Lakini wakati mwaka 2016 wananchi wakilalamikia ‘mifuko kutoboka’ nakumbuka Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu kupitia vyombo vya habari aliutangazia umma kuwa hadi tulipofikia robo ya kwanza ya mwaka 2016, ukuaji Pato la Taifa ulikadiriwa kuongezeka kwa asilimia 5.5, ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 5.7 katika kipindi hicho cha mwaka 2015.
Ni kauli mbili zilizogongana kati ya kiongozi huyo mkubwa wa taasisi za fedha nchini na wananchi.
Kundi kubwa na Watanzania, wafanyabishara, wakulima na wanasiasa wote kwa pamoja walikuwa wanalalamika kuwa fedha zimepotea mitaani.
Hakika! Mwaka 2016, kilio kikubwa kilikuwa ni fedha kuadimika.
Kilio hicho cha fedha kuadimika kilimfikia Rais John Magufuli, kwa maana kila aliyekuwa analia alikuwa anailalamikia Serikali kuwa, ndiyo iliyokuwa imesababisha hali hiyo.
Nakumbuka Rais Magufuli alipokuwa anahutubia sehemu mbalimbali alieleza kuwa fedha hazijaadimika mitaani bali watu walikuwa wanapata fedha kwa njia zisizo halali, hivyo Serikali imeziba mianya hiyo na ndiyo sababu watu hao wanalalamika kuwa fedha hazipo.
Pia, Rais Magufuli aliwahi kueleza kuwa watu wanatakiwa kufanya kazi ili wapate fedha, wasifanye ‘dili’ bali wafanye kazi za uhalali na fedha watapata.
Ni kweli, namuunga mkono Rais Magufuli kwa kauli yake kuwa watu wafanye kazi halali ili wapate pesa za halali.
Mwaka 2017 tunaotarajia kuuanza siku chache zijazo watu wanapaswa kujituma katika kufanya kazi za uhalali, kazi ambazo zinatambuliwa na Serikali, kazi ambazo zitaiongezea Serikali mapato, kazi ambazo zinatambulika na watu wote.
Mwaka 2017 uwe mwaka wa watu kujishughulisha na kuiwezesha nchi kukuza uchumi wa taifa.
Endapo mwaka 2017 kila mtu atafanya kazi kwa kujituma, nina imani nchi nayo itapiga hatua ya kimaendeleo, na kila Mtanzania atanufaika na kuvuna matunda ya nchi.
Wafanyabiashara watanufaika kihalali kupitia kipato halali cha kuwawezesha kuongeza faida na kuimarisha biashara zao.
Wananchi nao watanufaika kwa kulindwa ajira zao.
Mifuko ya hifadhi ya jamii itanufaika kwa kuwa na wanachama wa kutosha walio kwenye ajira za uhakika.
Serikali itanufaika kwa kupunguziwa changamoto ya ajira, kuongezeka kwa makusanyo ya kodi ya mapato kupitia shughuli na biashara mbalimbali kama za hoteli na mishahara ya wafanyakazi nao itaongezeka, hivyo mzunguko wa fedha.
Kwa upande wa Serikali, wananchi wangependa kuona mwaka 2017 unakuwa mwaka wa ujenzi wa miundombinu, kama ya barabara za lami, madaraja na reli ili kuwezesha sekta ya usafirishaji kuwa safi.
Pia mwaka 2017, serikali inapaswa kuboresha huduma za kijamii, hospitali, shule, upatikanaji wa maji safi kwa upana zaidi, kwa kutoa kipaumbele.
Ahadi ya serikali ya ujenzi wa Zahanati kwa kila kijiji, na kituo cha Afya kila kata na kuwa na Hospitali kila halmashauri, ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma za afya popote alipo basi ianze kutekelezwa mwaka 2017.
Wabunge waliotoa ahadi kwa wananchi wakati wanafanya kampeni katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, watimize ahadi zao, wasisubiri hadi miaka yao ya uongozi ikaribie kumalizika ndipo wanatekeleza.
Ulinzi na usalama uimarishwe kwa wananchi mwaka 2017, matukio ya wananchi kuvamiwa pindi wanapofanya huduma za kifedha katika taasisi za fedha yadhibitiwe.
Jeshi la Polisi lihakikishe linaimarisha doria katika maeneo yote.
Mwaka 2017, uwe mwaka wa kutokomeza ajali barabarani.
Jeshi la Polisi kupitia kikosi cha usalama barabarani kihakikishe ajali zinatokomezwa kwa asilimia 99, madereva wazembe wapewe adhabu kali kwa maana wamekuwa wakisababisha vifo vya mamia ya Watanzaia, huku wengine wakiwa vilema wa maisha.
Mwaka 2017 pia uwe mwaka wa kujituma kwa kila mtu, Mkulima aongeze juhudi ya uzalishaji, mfanyabiashara awajibike kisawasawa katika kufanya bishara halali na siyo kukwepa kodi.
Mwaka 2017 uwe mwaka wa amani na utulivu, wanasiasa hususani wapinzani waelewane na Serikali na kupatana, wawe ndugu.
Tusione wala kusikia yale maneno au misamiati ya kutisha ambayo itawaogopesha wananchi kwenda makazini.
Kila mtu auone mwaka 2017 kama mwaka wa maendeleo kwake, uwe mwaka wa kusukuma gurudumu la maendeleo katika sekta zote muhimu, mawaziri wote wahakikishe wanasimamia wizara zao vizuri.
Watanzania wote bila ya kubagua rangi, dini wala kabila, mwaka 2017 tunapaswa kushikamana kwa pamoja kama ndugu na kuijenga nchi yetu, kwa maana hakuna mtu atakayetoka nje ya nchi kuja kutujengea nchi yetu.
Kwa heri mwaka 2016, karibu mwaka 2017, Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








