Mafunzo hayo yalilenga kuwapatia uelewa kuhusu usalama na madhara ya matumizi ya chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba visivyo bora kwa jamii.
Hatua ya TFDA kuwashirikisha wadau baada ya kutambua kuwa hawawezi kufikia malengo ya kulinda afya ya jamii bila kupata ushirikiano kwa jamii na taasisi mbal mbali.
Kila mdau anapaswa kuzingatia mfumo wa upatikanaji wa chakula toka eneo la uzalishaji, wakiwamo wakulima ambao ni wadau namba moja kwa kuwapatia elimu kuhusu usalama wa mazao shambani.
Hii ni kutokana na ukweli kuwa, kama udhibiti utaanza toka kwa mzalishaji , itarahisisha shughuli za udhibiti wa usalama na ubora wa chakula katika ngazi zinazofuata.
Hiyo ni hatua kubwa kwa TFDA kuainisha kuwa udhibiti wa usalama wa chakula ni suala mtambuka linalohitaji wadau wengine kushirikishwa licha ya kupewa dhamana ya kusimamia suala hilo.
Siyo rahisi kufikia malengo ikiwa wadau kutoka taasisi za serikali na zisizo za kiserikali hawashiriki katika kuhakikisha kuwa suala la udhibiti wa usalama wa chakula linapewa kipaumbele.
Lazima tufikie mahali kila mwananchi anazingatia usalama wa chakula hasa kwa kutoa taarifa inapobainika dosari au baadhi ya bidhaa kuingizwa nchini isivyo halali ili hatua stahiki zichukuliwe haraka kabla ya bidhaa hiyo kuingia sokoni.
Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula TFDA, Raymond Wigenge, amesema udhibiti wa usalama wa chakula ni suala la kisheria, hivyo linapaswa kufuata mfumo wa mnyororo wa thamani na kushirikisha wadau mbalimbali.
Licha ya changamoto ya utekelezaji wa sheria unaotokana na utitiri wa viwanda vidogo vidogo ambavyo baadhi yake huzalisha bidhaa zisizo na ubora, hata kusababisha udhibiti wa bidhaa hizo kwenye soko kuwa mgumu.
Siyo rahisi changamoto hiyo kudhibitiwa na TFDA pekee bali wadau wanaozalisha bidhaa hizo lazima washirikishwe kwa kupatiwa elimu ili wafahamu madhara ya kuzalisha bidhaa duni kwa afya ya jamii.
Nafahamu kuwa, ikiwa jamii itashirikishwa kikamilifu katika suala la udhibiti wa chakula ni kwamba kila mdau ataacha tabia ya kunyoosheana vidole kuwa anayehusika ni yule na kujitenga na uchukuaji wa hatua stahili kwa lengo la kuhakikisha kuwa udhibiti wa usalama wa chakula unafanikiwa.
Ni ukweli usiopingika kuwa wafanyakazi wa TFDA hawatoshelezi kuwepo kila mahali, hivyo ni muhimu kwa taasisi nyingine kuhakikisha kuwa zinatoa mchango wake muhimu wa udhibiti kwa kushirikiana na wananchi ambao ni wadau muhimu .
Changamoto katika taasisi hiyo bado ni kubwa hasa suala la upimaji wa sampuli, maabara ni moja hivyo inakuwa vigumu kubaini kwa haraka bidhaa inapokamatwa mipakani na kuipima kikamilifu.
Kwa sasa, maabara ipo moja tu jijini Dar es Salaam. Katika hali hiyo, kama bidhaa imekamatwa Kigoma lazima sampuli hiyo isafirishwe hadi Dar es Salaam ili ifanyiwe uchunguzi wa kimaabara.
Kwa namna yoyote ile, safari bado ni ndefu hadi kufikia viwango vya udhibiti wa usalama wa chakula,kutokana na ukweli kuwa mipaka mingi hata kusababisha baadhi ya watu kutumia mwanya huo kufanya wanayoyafanya kufanya uhalifu.
Watanzania tunahitaji mabadiliko siyo kwenye siasa pekee, hata kwenye udhibiti wa usalama wa chakula. Kila mtu ajitahidi kutoa taarifa kwa mamlaka husika inapobainika kuwa kuna bidhaa duni zinaingizwa kinyemela nchini hata kuhatarisha usalama wa afya ya watumiaji.