Ni wakati sasa kila mmoja wetu aijue kansa kwa ufasaha, ajihami 

15Sep 2022
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ni wakati sasa kila mmoja wetu aijue kansa kwa ufasaha, ajihami 

NI muhimu elimu iendelee  kutolewa kwa jamii, ili iweze kujikinga wasipate ugonjwa wa saratani, ambao huko wazi inaonekana ni tatizo kwa jamii, hata kuchangia vifo kwa watu wengi.

Sasa kuna swali la awali, nini kifanyike kujinusuru nayo? Iko bayana kwamba, kunatakiwa kwanza elimu ya kina iendelee kutolewa kwa jamii, kwani inaonekana ndani ya jamii hakujakuwapo elimu kwa usahihi kuchangia kupanuka kwake.

Ushuhuda wa jamii, kuna shida ya mwamko wa kuchunguza afya kwa usahihi, kwani hatua hiyo ingewasaidia kutambua maradhi yanayowasibu na hata wakachukua hatua za kujitibabu ya awali. Kuchelewa kujitambua imechangia mgonjwa kufika kwenye matibabu ameshachelewa sana.

Hivi karibuni, serikali imesema saratani nchini imeendelea kukua kwa kasi, pia ikisababisha vifo vya wengi duniani. Hapo tena inaibua msukumo wa haja ya elimu ya ugonjwa iendelee kutolewa ndani ya jamii, kuhusu namna ya kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Makamu wa Rais, Dk. Phillip Mpango, mara baada ya kuzindua jengo la Huduma za Saratani katika Hospitali ya Rufani Kanda, Bugando Mwanza, amelitamka hilo akinena takwimu zinaonyesha nchini kila mwaka, kuna watu 42,000 hupata ugonjwa wa saratani.

Hapo anafafanua kuwa serikali imewekeza na kutekeleza hatua mbalimbali za kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza, ukiwamo mkakati wa kupunguza vihatarishi vya magonjwa yasiyoambukiza kwa kutoa elimu zaidi ndani ya jamii.

 Mengine nakumbuka ametaja, ni haja ya kuchukua hatua stahiki za kuboresha mtindo wa maisha katika jamii, akizingatia ulaji unaofaa, kupunguza matumizi ya pombe, kuacha matumizi ya tumbaku, kufanya mazoezi na kuepuka tabia ya kutojishughulisha.

Dk.Mpango, anawataka watu kuchunguza kila mara afya zao, ili kubaini mapema endapo watakutwa na saratani na maradhi mengine katika hatua ya awali, basi watapata tiba na kupona kabisa.

Mwaka 2021, kuna wanawake 365,164 waliofanyiwa uchunguzi, kati yao 8,762 walibainika kuwa na dalili za awali za saratani ya shingo ya kizazi.

Ndio eneo ambalo Dk.Mpango, anaitaka jamii iachane na dhana potofu ya saratani kuhusishwa na ushirikina na hapo yuko wazi akiwaomba wazazi na jamii kwa ujumla, kuhamasisha chanjo dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi, inaongoza kuwaathiri kina mama wengi.

Ndani yake, mkuu huyo wa nchi anabainisha pongezi zake kwa uongozi wa Hospitali ya Rufani ya Kanda Bugando, kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali na ikisaidia kutoa huduma za kijamii.

Anatamka: “Nichukue fursa hii kwa niaba ya Serikali kulipongeza na kulishukuru Kanisa Katoliki na taasisi zetu zote za dini hapa nchini kwa kuunga mkono juhudi za serikali na kutoa mchango mkubwa sana kwa ustawi wa taifa letu kiroho, kiuchumi na kijami."

Vilevile, raha ya mchango huo ukaendana na hoja ya

 Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, anayechangia kwamba, serikali inaendelea kushirikiana na hospitali hiyo kuboresha huduma, miundombinu, ununuzi vifaa tiba, mashine na kuajiri watumishi wa kuhudumia tiba.

 

Kwa mujibu wa taarifa za kiserikali , imeshatoa shilingi bilioni 1.9 kuchangia ujenzi wa huduma za saratani katika Hospitali ya Rufani Kanda ya Bugando, kununua mashine iitwayo MRI yenye thamani ya shilingi bilioni 2.2 inayotumika katika uchunguzi,

 

Nikirejea ufafanuzi huo ni kwamba serikali imejenga kiwanda cha mionzi dawa kwa ajili ya tiba kwa wagonjwa wa saratani nchini, ili kuwezesha upatikanaji huduma bora za matibabu na kwa haraka zaidi kitaifa.

 

Ni aina ya ujenzi  unaofanyika ndani ya

Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dar ss Salaam, ikitufungua kwamba hakuna haja ya mtu kwenda nje ya nchi, kama vile Afrika ya Kusini, kufuata mionzi dawa. Kila kitu sasa kinapatikana nchini.

 

Kutoka kwake Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Dk. Fabian Massaga, hospitali hiyo inahudumia watu zaidi ya milioni 17 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa na maeneo mengine jirani, hali kadhalika kwa wageni watokao nje ya mipaka ya nchi.

Top of Form

Bottom of Form