Ongezeko la mapato ya serikali lionekane kwa wananchi

10Feb 2016
Mary Geofrey
Nipashe
Mjadala
Ongezeko la mapato ya serikali lionekane kwa wananchi

MWEZI uliopita serikali ya Rais John Magufuli ilikusanya mapato ya kodi kiasi cha Sh. trilioni 1.045 kutoka kwa wafanyabiashara.

Kaimu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alfayo Kidata, alieleza kuwa makusanyo hayo ni sehemu ya malengo waliyojiwekea kwa mwezi huo.

Ukusanyaji huo wa kodi kwa mapato ya ndani umeongezeka ukilinganisha na mwaka jana mwezi Januari, ilipokusanya mapato kidogo.

Makusanyo hayo na yale ya mwezi Desemba mwaka jana Sh. trilioni 1.3 yanadhihirisha inadhihirisha wazi kuwa ni kwa kiasi gani TRA wamefanya vizuri katika eneo la ukusanyaji.

Tuliona fedha hizo zikigawanywa katika shughuli mbalimbali za miradi ya maendeleo.
Jumla ya Sh. bilioni 318.406, ziligawanywa na serikali kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Servaciaus Likwelile alibainisha kiasi cha Sh. bilioni 274 zilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara na Sh. bilioni 40 kwa ajili ya mradi wa umeme kinyerezi 2.

Kiasi kingine cha Sh. bilioni 7.7 kilitengwa kwa ajili ya miradi ya maji kati ya bilioni 46.3 zilizotengwa kwa ajili ya mfuko huo na awali zilitolewa bilioni 12.5.

Pia Sh. bilioni 21.959 zilitengwa kwa ajili ya mradi wa umeme vijijini (REA) na Sh. bilioni 82.2 kwa ajili ya mifuko ya hifadhi ya jamii ili kulipa madai ya wastaafu.

Serikali pia ilishatoa fedha kwa ajili ya magari ya wabunge kiasi cha Sh. bilioni 35.5 sawa na milioni 90 kwa kila mbunge.

Kwa mujibu wa Gavana wa Benki Kuu Tanzania, Benno Ndulu, kwa sasa uchumi umekuwa kwa asilimia saba kutoka asilimia 6.9 mwaka jana hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza katika ya nchi za Afrika ya Mashiriki na kufuatiwa na Rwanda ambayo uchumi wake ni asilimia 6.2 na Kenya asilimia 5.6.

Pia mfumuko wa bei umepanda hadi kufikia 6.8 kiwango ambacho kipo chini ukilinganisha na kigezo cha Afrika ya Mashariki ambacho ni 8 huku nchi za Uganda ikiwa kiwango cha 9.5 kuvuka kigezo na Kenya kiwango cha 8.1.

Kwa sasa serikali inategemea mapato yanatokanayo na fedha za kigeni kutoka sekta ya utalii, mapato ya Dola bilioni 2.2 kutoka Dola bilioni 1.3 mwaka jana.

Kwa makusanyo haya ya kodi na matumizi yaliyopangiwa, inadhihirisha wazi kuwa, serikali imetekeleza vyema majukumu ya kukusanya kodi na kuzitengea kazi yake.

Jukumu kubwa lililobaki ni wananchi kuhamasishana kulipa kodi na pia kutoa taarifa kwa wakwepa kodi kwa kutambua kuwa kazi za miradi ya maendeleo haiwezi kutekelezwa kwa miujiza bali kwa makusanyo yatokanayo na kodi.

Serikali inawajibu mkubwa wa kuhakikisha fedha zilikokusanywa na kutengwa katika sekta mbalimbali zinafika kwa wakati na kutumika kikamilifu.

Wizara ya fedha inao wajibu wa kueleza imetenga kiasi gani cha fedha kwa ajili ya sekta fulani.
Serikali ihakikishe kazi fedha hizo, zinafanya kazi zilizotengewa kufanya ili wananchi wazione.

Usimamizi wa fedha uwe madhubuti isije ikawa serikali inawabana wananchi na kukusanya fedha ambazo zinaenda kuingizwa kwenye mifuko iliyotoboka kwa maana mikononi mwa watumishi wasiyo waadilifu.

Ni vyema serikali na wanachi wakatekeleza vyema majukumu yao, kila mtu katika nafasi yake ili kufikia lengo la kuwa nchi iliyo katika uchumi wa kati.

Tumeshuhudia Rais John Magufuli, akionyesha dhamira yake ya dhati ya kuwatumikia Watanzania kwa uadilifu na kuhimiza kila mmoja kusimama katika nafasi yake ya kulitumikia Taifa.

Mtoza kodi atoze kodi halali, mlipa kodi ahahakikishe analipa kodi stahiki pamoja na kudai risiti, wanaotekeleza majukumu ya fedha hizo wazitumie vyema kufanya shughuli zilizoelekezwa ili mwisho wa siku Watanzania wote wanufaike na kodi zao.

Ni matumaini ya wengi kuwa miradi mbalimbali ya maendeleo itaonekana pamoja na kutatua kero zingine zikiwamo za kuwalipa wastaafu, kujenga barabara, na shughuli nyingine.