CCM isiisahau misingi yake, ikawekeza kwa upinzani

10Feb 2016
Mashaka Mgeta
Nipashe
Mtazamo Yakinifu
CCM isiisahau misingi yake, ikawekeza kwa upinzani

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetimiza miaka 39 tangu kuanzishwa kwake Februari 5, 1977 visiwani Unguja.

Kikiwa kimetokana na Afro Shiraz Party (ASP) na Tanganyika African National Union (TANU), chama hicho kimeendelea kuwapo madarakani, licha ya kukabiliwa na upinzani unaokuwa kwa kasi nchini.

Kama kilivyo chama chochote cha siasa, CCM ina historia yake inayojikita kwenye misingi, dira, mwelekeo na itikadi zake.

Kihistoria chama hicho ninachokijadili kutokana na mwenendo wake katika siasa za ndani ya nchi, kimewekeza zaidi kwa wakulima na wafanyakazi.

Hata alama za awali zinazodumu hata sasa, zikiwa nembo ya CCM ni jembe la nyundo; nyembe likiwawakilisha wakulima na nyundo kwa wafanyakazi.

Katikati ya jamii iliyoanza kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, CCM inajikuta katika upinzani rasmi unaotambulika kisheria.

Ukuaji wa demokrasia unaotoa fursa kwa raia kuanzisha ama kujiunga kwenye vyama vya siasa unakuwa changamoto kwa CCM iliyokuwapo kwa takribani miaka 15 pasipo kuwapo upinzani.

Lakini ikiwa ni miaka 24 ikikabiliwa na upinzani, ni sawa na kusema CCM imetumia muda mrefu kukabiliana na upinzani kuliko ilivyokuwa madarakani katika mfumo wa chama kimoja.

Muda huo ni kuanzia pale chama hicho ‘kilipozaliwa’ kikitokana na ASP na TANU.

Kwa hiyo na jambo linapokuwa kuwa miongoni mwa yenye vipaumbele kwa CCM kuhakikisha kuwa kama kinahitaji kuendelea kutawala, kiweke mazingira bora yanayokipa nguvu thabiti katika kuukabili upinzani unaokuwa kwa kasi.

Kwa miaka ya hivi karibuni, umma umesikia kutoka kwa walio ndani ya CCM wakielezea uwapo wa magamba, mafisadi na sasa mamluki wa kisiasa.

Kada hizo zinatajwa na viongozi wa juu wa CCM na kuahidi kuwa wahusika watashughulikiwa kwa ukali na haraka, ili chama hicho kiendelee kuwa mahali salama kwa Watanzania kujiunga.

Lakini ukweli wa kitakwimu unaonyesha jinsi CCM inavyozidi kupoteza kuungwa mkono kwake, kuanzia nafasi ndogo ya ushindi kwa urais na kuzidi kupoteza nafasi za ubunge na udiwani.

Wakati hali ikiwa hivyo, wanachama wa CCM wamejikuta katika mkumbo wa ‘safari ya kisiasa’, ile inayowatoa kutoka chama kimoja, kwenda chama kingine.

Wakati wa utawala wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amani Karume, kuwa ndani ya CCM ilikuwa mfano wa kuiishi imani.

Si kwamba hapakuwa na asili ya upinzani, la hasha. Upinzani ulikuwapo hadi ndani ya watawala, lakini misingi, dira, mwelekeo na itikadi vilisimamiwa na kuwaweka wanachama hao pamoja.

Sasa kunapokuwapo ‘kilio’ cha magamba, mafisadi na mamluki ndani ya CCM, inakuwa moja ya viashiria kwamba chama hicho kinakosa usalama zaidi kwa Watanzania kujiunga ili kuitumikia nchi ndani ya mifumo rasmi.

Inawezekana kukawa na sababu za kuwapo hali hiyo. Miongoni mwa hizo ni ‘kupotea’ kwa misingi, dira, mwelekeo na itikadi kwa wanachama wake.

Wanachama wa CCM kama walivyo wa vyama vingine, wanaposhindwa kuielewa misingi, dira, mwelekeo na itikadi za chama husika, si rahisi kuyakwepa mambo mawili makubwa;

Mosi ni kujiunga katika CCM, wanachama wasiokuwa waadilifu, wale wanaofikia hatua hiyo ili kufanikisha azma ya kuyafikia matarajio yenye maslahi binafsi, hivyo ‘kukichafua’ chama cha siasa.

Pili ni ‘hama-hama’ inayoweza kuwajumuisha wanachama wenye uwezo, ushawishi na vipaji vya kuielezea misingi, dira, mwelekeo na itikadi za chama hicho, kikazidi kuungwa mkono.

Sasa pamoja na umuhimu wa kuvishambulia vyama vya upinzani kupitia propaganda inayolenga kuuaminisha umma kwamba havifai, CCM ina kazi ya kujirejesha katika uenezi thaibiti wa misingi, dira, mwelekeo na itikadi zake.

Chama hicho hakipaswi kuwekeza muda mwingi katika kuushambulia upinzani huku ndani yake wanachama wakikosa haki ya kukijua chama hicho na undani wake jinsi kilivyo.
Haiwezekani, kwa mfano safu ya viongozi wakuu zaidi ya watatu wa CCM kujielekeza katika mashambulizi dhidi ya upinzani, huku wakishindwa kuufahamisha umma kuhusu misingi mikuu ya chama hicho na namna inavyosimamiwa.

Ilitokea kabla, wakati na sasa baada ya kampeni za Uchaguzi Mkuu ambapo mashambulizi kutoka CCM kwenda upinzani yanachukua nafasi kubwa kwa watawala.

Si nia yangu kuipa CCM mbinu hata kama hazikubaliki kwa walio kwenye mamlaka ya kukiongoza chama hicho kwa sasa, lakini kikiwa ni moja ya taasisi za umma, nina wajibu wa kuandika kwa ajili yao.

Ikumbukwe kwamba kwa asili yake, kujiunga katika CCM kulitanguliwa na mhusika kupitia mafunzo mahususi yaliyomuwezesha kukitambua chama, hivyo kuwa na uwezo mpana wa kukieneza kwa umma.

Wakati programu hiyo ikitumika, hapakuwapo mageuzi ya sayansi na teknolojia, hivyo kuwanufaisha watu wachache.

Katikati ya hali ngumu hiyo, CCM ilikuwa na wanachama walioielewa, wakaiishi misingi, dira, mwelekeo na itikadi zake tofauti na ilivyo sasa.

Kwa sehemu kubwa, kunapofanyika jumuiko lolote la CCM, miongoni mwa mambo makubwa yanayotarajiwa kusikika ni mashambulizi dhidi ya upinzani. Binafsi sioni kama hatua hiyo ni yenye ufanisi kwa CCM.

Pengine ni kutokana na hali hiyo, ndio maana siasa zimegeuzwa kuwa eneo la kurushia michapo na si kuzungumzia masuala.

Wanachama na wafuasi wa vyama vya siasa wanajikita katika michapo, mambo binafsi ama namna nyingine isiyokuwa na tija, hivyo kuiharibu dhana na umuhimu wa vyama vya siasa kwa taifa.

Hivyo inapoadhimisha miaka 39 tangu kuanzishwa kwake, CCM inapaswa kuondoka na kuwekeza muda mwingi kuwashambulia wapinzani, badala yake ijiimarishe zaidi katika misingi, dira, mwelekeo na itikadi zake.

+255 754691540, 0716635612
[email protected], [email protected]