Waamuzi wafanyie kazi ushauri wa Bodi ya Ligi

19Sep 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Waamuzi wafanyie kazi ushauri wa Bodi ya Ligi

AKIZUNGUMZA na Kamati ya Waamuzi jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi (TPLB), Almasi Kasongo, alisema baadhi ya waamuzi wanaochezesha mechi za Ligi Kuu...

...wana mapungufu ya vitu kadhaa ambavyo kama wakijirekebisha watakuwa ni bora na wala hawatokuwa wakizungumzwa na kulaumiwa mara kwa mara.

Kwa niaba ya Bodi ya Ligi, Kasongo akakumbusha kuwa ili mwamuzi awe bora kuna vitu lazima awe navyo, lakini baadhi yao wanavikosa hivyo kusababisha malalamiko mengi kwenye baadhi ya mechi za Ligi Kuu.

Akazitaja sifa hizo kuwa ni mwendelezo mzuri wa uchezeshaji kwa dakika zote 90 au mechi tofauti, ujasiri, ukosefu wa mawasiliano na mwisho ni akili ya kuzaliwa. Alisema malalamiko mengi yanayojitokeza kwenye mechi mbalimbali ni mapungufu ya vitu hivyo alivyoviainisha.

"Mwamuzi ni kama hakimu au jaji, ni lazima kwanza uwe jasiri, na mwamuzi mzuri anapimwa kwa vitu kama hivyo. Kuna baadhi ya waamuzi hapa wamekariri kuwa penalti haitoki dakika ya 94, au dakika ya kwanza, huko ni kukosa ujasiri, penalti inatoka dakika yoyote ile hata 97 na kadi nyekundu inatoka muda wowote ule na anaonyeshwa yeyote yule, usiangalie huyu nani nimwonyeshe au huyu ni staa wa timu unaogopa, unajiuliza nikimpa huyu mwezi mzima nitakuwa na amani kweli, unatakiwa utoe bila kujali ni nani, hivyo ni sifa ya ujasiri anayotakiwa kuwa nayo mwamuzi," akasema Kasongo.

Ni kweli kabisa alichokisema Kasongo hapa. Kumekuwa na tabia ya baadhi ya waamuzi wa kizazi hiki kutoa maamuzi hasa kwa timu kubwa zenye mashabiki wengi hususan wa timu za Simba na Yanga.

Wengi wa waamuzi wanaweza kutoa kadi nyekundu au penalti dhahiri kwa timu zinazoitwa au kujiita ndogo, lakini inakuwa ngumu sana kufanya hivyo inapotokea kosa limefanyika kwa timu hizo mbili.

Hii tabia huwa inawapa nguvu baadhi ya viongozi wa Azam FC kudai kuwa kuna maeneo huwa hawatendewi haki, au hawapati faida ya makosa ya kibinadamu kama inavyokuwa kwa timu za Simba na Yanga.

Wanadai makosa mengi ya kibinadamu ya waamuzi hulalia kwa timu yao na timu zingine, lakini huwezi kukuta kwa vigogo hao, ndiyo maana wanaukosa ubingwa.

Mwamuzi anayeona kufanya maamuzi sahihi kwa kuogopa kuwakera mashabiki, kusemwa kwenye mitandao ya kijamii au kutishiwa hana chembe ya ujasiri, hivyo hafai kuwa mwamuzi kwa kuwa atakuwa akizipa adhabu timu dhaifu tu zisizokuwa na uwezo wa kusema au kwa kusemea.

"Kwenye vikao vya kamati hakuna timu ambayo haijapigwa faini kwa mashabiki wake kurusha chupa na mawe, tumefuatilia msingi wake, imegundulika kuwa waamuzi wanakosa muendelezo mzuri wa uchezeshaji na maamuzi. Kosa hilo hilo linafanywa na timu A anaonya, likifanywa na timu B anatoa njano, lingine likifanywa na timu A anatoa njano, lakini hilo hilo likifanywa na timu B anatoa nyekundu.

"Unawafanya mashabiki kuwa na hasira kwa sababu wapo uwanjani na wanaona matukio yote unavyoamua, kwa nini kosa moja utoe maamuzi tofauti kwa timu hii na hii? Akahoji Ofisa Mtendaji Mkuu huyo."

Hapa ukiangalia ni kwamba msingi wake ni mmoja tu. Ule ule wa kutokuwa na ujasiri. Mchezaji wa Simba akifanya kosa ataonywa, hilo hilo akifanya wa KMC atapewa njano,  kuna kosa akifanya wa Yanga anapewa kadi ya njano, lakini linafanana hivyo hivyo, wa Dodoma Jiji atapewa nyekundu. Ni woga ule ule aliosema Kasongo ndiyo unasababisha kutokuwa na mwendelezo mzuri wa uchezeshaji.

Mbali na kutumia akili ya kuzaliwa, Kasongo alibainisha kuwa kuna kesi za waamuzi wanaopelekwa kwenye kamati, lakini ukiziangalia unakuta tatizo ni dogo tu, kutokuwa na mawasiliano.

Ni kweli, mawasiliano ni kitu muhimu sana kwenye nyanja yoyote ile, hata kwenye ngazi ya familia tu. Kuna makosa utayaona mwamuzi msaidizi anatakiwa kumsaidia mwamuzi lakini wa kati yeye 'anauchuna' tu na kumwachia kazi kubwa mwenzake kiasi kwamba likitokea tatizo yeye anakuwa kama vile amejiondoa kwenye lawama.

Mwamuzi wa kati na wasaidizi wake wanatakiwa wawe na mawasiliano, huku maeneo yote ambao msaidizi anayatazama awe tayari kumsaidia mwenzake ili kumrahisishia kazi.

Ni baadhi ya waamuzi wasaidizi wachache tu wakiongozwa na Frank Komba na Janeth Balama mara kwa mara ameonekana kufanya kazi kubwa ya kuwasaidia waamuzi kwenye maeneo ambayo wao si rahisi kung'amua, na wamekuwa wakiifanya kwa usahihi mkubwa.

Hawa wanasababisha waamuzi kuchezesha wakiwa hawana presha kwa sababu wanajua wana wasaidizi wazuri na si wa kunyoosha tu kibendera mpira ukitoka, au kuwekwa kona.

Nadhani imefika wakati alichokiona Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPLB kwa niaba ya Bodi ya Ligi kifanyiwe kazi na waamuzi wote wa Ligi Kuu Tanzania Bara ili kuondoa malalamiko yasiyo ya lazima.