Kwamba kupitia Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), kazi ya kutumbua majipu inayofanywa na Rais Dk. John Magufuli, ingerahisishwa kabisa.
Hii ni kwa sababu, watendaji wabovu wangebanwa serikalini na kwenye Bunge pia, hasa kupitia kwenye kamati hizo, ambazo kwa mujibu wa kanuni zinaongozwa na kambi ya upinzani zikiwa na jukumu la kuchambua taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Lakini katika hali ya kusikitisha, imekuwa kinyume chake. Siyo tu kwenye uteuzi wa wajumbe wa kamati husika; bali Bunge pia limenyofoa baadhi ya majukumu ya PAC na kuyapeleka kwenye kamati nyingine inayoitwa ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) itakayoongozwa na mbunge kutoka Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
Yamekuwapo malalamiko mengi, lakini kubwa ninalotaka kulieleza hapa ni kwamba, njama hizi kamwe hazikisaidii Chama Cha Mapinduzi(CCM) wala Rais Magufuli ambaye amepania kurudisha nidhamu kwenye utumishi wa umma.
Ikiwa sote (pamoja na wabunge wa CCM), tunakemea rushwa na ubadhirifu, basi PAC na LAAC ni kamati muhimu sana za kuisaidia serikali kwani ni kwenye mashirika kama ATCL, TRL, Tanesco, TPDC na kwenye Halmashauri zote nchini ambako fedha za walipa kodi zinapelekwa kuboresha huduma mbalimbali.
Sasa kama njama zilizofanywa na wachache bungeni ni kulinda ‘mchwa’ wa fedha za umma; ni aibu kubwa lakini pia wana nia ya kuendelea kulea wezi.
Haiwezekani kwa mfano, Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania), linalopata hasara ya mabilioni ya fedha kila mwaka kutokana na mikataba ya kinyonyaji iliyoingia na kampuni zinazoliuzia umeme liachwe tu kwa kuhamisha majukumu ya PAC kwenda PIC; hii siyo sawa.
Mathalani wakati Tanesco ikieleza kupata hasara ya Sh. milioni 500 kila siku kutokana na kukatikatika kwa umeme (taarifa ya mwishoni mwa mwaka jana), wanaolinyonya shirika hilo waachwe tu kwa kuhofia CCM kukosolewa? Jibu hapa ni hapana kwa sababu nia ni kuhakikisha tunaachana na bajeti ya ‘sungura’ kwenda kwenye bajeti ya ‘ng’ombe.’
Sote tunajua namna ambavyo wajanja wachache wanavyotafuna fedha za umma huku wananchi wakihangaika mchana na usiku kutafuta huduma bora za kijamii bila mafanikio.
Kilichotokea bungeni kimefanyika miezi michache tu kabla Watanzania hawajasahau zaidi ya Sh. bilioni 600 zilizobainishwa na CAG kwamba zimetumika kifisadi kwa hesabu zilizoishia Juni 30, 2014.
Ripoti ya CAG ilibaini ubadhirifu huo baada ya ukaguzi aliofanya Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, mashirika ya umma, miradi ya maendeleo na ufanisi wa maeneo mbalimbali. Ripoti hiyo ilikuwa doa kwa CCM hata kukilazimisha chama hicho kihubiri mabadiliko wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana, kikieleza kuwa viongozi watakaochaguliwa watafanya mabadiliko ili kuzuia ubadhirifu kama huo.
Lakini katika hali ya kushangaza, CCM hiyo hiyo inayojinasibu kumuunga mkono Rais Magufuli katika kutumbua majipu, ndiyo hiyo inayompinga kupitia Bunge; hili halikubaliki.
Moja ya mabadiliko ya msingi wananchi wanayoyahitaji ni pamoja na kuzuia wizi wa kila namna serikalini na kwenye sekta ya umma kwa ujumla, hili litawezekana kama Mihimili yote itashirikiana; tafadhali Bunge lisituangushe. Mungu Ibariki Tanzania.