Ni wakati sahihi,elimu lishe kupamba moto kufuta shida udumavu

16Sep 2022
Pilly Kigome
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ni wakati sahihi,elimu lishe kupamba moto kufuta shida udumavu

WAKATI tulikuwa masomoni katika umri mdogo tulifunzwa mengi kuhusu afya ya binadamu. Eneo mojawapo ambalo tulikaririshwa na kueleweshwa ni kuhusu mlo na aina ya vyakula kwamba vipo vya aina tatu; vinavyojenga mwili, kuulinda na mwisho kingine kinachotia nguvu mwilini.

Ni elimu iliyoenda sambamba na kampeni za kupeleka watoto masomoni shule.Naam! Ilikuwa sehemu ya mikakati ya maendeleo, baada ya kupatikana uhuru wa nchi, nasi tukiwa ndiyo bado wadogo sana.

Mitaala ya shule ilienda sambamba nasi, somo la Sayansi Kimu lilitunoa kuzingatia afya  yetu, basi ndani yake elimu lishe na ya kujijali ikaenda sambamba kuwa sehemu ya maisha yetu

Tumekuwa wakubwa hata tukatua kliniki, nako tukakuta nadharia hiyo hiyo na masomo yake. Tuliohudhuria hapo, miongoni mwa mambo nyeti tukajifunza ni lishe bora kwa mama, mtoto na familia.

Hata kwenye burudani nje ya kliniki na shule, nakumbuka mwanamuziki maarufu Mbaraka Mwinshehe Mwaruka alishawahi kutunga wimbo maalum wa muziki, akiainisha aina ya vyakula muhimu makundi matatu, ambazo zimeanishwa juu. Pia, ndio ilikuwa sehemu ya sera ya taifa.

Hivyo kwa ujumla wake, ndio inapoibua umuhimu mkubwa wa kutoa elimu ya lishe ngazi ya jamii kote nchini, ili jamii hiyo iweze kujitambua ipasavyo na hata kushiriki kupunguza, kama sio kuondoa magonjwa yanayoweza kupatikana kuhusiana na tatizo la lishe duni.Nikiri katika kizazi hicho tuliona mabadiliko.

Hivi sasa nimesikia namna malalamiko ya kitaifa kwa asimilia kubwa lishe duni au isiyo na mpangilio sahihi, unaangukia katika kuwaweka watoto wadogo katika kilio cha shida ya udumavu.

Mikoa kama Dar es Salaam na Shinyanga, hivi sasa iko katika orodha ya vinara wa udumavu ambao chanzo kikuu ni lishe duni. Vivyo hivyo, inasikitisha katika baadhi ya mikoa mingine kama Mbeya inataabika kwa udumavu, wakati wana utajiri wa vyakula. Huwa najiuliza shida ni nini?

Hapo linanijia jibu la kwanza elimu na hoja kwamba, sasa ni wakati wetu kujihadhari kuanza kutoa elimu ya lishe kila mmoja kwa nafasi yake na aelimishe na aendeleze, ili jamii iweze kujitambua kuhusiana na ulaji vyakula kwa usahihi kukabiliana na magonjwa yanayoepukika.

Tatizo la upungufu wa damu linaonekana kuwa kubwa katika jamii na moja ya sababu ni ukosefu wa virutubisho lishe muhimu katika mlo.

Ipo sababu kwa serikali kutoa elimu kwa jamii zaidi ya mahali tuliko sasa. Iwe kuanzia ngazi ya kata hadi taifa kwa ujumla, ili wananchi waweze kujitambua na kuanza kukabiliana na tatizo hili.

Kutoka kwa jamii, najua kuna shida ya mwamko wa ulaji wa vyakula na makundi yake. Wapo ambao wanakiri kwa baadhi ya makundi ya vyakula na kusahau ulaji makundi yanayoleta virutubisho mwilini.

Ushuhuda wa jamii unaothibitika, unaonyesha wengi wao hawana mwamko wa elimu ya lishe kwa ujumla katika upande wa afya na kuchunguza makundi ya vyakula kwa usahihi na umuhimu na kazi zake mwilini.

Naamini, jamii ikijitambua kikamilifu juu ya umuhimu wa lishe, ni wazi itaweza kupunguza wimbi  la tatizo la upungufu wa damu ambalo kwa kiasi kikubwa linatokana na tatizo la lishe duni.