Hii ni kutokana na majiji na miji kupambwa na marundo ya taka pembeni ya barabara, mitaani na ndani ya mitaro.
Kwa hali hiyo kunahitajika namna bora ya kuhifadhi taka kabla hazijachukuliwa kwenda kutupwa dampo.
Kila mara kumekuwapo na mazoea ya kuacha takataka kwenye maeneo hayo zikisubiri kukusanywa na kupelekwa dampo, lakini zikikusanywa na kuwa milima ya marundo ya uchafu mijini.
Taka hizo zinaachwa kando ya barabara lakini zinatumbukia mitaroni na hata nyingine kutokana na wingi wa milima zinasambaa hadi kwenye maeneo ya makazi zikirundikana kwa miezi kadhaa kusubiri gari la taka lifike kuziondoa.
Ni jambo jema taka hizo kukusanywa kwa utaratibu unaotumika lakini madhara yake ni makubwa katika jamii hasa wakazi wa maeneo jirani.
Kuna athari kama maradhi hii ni kutokana na taka zinavyorundikwa zinasababisha wadudu wachafuzi kama panya, mende, inzi na hata nyoka wanaozalia ndani ya marundo hayo.
Aidha taka, zinanuka na kuchafua hali ya hewa, huku majimaji zikichuruzika yakichafua mazingira na kusababisha kinyaa.
Taka kuachwa hadi kutoa harufu kali na kubakiza wadudu pale chini zilipokusanywa baada ya kuondolewa ni kero nyingine kwa mazingira.
Ni chanzo cha kusababisha maradhi mbalimbali kama kipindupindu, kuhara, kutapika damu, malaria na homa ya dengu kutokana na mazalia ya mbu.
Pia, husababisha uchafuzi wa hali ya hewa kwa kiwango kikubwa kwa sababu taka hizo zinapooza zinanuka na kuacha hali hiyo kwa muda mrefu.
Wakati umefika wa kuangalia njia bora ya kutupa taka hizo na kama makandarasi wakionekana wanafanya vibaya na hawatimizi wajibu ipasavyo mikataba yao isimamishwe na wengine wenye vifaa na vitendea kazi wapewe jukumu hilo.
Serikali inapaswa kulichukulia hatua suala hili si jambo jema kuendelea kuishi na taka kwa miaka mingi na historia kuonyesha kuwa Dar es Salam na miji mingine ya Tanzania ni michafu na hiyo ni kawaida yake.
Ni vyema serikali ikatenga maeneo maalumu na yenye miundombinu ya kisasa kwa ajili ya kuhifadhia taka kabla hazijachukuliwa na magari kutupwa dampo.
Kama likifanyika hilo ni matumaini yangu kuwa hakutakuwapo tena na mrundikano wa taka kando ya barabara kitu ambacho kinachafua mandhari na kushusha heshima ya taifa.
Mrundikano wa taka unasababisha kuwapo na kazi ngumu kwa magari ya taka ambayo yanajaa shehena za taka barabarani na hata kukera watumiaji wengine.
Ni vyema barabara ikabaki na suala moja tu la kupitisha vyombo vya moto na siyo kugeuzwa maghala ya taka.
Takataka barabarani ni maua yanayoonekana zaidi majiji ya Dar es Salaam, kuanzia kwenye barabara kuu na barabara za mitaa kama maeneo ya Mwananyamala kwa Mama Zakaria, kwa Kopa na kuelekea barabara ya Kinondoni.
Maeneo hayo imekuwa kama utamaduni kurundika taka kando ya barabara hadi zinaoza na kuwa kero zaidi wakati wa mvua.Nimetumia ukurasa huu adhimu kufikisha kilio cha wanajamii wengi ili serikali, wizara na mamlaka za afya kuangalia namna bora ya kuzihifadhi taka kabla hazijachukuliwa kwenda kutupwa dampo.
Unahitajika usasa zaidi kwenye kutunza taka na kutengeneza utaratibu ambao Watanzania wataachana na mazoea ya kukerwa na takataka kila wakati.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







