Mashabiki kwa sasa wamekuwa wakijazana hotelini, baa, majumba mengine ya starehe, majumbani mwao na hata kwenye vibanda vya kuonyesha michezo maarufu 'vibanda umiza' ili kufuatilia mechi hizo.
Kutokana na hali hiyo, Bodi Ligi Tanzania Bara, imesema ipo katika mchakato wa kupata mshauri wa kufanya tathmini kugungua kwa nini idadi ya watu wanaohudhuria mechi uwanjani inashuka, hivyo kusababisha mapato ya mlangoni kupungua katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almasi Kasongo, anasema idadi ya mashabiki uwanjani imepungua na bodi ipo katika kufanya tathmini na kutafuta ufumbuzi wa sababu ya watu kutoingia uwanjani kama ilivyo miaka ya nyuma.
Alisema wapo kwenye kipindi cha mpito, hivyo wanatakiwa kutafakari na kuangalia jinsi ya kupunguza viingilio.
Hata hivyo, wakati bodi inaendelea kutafuta mshauri, ngoja mimi nianze kuwapa ushauri ambao unaweza baadaye ukawasaidia kujua ni kwa nini mashabiki wengi kwa sasa wamepungua kwenda viwanjani.
Kwanza kabisa naweza kusema pamoja na kwamba Kasongo amelichukulia kwa ujumla, lakini suala hili linawahusu zaidi mashabiki wa Dar es Salaam.
Mashabiki wa mikoani tunaona huwa wanajazana viwanjani na hasa zinapokwenda klabu kubwa mbili maarufu na kongwe nchini Simba na Yanga. Mechi zingine zikichezwa hata huko mikoani kama vile Kagera Sugar dhidi ya Ihefu huwezi kuona idadi kubwa ya mashabiki.
Hata hapa kinachozungumzwa, mashabiki wanaotajwa kuwa wamepungua viwanjani si wa Singida Big Stars, wala Coastal Union, ni wa Simba na Yanga tu. Huu ndiyo utamaduni wa soka la Tanzania tangu enzi na enzi.
Tuje sasa kwenye muktadha wa kwa nini mashabiki wengi hawaendi viwanjani. Nawatetea wa mikoani, wao huwa wanaenda zinapokwenda timu pendwa. Nawaongelea wa Dar es Salaam ambao kwa sasa hata timu zao Simba na Yanga zikicheza hawajazani kama zamani. Na Bodi imeshindwa kuweka bayana hili.
Sababu zipo nyingi sana kama vile mazingira magumu ya kupata tiketi, usumbufu milangoni na kuchukuliwa kama mhalifu na si mteja, mazingira ya vyoo, pamoja na shabiki kutokuwa na kitu kipya kigeni kinachoweza kumvutia kuwa uwanjani zaidi na zile dakika 90 tu, lakini kwa sasa kuna kitu kingine kinaitwa muda wa mechi.
Kwa sasa asilimia 90 au zaidi mechi zote za Ligi Kuu au Kombe la FA za Simba na Yanga zinazochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa muda wake ni saa 1:00 usiku. Hii ni moja ya sababu kubwa kupungua kwa mashabiki viwanjani.
Zamani mashabiki waliokuwa wakija viwanjani walikuwa wanatoka Temeke, Tandika, Magomeni, Mwananyamala, Kigogo, Mburahati, Ilala na sehemu zilizo ndani ya Jiji la Dar es Salaam, hivyo walikuwa wanajazana viwanjani.
Kwa sasa jiji limekuwa kubwa, kuna wakazi wa Goba, Mbezi Louis, Mbezi Beach, Bunju, Boko, Kisemvule, Chanika na sehemu nyingine nyingi zilizo nje ya jiji.
Kuna mashabiki wengine wanatoka Bagamoyo mkoani Pwani hadi Chalinze kuangalia mechi. Hawa ukiwawekea mechi ya saa moja usiku tatizo lao inakuwa ni usafiri wakati wa kurejea makwao. Kutoka Benjamin Mkapa usiku wa saa tatu, hadi kufika kwao ni usiku wa manane kutokana na umbali pamoja na shida ya usafiri. Atapanda daladala ambayo bei imeongezwa mara mbili ya kawaida, akishuka anapokwenda anaweza kupanda tena daladala nyingine ya kuingia kwenye viunga vya ndani. Halafu pia atashuka na kupanda bodaboda ili kumfikisha nyumbani kabisa. Gharama za usafiri usiku mara nyingi inakuwa kubwa. Halafu muda atakaolala kesho yake anatakiwa aamke alfajiri kwenda kibaruani. Shabiki huyo ni lazima aamue kubaki mitaa yake ya nyumbani na kuangalia kwenye kibanda umiza.
Cha kushangaza wakati Bodi kwa sasa inaonekana kupenda sana mechi za usiku, Ulaya hasa kwenye Ligi za England wameonekana kupunguza sana mechi za usiku mnene.
Hispania nao wamefanikiwa sana, kwa sasa hata Watanzania wamekuwa wakishuhudia Barcelona na Real Madrid zikicheza hata saa mbili za usiku, tofauti na zamani mechi zao zinakuwa usimu mnene kuanzia saa nne, tano hadi sita.
Hii ina maana nao wamezipunguza mechi za usiku mwingi kutokana na masaa ya kwao. Bodi ya Ligi inapaswa kuliangalia hili.
Hakuna ulazima wa mechi za Dar es Salaam kuchezwa usiku hasa zile za kawaida sana. Labda za kimataifa na zile mechi muhimu na zenye mvuto tu.