Simba, Yanga, Geita kazi CAF haijamalizika

17Sep 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Simba, Yanga, Geita kazi CAF haijamalizika

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara,Yanga leo usiku watakuwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kucheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zalan FC ya Sudan Kusini, ...

...huku wawakilishi wengine katika michuano ya Kombe la Shirikisho, Geita Gold wao wakiivaa Hilal Alsahili kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Simba, kesho nayo itakuwa dimbani katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nyasa Big Bullets kutoka Malawi.

Mechi zote ni marudiano ya michuano hiyo ya kimataifa, Yanga ikishinda mabao 4-0 kwenye mechi ya kwanza iliyochezwa hapa hapa nchini, Simba ikishinda magoli 2-0 ugenini Malawi, na Geita Gold ikipoteza kwa bao 1-0 huko Sudan.

Ukiangalia hapa kwa kiasi kikubwa ni kwamba timu za Tanzania zipo katika mazingira mazuri ya kusonga mbele kwenye hatua ya raundi ya kwanza ya michuano hiyo ya kimataifa.

Binafsi ninaziombea timu zote za Tanzania zifanye vyema kwenye michuano hiyo kwa sababu itakuwa ni faida kubwa wa soka la Tanzania.

Tukianza katika Ligi ya Mabingwa Afrika kama Simba na Yanga zitavuka hatua hii, ina maana zina uhakika wa kuendelea tena mbele.

Kwa sababu kama zitashinda kwenye mechi za raundi ya kwanza, zitaingia kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga kama itapita itasubiri mshindi kati ya St George ya Ethiopia na Al Hilal ya Sudan, huku Simba kama itaitoa Nyasa Big Bullets, itasubiri mbabe wa mechi kati ya Red Arrows ya Zambia na Primeiro de Agosto ya Angola.

Lakini pia kama zitatolewa kwenye hatua hii ya raundi ya kwanza, zitashuka kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwenda kwenye hatua ya mchujo, kutafuta kutinga hatua ya makundi ya kombe hilo.

Hii inaonyesha kazi kubwa ambayo Simba na Yanga zinatakiwa kufanya kwanza ni kupita kwenye hatua hii kwanza.

Yoyote itakayotolewa hapa, ni kwamba itabidi kusubiri tena mwakani na si vinginevyo.

Hivi karibuni Rais wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), Wallace Karia alisema anachotaka safari hii ni kuona timu za Tanzania zinafanya vema kwenye michuano ya kimataifa ili kuzilinda nafasi nne za uwakilishi.

Kwa miaka ya hivi karibuni tumeona Tanzania ikitoa wawakilishi wawili, bingwa na mshindi wa pili kucheza Ligi ya Mabingwa, mshindi wa tatu na bingwa wa Kombe la FA wanaopata tiketio ya kucheza Kombe la Shirikisho.

Tanzania imeipita mpaka Zambia, nchi ambayo ina historia kubwa kwenye soka, lakini mwaka huu inatoa mwakilishi mmoja tu kwenye Ligi ya Mabingwa na mshindi wa pili anayecheza Kombe la Shirikisho.

Kwa sababu hiyo ni lazima Karia atoa rai ya kuzilinda nafasi hizo ili Tanzania isirudi tena nyuma kwa sababu zinapatikana kutokana na timu zinazoshiriki kufanya vizuri.

Imefika wakati sasa Watanzania kuacha mambo yaliyopitwa na wakati ya kuwasaidia wageni ili kuifunga timu mwenyeji.

Tumekuwa tukiona huko nyuma, viashiria vya baadhi ya timu kuzipokea timu pinzani zinazocheza na timu za hapa hapa, kwa sababu tu ya kisingizio cha utani wa jadi, hii si sahihi kabisa.

Mbali na hilo, tumekuwa tukiona baadhi ya viongozi wa klabu hapa nchini wakitoa mbinu kwa wageni jinsi gani ya kufanya ili kuepuka kufungwa kwa kile wanachodai kuwafundisha kuepuka hujuma.

Kwenye soka la kisasa haya mambo hayana nafasi. Cha ajabu ni kwamba huko nyuma hakukuwa na vitu kama hivyo.

Yanga ikicheza mechi ya kimataifa, mashabiki wa Simba watakwenda tu kutazama, kupongeza kama wenzao watashinda na kuwazodoa kama wakifungwa. Na upande wa pili ni hivyo hivyo. Lakini hatukuona timu zikifanyiana hujuma, mmoja ufungwe ili asimcheke mwenzake.

Hili limeanza kwenye miaka ya karibuni kwenye kipindi ambacho tunadhani soka likua kuliko zamani. Inashikitisha sana.

Ifike wakati sasa kila timu iangalie mechi zake, inacheza, inashindaje na inasongaje mbele, badala ya kutumia nguvu nyingi kutaka kuhujumu mechi za kimataifa za timu nyingine.

Nadhani kufanya hivi ni sawa tu na kuhujumu maendeleo ya soka la Tanzania na nchi kwa ujumla kwa sababu kama timu hizi zikisonga mbele licha ya nchi kupata sifa, lakini kuna vitu vingi ambavyo nchi inanufaika navyo pamoja na Shirikisho la Soka Nchini.

Klabu ziwe na wivu wa maendeleo kuangalia zingine zimefanya nini na kupita wapi ili zifuate, na siyo kutaka kuzishusha kwa mtindo wa 'tukose wote'.

Narudia tena kutoa rai kama ile ya Karia kuzitakiwa timu zote kila la heri, lakini kuacha tabia ya kuhujuliama kwa sababu siyo kama inasababisha timu hiyo kufungwa tu, lakini pia inadumaza soka la Tanzania kwa kuonekana timu zake labda si imara, kumbe kuna mchezo mchafu unafanywa wa kudhoofisha nguvu ya timu zingine kwenye mechi za kimataifa.

Kama ikitokea, TFF ilichukulie hili kama hujuma kwa soka la Tanzania.