Hongereni fomu 4, msiibe mitihani

15Nov 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hongereni fomu 4, msiibe mitihani

WATAHINIWA 566,840 nchi nzima, walianza mtihani kidato cha nne jana, huku Baraza la Mitihani la Tanzania -NECTA likitoa onyo kwa wanafunzi watakaojihusisha na udanganyifu katika mitihani hiyo.

Baraza linatoa onyo hilo kutokana na ukweli kwamba, kumekuwapo na tuhuma za wizi wa mitihani ambao imekuwa ikijitokeza kila mwaka kwenye baadhi ya shule za msingi sekondari zikihusisha wanafunzi na walimu. 

Ninadhani wanaojihusisha na wizi huo, wangeachana nao, kwani mtihani huo ni muhimu kwa wanafunzi na jamii, unapima umahiri wa wanafunzi katika masomo yote waliyojifunza kwa miaka minne. 

Baada ya mtihani, matokeo yake yanatumika katika uchaguzi wa wanafunzi wanaojiunga na elimu ya juu na fani mbalimbali, hivyo ni muhimu ufaulu wao ulingane na uwezo wao wa darasani. 

Ikumbukwe, wizi wa mitihani umekuwapo muda mrefu na unagharimu mustakabali wa maisha ya wanafunzi kutokana na adhabu zinazotolewa na NECTA kila mara yanapotangazwa matokeo. 

Adhabu yenyewe ni kufutwa kwa matokeo ya mtihani kwa shule nzima, badala ya kutoa adhabu aidha kwa wanafunzi waliothibitika kufanya udanganyifu huo kwa lengo la kufaulu. 

Hivyo, wale waliojiandaa kwa wizi au udanganyifu katika mtihani huo, ni vyema wasiwaponze wenzao, badala yake kila mwanafunzi atumie maarifa aliopewa na walimu kwa miaka minne aliokuwa shuleni. 

Udanganyifu wa aina yoyote katika mitihani kwa ngazi zote haukubaliki, ni vyema hatua zichukuliwe kwa wahusika, ingawa bahati mbaya wakati mwingine hata wasiohusika hujikuta wakihukumiwa. 

Niwakumbushe tu wale wenye nia ya kuiba mitihani kwamba, wanawaponza wenzao hasa pale baraza linapoamua kufutia shule matokeo na kumbe walioshiriki katika wizi na udanganyifu ni wachache. 

Ninadhani umefika wakati sasa mtindo wa kufutia matokeo shule nzima kama adhabu kwa wizi wa mitihani, iwe ni kwa wahusika tu, kwani sidhani kama inawezekana wanafunzi wote wakafanya udanganyifu. 

Kwa ujumla linapozungumzia suala la udanganyifu, wizi au kuvuja kwa mitihani, huo ni mnyororo mzima wa udanganyifu unaohusisha hata baadhi ya wasimamizi wasio waaminifu na wenye tamaa ya fedha. 

Wakati mwingine hata wamiliki wa shule au yeyote anayetengeneza mazingira ya wanafunzi kufanya udanganyifu ndani ya chumba cha mtihani. Hiyo ni kwa kuonyeshana majibu au maswali kufanyika nje ya chumba cha mtihani. 

Lakini baadhi ya wamiliki au viongozi wa shule huwa wanatuhumiwa kushawishi wasimamizi kuhusika kufanya udanganyifu, ambapo ukiangalia utabaini kuwa sababu zote hizo haziwahusishi wanafunzi moja kwa moja. 

Jambo la kusikitisha ni kwamba, athari za uamuzi wa kuwafutia zinawakumba wanafunzi moja kwa moja, hatua ambayo kwa namna moja au nyingine inaweza kuharibu malengo yao ya baadaye. 

Pamoja na yote hayo, jambo la muhimu kutambua ni kwamba wizi haufai katika mitihani, badala yake mwanafunzi anatakiwa kutumia akili yake itakayomwezesha kusonga mbele kielimu. 

Siyo siri kwamba, mwanafunzi anaweza kukwepa katika masomo iwapo atakuwa amefaulu kwa udanganyifu kwani sidhani kwamba huko anakoelekea ataendelea kuwa na watu wa kumbeba kwenye mitihani. 

Mtindo huo wa wizi wa mitihani unaweza kulifanya taifa likawa na wasomi wasio na manufaa katika jamii au kwa nchi yao, kwa kutokuwa na weledi wa kutosha kuhusu fani na ujuzi wa aina mbalimbali. 

Hivyo ni vyema wanafunzi wakaachwa wafanye mitihani, wafaulu kulingana na uwezo wao wa darasani, si kwa njia hizo ambazo zinaweza kuwaingiza kwenye matatizo na kusababisha kufutiwa matokeo.

Niwatakie kila la heri wanafunzi mnaofanya mtihani wa kidato cha nne, lakini mjaribu kuepuka njia zozote za udanganyifu na wizi wa mitihani, kwani ni sawa na kujiharibia.