Mazungumzo ya kusaka muafaka wa kisiasa Zanzibar yametuacha hewani!

10Feb 2016
Richard Makore
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mazungumzo ya kusaka muafaka wa kisiasa Zanzibar yametuacha hewani!

MWAKA jana baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kutangaza kufuta matokeo na uchaguzi wote Watanzania walisikia mambo mengi ikiwamo yaliyohusu vikao vilivyokaa kwa kutafuta muafaka wa kisiasa.

Muafaka uliokuwa ukitafutwa ni kati ya aliyekuwa mgombea wa urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF) na Ali Mohamed Shein aliyegombea nafasi hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wakati wa vikao hivyo Watanzania waliambiwa watulie kwani kulikuwa na watu wazima tena wenye heshima kubwa kwa taifa walikuwa wanaweka mambo sawa kupitia mazungumzo.

Tulishuhudia viongozi wakisimama lango la Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam, wakizungumza lugha ya kutia matumaini kwamba hakuna jambo litakaloharibika.

Lakini kilichonishangaza na kuwashangaza wengi ni pale mazungumzo ya watu wazima hawa tena wenye heshima yaliyoishia hewani bila kuwaambia wananchi nini walichokuwa wamezungumza.

Nasema yaliishia hewani kwa sababu sijawahi kusikia mtu akisema tulishindwa kufikia muafaka kutokana na vipengele fulani kuleta utata badala yake tulishuhudia ZEC ikitangza tarehe ya marudio ya uchaguzi Zanzibar.

Tuliambiwa mazungumzo yalikuwa yakienda vizuri pande zote mbili ziliwahakikishia kila kitu kitakwenda vizuri, lakini jambo la msingi la kujiuliuza kwa nini mazungumzo yaliishia hewani.

Kuna msemo usemao kwamba ngoma ya kitoto haikeshi, lakini sitaki kufananisha na hili kwa sababu hawa walikuwa watu wazima, tena wazito sana.

Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema katika hotuba zake kwamba kipindi fulani wa CCM walitoka Zanzibar na walipofika wakaanza kufanya vitu ambavyo havifanani na Azimo la Arusha, sasa yee anasema kwa watu wazima walijua hili limekwisha na Azimio la Arusha sasa halipo.

Mwalimu Nyerere alitoa mfano huo mapema miaka ya 90 pale Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM ilipokutana Zanzibar na kuanzisha kuondoa misingi ambayo ilikuwa inaongoza Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na hivyo kuliua Azimio la Arusha lililokuwa linatekeleza itikadi ya Ujamaa.

Nayasema haya kujaribu kuweka sawa kumbukumbu na historia ya nchi kwamba kunaweza kufanyika vikao vikubwa kama hivi vilivyofanyika Zanzibar kutafuta muafaka wa kisiasa halafu vikaishia hewani bila watu kujua nini kilikuwa kinazungumzwa ama nini kilikwamisha mazungumzo hayo muhimu kwa ajili ya kumaliza mgogoro wa kisiasa, ambao ni tishio kwa umoja na utulivu wa taifa letu.

Wananchi hawakupata mrejesho wa kile kilichokuwa kikizungumzwa na sasa wanahamishwa kujiandaa na marudio ya uchaguzi wa Zanzibar Machi 20, ambao dalili zake zinaonyesha kuwa ni wa kuchochea mgawanyiko miongoni mwa Wazanzibari, badala ya kujenga umoja wa kitaifa.

Panapotokea kasoro za kisiasa popote duniani njia nzuri ya kupata suluhu ni kupitia meza ya mazungumzo na siyo vinginevyo.

Kwa bahati mbaya mazungumzo haya hayakukesha bali yalimazika huku kila upande ukiweka lake moyoni na kuwaacha Watanzania vinywa wazi.

Kinachoshangaza zaidi ni kuwa ahadi ya kutolewa kwa taarifa rasmi kwa umma iliahidiwa na viongozi wakubwa wenye dhamana, hivyo ukimya wao unaashiria kwamba mazungumzo hayo yalilenga maslahi ya vyaoa na siyo ya taifa.

Kikubwa hapa ni kuomba amani iendelee kutawala na ifike mahala haki ipatikane kwa pande zote mbili zilizokuwa zikibishana kuhusu kufutwa uchaguzi na matokeo yake yote.