko na morali  kwa watu kujihusisha na ukulima na inatakiwa kuiepuka fikra hiyo ili watu wengi wajiingize mashambani  kulima.

Kilimo ni cha watu wa rika fulani kama vile wazee tu ndio wanatakiwa kulima kwa hiyo hii dhana inaondoa ari ya vijana kujihusisha na kilimo, hivyo kwa pamoja tuungane tupinge mtizamo huo ili tukikuze na kuuendeleza uchumi kwenye sekta hiyo.

Dhana nyingine zinazosambaa miongoni mwa vijana ni pamoja na ile isemayo  kilimo ni cha watu waliofeli darasani, wengi wanaichukulia kuwa kulima ni kujitesa na ni jambo linalowahusu wasiofanikiwa hasa wale wenye  maisha duni na wasioweza kuchangamkia fursa za maendeleo zilizoko mijini.

Lakini si kweli. Hata yule ambaye alifaulu maisha anaweza kufanya kilimo na kuna ugunduzi na matumizi ya vitu kama vitalu nyumba ‘green houses’ kulima kwenye maji ‘hydroponics’ vyote vikilenga kukuza na kuboresha kilimo ili kuinua uchumi wa nchi na kuwa na tija ili kufikia maendeleo.

Hivyo ni vyema kuanzia shuleni, vyuoni na ndani ya jamii watu waelimishwe umuhimu wa kuithamini sekta hiyo kuwa ni mwanzo wa chakula mezani, biashara endelevu na maisha bora kwa kila Mtanzania na kila anayeishi kwa kuwa chakula ni uhai na bila kula hakuna uhai.