Kukubali matokeo kupewe  nafasi baada ya uchaguzi

10Aug 2022
Beatrice Moses
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kukubali matokeo kupewe  nafasi baada ya uchaguzi

MAJIRANI na wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kenya, wamemaliza uchaguzi mkuu unaotajwa na vyombo vingi vya  habari kuwa ni wa amani, utulivu na hali ya usalama.

Imedhihirisha  kwenye maeneo mengi nchini humo wakati wananchi wakitekeleza haki yao ya kidemokrasia, amani ilitawala.

Sasa kinachosubiriwa ni  matokeo ya uchaguzi huo na wapigakura wenyewe, pia nchi nyinginezo zikiwamo za ukanda wa Afrika Mashariki na marafiki wa nje na ndani ya Afrika.

Linalotumainiwa ni wagombea watakaoshindwa  watakuwa na hekima na uvumilivu badala ya kutawaliwa na jazba, chuki na pengine tamaa ya kujipatia madaraka hata bila ya kibali cha  sanduku la kura.    

Ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Kenya inatajwa kuongoza kwa maelezo kuwa iko  juu kiuchumi ikilinganishwa na mataifa mengine, hivyo matokeo ya uchaguzi huo ni muhimu yakapokelewa kwa amani na utulivu kwa kuwa ndiko kufanikisha, kuendelea na kutekelezwa kwa mipango iliyoko yenye lengo la kuimarisha mtangamano wa  Afrika Mashariki kwenye kibiashara na uchumi.

Mchuano mkali unabaki kwa wagombea William Ruto na Raila Odinga, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu anayepeperusha bendera  ya Muungano wa Azimio la Umoja, pia anaungwa mkono na Rais Kenyatta, na kwa  upande wake mshindani wake ni Naibu  Rais William Ruto, ambaye  anagombea nafasi hiyo kwa tiketi ya Muungano wa Kenya Kwanza, lakini akiacha historia ya kukwaruzana na bosi wake Rais Kenyatta. Wakati wa kampeni kali ya uchaguzi wagombea hao licha ya kushambuliana kwa maneno makali na kukosoana Odinga na  Ruto pia wameripotiwa mara kadhaa na vyombo vya habari wakisisitiza amani ili kuiepusha Kenya kuingia kwenye machafuko ya uchaguzi wa 2007/2008.

Kuwepo kwa  msisitizo huo waliouweka unaotoa matumaini kwamba wanajitambua vyema kwenye ushindani wakiamini kuwa kuna kushinda na kushindwa, hivyo atakayeshindwa asitumie nafasi yake vibaya kwa kuhamasisha machafuko nchini humo. Ni vyema nyakati za uchaguzi kila mmoja kuangalia mambo ambayo yamekuwa yakitajwa kuichafua Afrika kwa kuwa yamesababisha watu wengi kupoteza maisha na wengine kupata ulemavu wa kudumu, kukosa makazi na mali zao kupotea.Pamoja na kuchelewesha maendeleo kwa jamii na taifa, hivyo ni vyema  kukubaliana na matokeo ili kuepusha machafuko na kulinda amani na maisha ya watu.

Katika machafuko ambayo yanatajwa kusababishwa na kuenezwa kwa taarifa za  madai ya udanganyifu katika uchaguzi wa rais wa Desemba 2007, Kenya iliingia kwenye vurumai zilizochochea kuzuka kwa vurugu zilizosababisha Wakenya zaidi ya 1,500 kuuawa na wengine wengi kuwa  wakimbizi wa ndani. Iwapo machafuko yataibuka nchini humo  kutokana na matokeo ya uchafuzi, ni wazi kuwa miongoni mwa nchi hizo wanachama zitalazimika kupokea wakimbizi, hivyo zile fursa za ushirikiano wa kibiashara katika mazingira hayo zitakuwa zimelegea au kufungwa kwa muda usiojulikana, ndiyo maana  inasisitizwa kuwa matokeo yapokelewe kwa utulivu na uvumilivu. Bado zipo juhudi za kuwa na sarafu moja na soko la pamoja la Afrika Mashariki, kuna ujenzi wa miundombinu ya kuimarisha mtangamano na mengine mengi. 

Ikumbukwe mara  nyingi wanaokufa ama kujeruhiwa kwenye machafuko ya kisiasa wengi ni wananchi wa hali ya kipato cha kati na cha chini, kwa hiyo ni vyema raia nao wakaepuka kutumika na wanasiasa wanaotaka kama kutakuwa na jambo ambalo litabainika kuwa limefanywa isivyo lifikishwe kwenye vyombo vya sheria ili kuipata nafasi kufuata mkondo wake badala ya kufanya vurugu.