Athari za mvua hizi ni zaidi ya mafuriko

11Feb 2016
Restuta James
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Athari za mvua hizi ni zaidi ya mafuriko

MVUA zinaendelea kunyesha kila kona ya nchi zina athari mbalimbali. Baadhi ya maeneo zimeharibu miundombinu ya barabara kiasi cha kukata mawasiliano, mafuriko kwenye makazi ya watu, na kuezua madarasa na zahanati kwenye shule na vijiji kadhaa.

Katika baadhi ya maeneo, shule zimelazimika kufungwa kwa muda kutokana na kuzingirwa na maji. Na nyingine kupata nyufa au kuanguka sehemu kutokana na mvua hizo.

Kwa waishio mabondeni hususani jijini Dar es Salaam, hali ni mbaya zaidi. Hata hivyo, katika mjadala wangu, nitajikita zaidi kwenye njaa inayoweza kutukumba kutokana na athari za mvua zinazonyesha sasa.

Taarifa kutoka kwenye baadhi ya maeneo, mvua imeharibu mashamba na kuzoa mazao yaliyokuwa yamepandwa.
Mathalani, Kata ya Chimala, wilayani Mbarali, mkoa wa Mbeya, mashamba mengi ya mahindi, mpunga na karanga, yalisombwa na maji.

Hali hiyo imetokea pia Mikumi, Malinyi na Mvomero mkoani Morogoro; Kata ya Idodi-Iringa na sehemu nyinginezo nchini.
Kwamba katika maeneo hayo, mahindi yakiwa kwenye ‘umri’ tofauti yamesombwa na maji hivyo wananchi kulazimika kuomba chakula cha msaada.

Nafahamu tathmini ya uharibifu inafanyika sehemu mbalimbali; lakini wakati hayo yakiendelea, ni lazima tujizatiti kuhifadhi chakula kwa kaya moja moja na Taifa kwa ujumla.

Familia na mamlaka za mikoa yote, zinapaswa kuhakikisha kwamba chakula kilichopo kinatumika kwa uangalifu mkubwa.
Tunapaswa kufanya hivyo kwa sababu, Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), mara kadhaa yametoa taarifa kwamba mvua zitaendelea kunyesha na zitakuwa za el-nino.

Tafsiri nyingine ya mvua hizi ni kuendelea kukatika kwa mawasiliano kwenye sehemu kubwa ya nchi, hasa kwa kuzingatia kuwa barabara nyingi siyo za kiwango cha kuhimili misukosuko ya mafuriko.

Ninachomaanisha hapa ni kwamba, kama mvua zikinyesha zaidi, itakuwa vigumu hata kupeleka vyakula vya misaada kwa wahitaji kutokana na uharibifu mkubwa unaoweza kutokea.

Tumeshuhudia katika wilaya ya Malinyi namna ambavyo mvua imeharibu barabara kiasi kwamba ni matrekta tu ndiyo yanayotumika kutoa huduma kadha wa kadha; huku wakulima wakishindwa kusafirisha mazao ambayo walifanikiwa kuyaokoa toka shambani.

Wote tunafahamu mwendo wa trekta, itachukua muda gani kusafirisha chakula mathalani kutoka Tanga hadi Malinyi, kama itatokea Mkoa wa Morogoro kuishiwa chakula? Au chakula kitatokaje Babati (Manyara) kwenda Mpwapwa (Dodoma)? Hili ndilo lililonifanya nizikumbushe mamlaka kuangalia tatizo la mvua kwa jicho la tatu.

Kwamba wakati wananchi wakilalamika kukosa huduma za kijamii kama barabara, afya baada ya zahanati kuezuliwa au watoto kukosa elimu; tufikirie pia njaa inayotunyemelea kama Taifa.

Tena ikiwezekana, mikoa inaweza kununua chakula kutoka sehemu nyingine kabla mvua hizi hazijachanganya ili zijihakikishie kuwa na chakula pale baa la njaa litakaposhika kasi.

Wananchi pia wanunue mahitaji muhimu kama sukari,mahindi na mafuta ya taa na kula kwa kuwa wakati mwingine mvua inaweza kunyesha hadi wakashindwa kununua mahitaji hayo ya muhimu.

Serikali nayo ichukue hatua za haraka kujenga mitaro kwenye barabara zote ili maji yaweze kupita kwa urahisi na kuepusha mafuriko kwenye makazi ya wananchi.
Mungu ibariki Tanzania