Lakini pia polisi kwa namna yoyote ile wanatakiwa kuwa rafiki wa karibu na raia wema popote wanapokutana ili kupanga na kuweka mikakati ya kuhakikisha wanadumisha amani na ulinzi wa mali za raia.
Hata hivyo, jukumu hilo sasa naona kwa bahati mbaya linataka kuwekwa pembeni na baadhi ya Polisi wachache sana katika wilaya ya kipolisi ya Wazo, ambayo inahudumia kituo kikubwa cha Kawe Wilaya ya Kinondoni na kituo kidogo cha Goba Wilaya ya Ubungo.
Kwa muda mrefu wakazi wa Goba walikuwa wanaomba usiku na mchana kupatiwa kituo cha Polisi pamoja na ulinzi muda wote kutokana na matukio yaliyokuwapo siku za nyuma.
Kwa kutambua hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Saimoni Sirro alipitisha hilo na sasa Goba kuna kituo kidogo cha Polisi ambacho kinakuwa na askari saa 24 huku magari ya doria yakipita muda wote.
Hilo ni jambo jema sana na ambalo naamini kila raia mwema alilishangilia kwa mikono miwili kwa kuwa matukio ya uhalifu yalikuwa yamezidi.
Jambo ambalo linakuwa kero kwa raia hawa hususani eneo la Goba ni pale askari wale waliotoka mafunzoni huenda kwa bahati mbaya kutojua majukumu yao.
Nimeshuhudia vitendo vya ukiukwaji wanavyofanyia waendesha Bodaboda na wananchi wema wanaochelewa kurudi kazini.
Kwa mfano pale Goba mwisho mtu akichelewa katika shughuli zake za uzalishaji ikafika saa tano, pindi anaposhuka kwenye daladala lazima askari wamkamate, labda wawe hawajamuona ama wawe hawajafika.
Kibaya zaidi wakimkamata hawataki atoe maelezo yoyote kwa nini yupo pale kwa muda ule, badala yake askari hao wanamkamata na kuita gari la doria na kumpelea kituo cha Kawe.
Lakini pia askari hawa ambao nimesema ni wachache ikifika saa tano usiku wanasimama barabarani na kusimamisha kila gari inayopita pamoja na kukamata pikipiki zote zinazokuwapo Goba mwisho kwa wakati huo.
Mbaya zaidi askari hawa hawampi raia mwema nafasi ya kujieleza hata kama amepata dharura unakwenda kumuona mgonjwa inabidi uogope kupita mbele yao.
Katika mazingira hayo askari hawa wanatengeneza mfumo ambao unamfanya raia amuogope polisi badala ya kumuona kama rafiki ambaye analinda mali zake pamoja na usalama wake wa maisha.
Kwa mfano Desemba 12, askari hao walimkamata mwendesha bodaboda, Athuman Baruti na akiwa amempakia abiria saa tatu usiku, na katika mabishano wakapiga risasi juu ili kumtisha na walipofanikiwa kumweka chini ya ulinzi walimpeleka kituo cha Kawe na kumfungulia jalada la ujambazi.
Huu ni mfano mmoja lakini ipo mingi na kibaya zaidi askari hawa wameacha kufanya jukumu lao la msingi la kulinda raia na mali zao badala yake wanapambana na raia wema ama wanaotoka kazini wakiwa wamechelewa,ama bodaboda wema, ama kukamata wenye Bar.
Wafanyabiashara wa Bar wanafanya kazi ile kwa mujibu wa sheria na leseni za biashara zao, lakini jambo la ajabu ni pale gari lao la doria kwenda kuegeshwa nje ya Bar ama sehemu ya jirani kwa lengo la kuvia wafanyakazi wazidi muda hata kwa dakika tano ili wawakamate.
Kibaya zaidi wakiwakamata wanawadai rushwa ili wawachie vinginevyo wanawatisha kuwapeleka kituo cha Kawe.
Huenda RPC Kinondoni halijui hili pamoja na Kamanda Sirro, lakini hiyo ndiyo hali halisi na bughudha zinazowakumba wakazi wa Goba.
Kuna haja viongozi wa Polisi kuweka mikakati ya kuhakikisha askari hawa wanajikita katika majukumu yao ya msingi ya kulinda raia na mali zao pamoja na kupambana na uhalifu badala ya kujikita kuwabughudhi raia wema.
Nasema hivi kwa sababu huenda baadhi ni wageni na kazi hizi ama wale wenyeji wamejisahau na kujikuta wakifanya mambo ambayo siyo sehemu ya kazi zao.
Ulinzi wa raia na mali zao unahitaji ushirikiano badala ya kutishana kwa kuwa wao wamepewa nguvu ya kukamata mtu na kumfikisha kituoni.
Lakini pia ushirikiano kati ya raia wema na polisi unasaidia kufichua wahalifu ambao wanaishi katika jamii tunayoishi kila.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni bado unao muda wa kupanga vijana wako na kuwasaidia ili waweze kutimiza majukumu yao vizuri bila kuwa kero kwa raia wema, raia wema waache waendelee kufurahia uwepo wa askari mitaani kwao.