Taasisi za umma zisizo na tija zifutwe

14Dec 2016
Richard Makore
Nipashe
Mjadala
Taasisi za umma zisizo na tija zifutwe

MOJA ya hatua kubwa na ya haraka aliyochukua Rais John Magufuli alipoingia madarakani ni kuweka mikakati maalum ya kubana matumizi pamoja na kupambana na ufisadi kwa vitendo.

Ni mkakati muhimu ambao unalenga kulisaidia taifa kupiga hatua za kimaendeleo pamoja na kuhakikisha kila mwananchi anafaidi matunda ya nchi yake.

Mpango huu wa Rais ili uweze kufanikiwa ni lazima uzingatie baadhi ya mambo muhimu ikiwamo kuhakikisha anajenga mfumo ndani ya serikali ambao utaogopwa na kila mtumishi wa umma ama kiongozi yoyote atakayekuja.

Lakini sambamba na hilo kuna haja Rais Magufuli kupunguza ukubwa wa taasisi za serikali ambazo nazo zinatumia fedha nyingi za walipa kodi.

Kama mpango huu mzuri wa Rais Magufuli hautakuwa na mkakati wa kutengeneza mfumo unaoogopwa na watumishi wa umma inaweza kuwa kazi bure.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais anachaguliwa kila baada ya miaka mitano na anaruhusiwa kuongoza katika vipindi viwili kama ataendelea kuchaguliwa.

Kwa namna yoyote itakavyokuwa Rais Magufuli ataondoka madarakani baada ya mwaka 2025 kama mwaka 2020 atapewa ridhaa nyingine ya kuwaongoza Watanzania.

Kutokana na hali hiyo ili kulinda haya mambo mazuri aliyoanza kuyafanya mpaka sasa ni lazima ahakikishe anatumia wataalamu wake kuweka mikakati ya kuweka mfumo mzuri ambao kila mtu ataufuata au kama atashindwa kuufuata basi awe anauogopa.

Kwa mfano, hivi sasa watendaji wa umma wameanza kuogopa fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya miradi mbalimbali, lakini hawa watumishi hawafanyi hivyo kwa kuogopa mfumo bali wanafanya hivyo kwa kuwa wanamuogopa Rais Magufuli.

Kabla ya Rais Magufuli kuingia madarakani yeye mwenyewe alikiri kwamba kulikuwa na mambo ya ovyo yaliyokuwa yakifanyika ndani ya serikali na ilikuwa inaonekana ni jambo la kawaida.

Haya mambo ya ovyo ambayo Rais Magufuli amekuwa akiyasema mara kwa mara yalikuwa yakifanyika licha ya kuwapo sheria nzuri zinazozuia vitendo vya rushwa kwa watumishi wa umma.

Mbali na Rais kuhakikisha anaweka mfumo wa kuogopwa, lakini pia kuna haja ya kupunguza taasisi mbalimbali za umma.

Kwa sasa kila wizara inazo taasisi kadhaa zilizo chini yake na zote zinaoongoza na wakurugenzi wake, ambazo zinatumia fedha za walipa kodi kupitia bajeti zinazotengewa na serikali.

Sina sababu ya kutaja taasisi za umma idadi yake, lakini ni ukweli ambao upo wazi kwamba zinatumia fedha nyingi za kodi na kama kungekuwa na uwezekano hizi zingebadilishwa na kuwa vitengo ndani ya wizara husika.

Kiongozi wa taasisi ya umma anatumia gari la gharama kama analotumia Waziri, anakuwa na dereva wake, anakuwa na msaidizi wake pamoja na kutengewa bajeti ya kuhudumia familia yake kuanzia matibabu, gharama za maji, umeme, ulinzi na wengine kulipia hata ada za watoto wake.

Najua taasisi hizi zilianzishwa kwa mujibu wa sheria ya Bunge, lakini kumbuka sheria zinaweza kubadilishwa kama kutakuwa na utashi na dhamira njema ya kuhakikisha serikali inabana matumizi yake.

Ndani ya serikali kuna taasisi zingine hata mtu wa mtaani akiulizwa hajawahi kuisikia na wala hajui hata kazi zake za msingi, lakini inaongozwa na Mkurugenzi na watendaji walio chini yake.

Kuna taasisi nyeti kama Tanesco, Bandari na nyingine chache ambazo huwezi kuzigusa kutokana na unyeti wake katika uchumi wa nchi hii.

Lakini kuna taasisi nyingine ambazo zinaweza kuwa vitengo ndani ya wizara na kuongozwa na watu wasiozidi watano na bado kila kitu kikaenda sawa.

Sitaki kuzitaja taasisi hizo, lakini cha msingi sasa umefika wakati wa kuziangalia ili kuona bajeti zake kwa mwaka na umuhimu wa kazi zake katika kuchangia maendeleo ya nchi.

Kama taasisi haizalishi chochote mwaka mzima badala yake inategemea fedha za serikali nadhani hili ni jipu na ingekuwa vizuri ikatumbuliwa ili kuwaondolea mzigo Watanzania.

Lakini pia kuna vitu viliwahi kuanzishwa na serikali kama sehemu ya watu kujipatia fedha na mpaka leo vipo ingawa kihalisia havijawahi kuleta tija kwa wananchi.

Kwa mfano kiliwahi kuanzishwa kitu wakati huo kikagharimu fedha nyingi za wananchi kwa kuandaa semina huku ukipigiwa debe kwamba ulikuja kupunguza umaskini.

Hata hivyo, mpaka leoo ukiuliza ni wananchi wangapi walifaidika na mpango huu unaweza usionyeshwe kwa sababu fedha zake ziliishia kwa wajanja wachache.

Juzi Rais mwenyewe katangaza kwamba kuna familia hewa zinazohudumiwa na TASAF kupitia fedha zinazotolewa na serikali na mfuko huu ni miongoni mwa maeneo ambayo yamekuwa yakipigiwa debe kwamba unasaidia kupambana na umaskini.

Siyo lengo la mjadala huu kuonyesha namna bora ya kuunda serikali, lakini kwa mtazamo huu chanya wa Rais Magufuli haya yanatakiwa kuangaliwa badala ya kuendelea kuishi kwa mazoea.

Taasisi za umma ni muhimu kwa maendeleo ya nchi, lakini kuna haja ya kubakiza zile ambazo zina tija na zile ambazo zilianzishwa kwa ajili ya kupeana ulaji zinabadilishwe na kuwa vitengo ndani ya wizara husika.