Ina maana klabu hiyo haitosajili kwa msimu mzima wa 2022/23, kwenye dirisha kubwa linalotarajiwa kuanza Julai Mosi hadi Agosti 31 mwaka huu, na ule wa dirisha dogo ambao unatarajiwa kuwa Desemba 16 mwaka huu hadi Januari 15 mwakani.
Shirikisho la Soka Nchini (TFF) likasema adhabu hiyo imetolewa baada ya timu hiyo kushindwa kuheshimu uamuzi wa awali wa FIFA kuifungia kusajili wachezaji hadi itakapokamilisha malipo ya madai ya mishahara ya aliyekuwa mchezaji wake, Timoth Balton Omwenga.
Kutokana na kutoheshimu uamuzi huo, ndipo FIFA ilipowasilisha suala hilo kwenye kamati yake ya nidhamu ambayo Mei 19, mwaka huu ilitoa adhabu hiyo kupitia mjumbe wake, Carlos Teran wa Venezuela.
Hili ni pigo zito kwa Biashara United ambayo tayari ipo hoi bin taaban katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa inashika nafasi ya 15 kati ya timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo.
Inapigania uhai wa kubaki Ligi Kuu, au hata kwenda tu kucheza mechi za mchujo 'play off''.
Kilichotokea ni kama vile mtu aliyebakisha nauli ya basi tu mfukoni, lakini hiyo hiyo baadaye nayo ikachukuliwa kwa kuibiwa au kupotea.
Ni huzuni iliyoje kwa timu hiyo ambayo msimu huu ilicheza michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika na ilikuwa bado kidogo itinge kwenye hatua ya makundi, kwani katika mechi ya kwanza hapa nchini iliichapa Al Ahly Tripoli ya Libya mabao 2-0, lakini kwa bahati mbaya au uzembe, ikashindwa kwenda katika mchezo wa marudiano ugenini.
Timu iliyofungwa na Biashara United na kusonga mbele kwa ushindi wa chee, ilifanikiwa kutinga mpaka hatua ya nusu fainali ya kombe hilo, ikitolewa na Orlando Pirates ya Afrika Kusini ambayo katika hatua ya robo fainali iliibwaga Simba.
Hapa unaweza kuona Biashara United ilikuwa ni timu iliyokamilika, lakini ukiangalia kwa makini ni kama imekosa viongozi bora.
Hata mechi za mwanzo za kombe hilo zilisafiri kwa kubahatisha, kabla ya kushindwa kwenda Libya.
Ibaki Ligi Kuu au ishuke daraja, Biashara United sasa itaendelea kuwa na wachezaji hao hao, ambao kwa ninavyolijua soka la Tanzania, baadhi yao msimu ujao watasajiliwa na klabu nyingine, tena kama ikishuka ndiyo kabisa wataondoka wengi, labda wale ambao hawatakiwi.
Nadhani watalazimika kuwapandisha wachezaji wengi wa chini ya miaka 20, sipati picha kama itabaki Ligi Kuu halafu uwe na vijana wa aina hiyo wengi kwenye timu.
Nilimsikia kiongozi wake mmoja akidai hawakujua kama ni usajili wa wachezaji wa ndani au wa nje.
Hii ni aina ya viongozi ambao hawajui hata kanuni na inapofanya kazi wanashangaa.
Mfano hivi sasa maoni ya wadau wa soka wanakusanywa ili kutengeneza kanuni ya msimu ujao wa ligi, cha ajabu unaweza kukuta baadhi ya viongozi wa klabu hawashiriki na wala hawazijui, ila watakuja kulalamika siku zikianza kufanya kazi na kuuma upande wao.
Viongozi wa TFF kupitia kamati zao sasa inabidi waendeshe semina kwa viongozi wa klabu, kwani ni aibu na kiongozi yoyote kuonekana kutojua chochote kuhusu kanuni za usajili, lakini hata klabu inapofungiwa, bado anakuwa haelewi.
Najua ingekuwa ni Simba au Yanga, zimefungiwa, lawama zingeenda zaidi TFF kuwa hadi viongozi hao wanasajili wao walikuwa wapi wasiwajulishe.
Imefika wakati kufungiwa Biashara United inawezekana kuonekana ni jambo dogo kwa baadhi ya mashabiki wa soka nchini, lakini hili ni somo na funzo kubwa kwa wadau wengine.
Tumekuwa na mlolongo wa taarifa za wachezaji na makocha kudai pesa zao kwenye klabu hata zile zinazoitwa au kujiita kubwa.
Tena unakuta wanadaiwa halafu wanajibu kwa jeuri na kujiamini. Inafaa waelewe FIFA huwa hawajali ukubwa wa timu na inapoamua kushusha rungu inashusha bila kujali mashabiki watasema nini. Wenyewe wanaangalia zaidi sheria inasemaje na si busara kama ambayo maamuzi yetu nchini yanavyokuwa wakati mwingine wa kisiasa.
Ni wakati sasa viongozi wa klabu kuendesha soka kisasa, kuwalipa wachezaji na waajiriwa wote mishahara kwa wakati na hata kama hawana, basi kuongea nao kirafiki, badala ya kuwajibu majibu yasiyoeleweka na kukimbilia FIFA.
Na hii imeonekana sana kwa wachezaji wa kigeni, wamekuwa wanajitambua sana na hasa kwenye kudai maslahi yao, tofauti na wachezaji wa Kitanzania ambao wanaona aibu kudai au wanaogopa.
Adhabu hii ambayo Biashara United imeipata kama viongozi wa klabu za soka hapa nchini hawatajirekebisha, basi tusishangae kuzikuta timu nyingine zikikumbana na rungu hili.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








