RC iboreshe 'magenge' yaliyokuwapo kunusuru ajali zinazorejea za treni

24Jun 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
RC iboreshe 'magenge' yaliyokuwapo kunusuru ajali zinazorejea za treni

TUMESHUHUDIA ajali ya treni juzi, taarifa zikisema watu wanne na wengine zaidi ya 132 wamejeruhiwa.

Kamanda wa Polisi wa Tabora, Richard Abwao, alisema jeshi hilo linaendelea kufuatilia taarifa za vifo na majeruhi kutokana na abiria wengi kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora Kitete, kwa matibabu, huku akieleza chanzo cha ajali hiyo mpaka bado hakijulikana.

Mashuhuda waliokuwapo kwenye eneo la ajali, ni kwamba ilitokea saa 5:00 asubuhi, baada ya mabehewa sita kuanguka kwenye eneo la Kilolo, Tabora.

Kwa siku za hivi karibuni tumeanza kusikia ajali za mara kwa mara za treni kitu ambacho huko nyuma hakikuwapo kabisa.

Miaka ya nyuma, ajali ya treni ilikuwa ni habari kubwa mno kama vile ya ndege kwa sababu ilikuwa haitokea hata baada ya miaka 10 za zaidi.

Wataalamu wa masuala ya usafiri duniani wanasema kuwa usafiri salama zaidi unaoshika namba moja ni ndege, halafu treni inafuatia.

Pia Tanzania ilikuwa moja ya nchi ambayo huwezi kusikia ajali za treni miaka hiyo na kuhesabiwa moja ya usafiri salama zaidi. Si kwa treni za mizigo au za abiria.

Kwa sasa hali ni kama imeanza kubadilika. Kumekuwa na ajali, ingawa si kubwa sana kama zile chache za zamani, lakini zimeanza kuongezeka na kutia wasiwasi wasafiri.

Itafika wakati sasa watu wataona ni afadhali kupanda basi kuliko treni ambao umekuwa ukiaminika zaidi ni salama na gharama ndogo.

Nadhani kuna tatizo kidogo ambalo serikali kwa kushirikiana na Shirika la Reli wanapaswa kukaa chini na kuangalia changamoto hizo.

Mabehewa sita kuanguka inawezekana kwa sababu mbalimbali, ikiwamo unyevu wa eneo hilo ambalo treni hiyo iliyokuwa ikitoka Kigoma kwenda Dar es Salaam, au hata kulegea kwa nati za reli.

Sina uhakika sana na hilo kwa sababu uchunguzi unafanyika, lakini moja ya sababu ambazo huko nyuma hakukuwa na ajali sana ni kuwepo na wafanyakazi wengi pembeni mwa reli inapopita maarufu kama 'magenge'.

Hawa watu walikuwa wanahakikisha usalama wa reli kila treni inapopita. Waliishi hata maporini maeneo ambayo treni inapita, na walikuwa wakishirikiana na wanavijiji ambavyo inakatiza kuweka ushirikiano wa kulinda reli.

Ushirikiano huo ulisababisha sio magenge tu kuwa walinzi wa reli, bali hata wanavijiji nao waliungana nao kuhakikisha usalama.

Hawa walikuwa wanafanya kazi ya kukagua eneo refu la reli, kuangalia kama kuna sehemu nyevu au udongo umeporomoka, lakini hata nati kulegea, wamekuwa wakirekebisha na kusawazisha kabla ya treni kupita eneo husika salama.

Baada ya kuondolewa kwa magenge wengi kutokana na kupunguza wafanyakazi, ni kwamba usalama ya reli uko mashakani.

Si sehemu nyingi na hasa maporini ambako kuna uhakika wa usalama huo. Kutokuwapo kwa ushirikiano wa TRC na wanavijiji kupitia kwa magenge, nako kunaweza kuwafanya baadhi ya wanavijiji kushindwa hata kutoa msaada au kuripoti eneo husika kama wataona kuna hitilafu kwenye reli.

Zamani watu wengi wakiliwa na utu na ujamaa, lakini kwa sasa ambapo kila mtu anajijali mwenyewe, kumekuwa na wahalifu ambao mtu tu kwa akili yake anaweza kulegeza nati au kundi la watu kutaka kung'oa reli kutokana na biashara ya vyuma chakavu.

Hali hii inasababisha kuwepo na umuhimu tena wa kuwarudisha magenge wengi kama zamani kando ya njia za treni wa ajili ya usalama.

Najua tatizo itakuwa ni kuwalipa, lakini sidhani kama TRC inapasa wawaajiri kama zamani na kuwapa nyumba, kinachotakiwa waende kisasa, wanaweza kupita vijijini vinavyopita reli na kuwatafuta vijana ambao wanaweza kufanya kazi kulinda reli kama wanavyofanya sungusungu na kuwalipa kama posho kwa jinsi watakavyokubaliana.

Hii inaweza kupunguza baadhi ya ajali zinazoweza kuzuilika, ambazo zinatokana na uhalifu wa uharibifu wa miundombinu.

Kuna ajali ambazo hutokea kwa matatizo ya kiufundi ambayo kwa treni ni nadra sana kutokea, lakini kwa hujuma kutoka kwa majahili na waharibifu wa miundombinu zitakuwa zimezuilika na kuufanya usafiri huo kuendelea kuwa salama na kuaminika.