Kichwa kikubwa na mgongo wazi visiwe vikwazo vya kupata elimu

23Jun 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kichwa kikubwa na mgongo wazi visiwe vikwazo vya kupata elimu

BAADHI ya wanafunzi wenye ulemavu kila mara hukumbana na vikwazo kadhaa katika kufikia malengo yao waliyojiwekea kupitia elimu, hali ambayo wakati mwingine inaweza kuwakatisha tamaa.

Miongoni mwa hao wenye ulemavu wanaokumbana na hayo ni wenye shida ya kuwa na kichwa kikubwa au mgongo wazi, ambao inaelezwa wanakataliwa usajili katika baadhi ya shule za serikali.

Watoto hao hupata shida hizo, hasa baada ya serikali kuanzisha utaratibu wa elimu jumuishi, inayolenga kuwafanya wanafunzi wenye ulemavu na wale wazima kusoma pamoja.

Hata hivyo, kumekuwapo madai kwamba, watoto wenye ulamevu wa kichwa kikubwa na mgongo wazi, wanakataliwa kuandikishwa kuchangamana na wenzao wenye viungo kamili.

Madai hayo yanatolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Wazazi wa Watoto Wenye Kichwa Kikubwa na Mgongo Wazi Tanzania (ASBAHAT), Abdul-hakim Bayakub na anaiomba serikali iwasaidie kumaliza tatizo hilo.

Ni katika mkutano wa chama hicho na wadau wengine wa elimu, anatoa malalamiko hayo na kufafanua kuwa elimu jumuishi ilianzishwa, ili wanafunzi wote wakiwamo wenye ulemavu na wasio na ulemavu, wasome pamoja darasa moja.

Ni vyema basi wanaowanyima fursa watoto hao wahitaji wakatafari kwa umakini, hata kuchukua hatua sahihi za kutowatenga watoto wenye ulemavu, kwani hawakuomba wazaliwe hivyo.

Pia bado inabaki kuwa busara kukumbuka msemo wa Kiswahili kwamba ‘hujafa hujaumbika.’ Hivyo, kila mmoja kati yetu ni mlemavu mtarajiwa, kwani anaweza kukumbwa na madhila au ugonjwa unaompa hali ya ulemavu.

Inawezekana mazingira kama hayo ya kuzuia yakawafanya baadhi ya wazazi kuacha kuwapeleka watoto wenye ulemavu shuleni, kwa kuhofia kuchekwa, kudharaulika, au kushushiwa heshima.

Vilevile, mazingira hayo ya mizengwe kwa namna moja au nyingine, yanaweza kukwamisha lengo la kuwapo elimu jumuishi, ambalo ni kuwafanya wanafunzi wote bila kujali ulemavu, kusoma pamoja.

Nadhani walimu kama walezi, wangesaidia au kuwa chachu kuondoa vikwazo hivyo, ili kuhakikisha wanafunzi wenye ulemavu wanapata elimu na wenzao wenye viungo kamili, ili iwasaidie katika maisha yao ya baadaye.

Kuwajumuisha wanafunzi katika elimu, kunahitaji ushirikiano na taasisi mbalimbali kama za kiafya, kijamii, ustawi wa jamii, maji na usafi wa mazingira, usafiri wa umma na sekta zinazohusiana na haki.

Ninaamini kwamba, wadau hao wote wakishiriki kwenye jambo hili, inaweza kusaidia kumaliza vikwazo wanavyokumbana navyo watoto wenye ulemavu hasa wa kichwa kikubwa na mgongo wazi vya kukataliwa kuandikisha shule.

Pamoja na hayo, ninaamini pia kuna haja ya kuwekeza katika kuongeza ubora wa majengo, vifaa vya kujifunza na kufundishia katika shule zetu, ili kuwasaidia wanafunzi wenye ulemavu, ambao serikali imeamua kuwajumuisha na wenzao kupata mafunzo kwa pamoja.

Ulemavu huo wa kuwa na kichwa kikubwa na mgongo wazi, kuna wakati Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, ameshawahi kutolea ufafanuzi, kwamba watoto wenye hali hiyo wanaendelea kupokelewa shuleni, pia serikali inajitahidi kuboresha miundombinu ya shule zote zinazojumuisha watoto wenye ulemavu.

Wakati fulani ameshawahi kutoa mfano, kwamba Shule ya Sekondari Patandi, iliyoko Arusha ni ya mfano, kwa vile inachukua wanafunzi wote wakiwamo wenye ulemavu, huku ikiwa na walimu wenye utaalamu wa kuwafundisha wanafunzi wenye hali hiyo ya dosari kiafya.

Ingekuwa vyema, kama shule zinazodaiwa kuwakataa watoto wenye ulemavu huo kuzingatia kile ambacho waziri, ameshawahi kukieleza kuhusu ujumuishaji wa watoto hao, ili kuondoa mkanganyiko uliopo.

Ikumbukwe kwamba, viongozi wa ASBAHAT wanabainisha kuwapo wenye ulemavu huo, ambao wamesoma na kuhitimu masomo yao vizuri na sasa wanategemewa katika taasisi mbalimbali za umma na binafsi katika utaalamu tofauti, ukiwamo  wa TEHAMA.

Mafanikio hayo yangewafanya walimu wanaowakataa walemavu wa kichwa kikubwa na mgongo wazi wabadili mtazamo na kutambua kuwa wana uwezo mzuri shuleni kama walivyo wengine wenye viungo kamili.