Maelekezo ya lengo hilo yanazitaka serikali kuhakikisha ifikapo mwaka 2030, zimetokomeza umaskini uliokithiri kwa wanaoishi kwa kipato chini ya dola 1.25 (kwa siku) aidha, idadi ya wanaume, wanawake na watoto wa kila umri wanaoishi katika hali ya umaskini inapungua angalau, kwa kuwa wote wana haki sawa za kiuchumi na upatikanaji wa huduma za msingi.
Kadhalika, serikali inatakiwa kutambua wananchi wanaoishi katika umaskini, ili kuelekeza rasilimali na huduma kwao, kwa ajili ya kuwasaidia kuepuka hali hiyo na kuwajengea uwezo watu maskini na kuwaimarisha.
Katika kufanikishaa lengo hilo, Tanzania, haijabaki nyuma, kutokana na uamuzi wake wa kukusudia kuwekeza katika makazi ya wazee ili kuwa na miradi mbalimbali itakayozalisha mazao na kuchangia katika mapato ya serikali.
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Zanaib Chaula, anasema anapozungumza na wana habari baada ya kuzungukia makazi mbalimbali ya wazee.
Anasema kuna makazi 14 nchini yanayosimamiwa na serikali, ili kuweka mikakati na mbinu mbalimbali zitakazosaidia makazi hayo kuwa na huduma bora na kuwekeza nguvu katika miradi ya kilimo, mifugo na uzalishaji mali katika makazi hayo.
Miongoni mwa makazi hayo ni Nunge Dar es Salaam, Kolandoto Shinyanga, Njoro Kilimanjaro, Magugu Manyara, Kiilima Kagera, Fungafunga Morogoro na Sukamahela Singida. Ninaamini kuwa, uwekezaji wa miradi ya maendeleo katika makazi ya wazee ni hatua nzuri, kwani itaipunguzia serikali baadhi ya gharama zikiwamo za chakula.
Kwa mfano, inaelezwa kuwa baadhi ya makazi ya wazee yana ekari 10 ambazo zinaweza kutumika kwa shughuli za kilimo cha mboga, ufugaji wa kuku na miradi mingine ya kimkakati.
Iwapo kilichukusudiwa na serikali kitatimia, ni wazi kila makazi yanaweza kuinuka kiuchumi na hata kusaidia wazee kuwa na afya bora inayotokana na vyakula na mboga ambazo zitakuwa zinalimwa katika makazi hayo.
Lengo hilo namba moja halitaki mtu kuachwa nyuma kiuchumi, kwani linataka kuwapo kwa matokeo chanya kwa wote, hapo ndipo unapokuja umuhimu wa kuboresha makazi ya wazee kwa kuyaanzisha miradi.
Nakumbuka katika bajeti ya mwaka 2021/2022, Wizara ya Afya ilitenga Shilingi bilioni 7.4, kwa ajili ya kuboresha makazi ya wazee taarifa ya Waziri Dk. Dorothy Gwajima alioiwasilisha mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, ilisema kuwa huduma za chakula na mahitaji ya msingi vimeboreshwa.
Kwamba uboreshwaji huo umekwenda sambasamba na kuanzisha miradi ya bustani na ufugaji ambayo hutekelezwa na kusimamiwa na wazee wenyewe, hatua ambayo inaweza kuinua uchumi wao.
Anaeleza kuwa katika makazi hayo 14 yanayohudumiwa na serikali, kuna watumishi 93 wa kada mbalimbali na 19 kati yao maofisa ustawi wa jamii, ambao wanashauriwa kuwa wabunifu wa miradi katika makazi hayo.
Lakini pamoja na juhudi hizo kuinua uchumi wa makazi ya wazee, ingekuwa vyema iwapo jamii itawajibika katika malezi ya wazee, kwa kuwa sehemu salama na ya kwanza ya wazee ni katika familia zao.
Ninaamini kuwa wazee wanaweza kupata huduma bora na uangalizi mzuri kutoka kwa ndugu na familia zao, suala la kupelekwa katika makazi ya wazee iwe ni ya mwisho baada ya kukosekana wa kuwalea.



.jpg?itok=nfwjwDzv)






