Na wale siyo miaka ya hivi karibuni tu kama kizazi cha sasa cha soka la kwenye mitandao ya kijamii wanavyotaka kuaminisha watu, ila hata ukirejea historia ya soka la Tanzania, hadi leo klabu ambayo inaonyesha kuwa inafanya vema zaidi ni Simba.
Ndiyo timu ambayo mwaka 1974 iliwahi kufika hatua ya nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika ambayo kwa sasa inaitwa Ligi ya Mabingwa, lakini kama haitoshi iliwahi kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) mwaka 1993.
Ukiachana na hapo ndiyo timu iliyotwaa hata Kombe la Kagame mara nyingi zaidi kuliko klabu yoyote ile Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Hata kuishia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa siyo kama imefanya kwenye miaka ya hivi karibuni tu kama baadhi ya wanavyodhani, imefanya hivyo mwaka 1994, kabla ya kutolewa na Nkana Red Delvis ya Zambia.
Ni kwamba linapokuja suala ya michuano ya kimataifa kwa ngazi za klabu, Simba ndiyo imekuwa timu pekee inayoiheshimisha nchi, achilia mbali ushiriki wao wa miaka ya hivi karibuni uliochangia kwa kiasi kikubwa kupeleka timu nne kwenye michuano hiyo.
Kwa maana hiyo ni lazima ipewe ushauri pale ambapo tunaona kuna tatizo ambalo labda kocha mpya Zoran Maki hajalifahamu vizuri na Selemani Matola analifumbia macho kwa makusudi, kwa bahati mbaya au kutokujua, lakini pia viongozi wa Simba wanashindwa kuling'amua.
Ni kwamba baada ya kuteleza msimu uliopita, viongozi wa Simba na benchi la ufundi wamesajili wachezaji wa hadhi ya juu kwa gharama kubwa, pia wenye uwezo mkubwa ambao umethibitishwa kwenye mechi dhidi ya St George Agosti 8 mwaka huu.
Simba ilishinda mabao 2-0 na baadhi ya mapungufu ya msimu uliopita yakaonekana kutatulika.
Kwa sasa timu ina viungo washambuliaji wengi wazuri, wabunifu na mawinga hatari kama ni Agustine Okra, Nelson Okwa, wakiunganika na kina Clatous Chama, Pape Sakho, Peter Banda, wakiungana na straika Moses Phiri na wengineo.
Tumemuona beki wa kati Mohamed Ouattara alivyoituliza beki kwa kiasi kikubwa.
Hata hivyo, Simba bado inaendelea kukosa kiungo mkabaji katili pale katikati mwenye nguvu, mapafu ya mbwa na kugongana na wachezaji wa timu pinzani, kuwapora mipira, kunusa hatari, ambaye kazi yake kubwa anayoifanya na kuipenda ni kuzuia zaidi kuliko kushambulia.
Wengine wanawaita wachezaji wa kazi chafu. Huyo ndiye mchezaji anayekosekana kwa upande wa Simba.
Mabeki wa Simba wanafikiwa kwa urahisi zaidi na wapinzani wao kwa sababu viungo wote wakabaji wa Simba waliopo, ni wale ambao wako vizuri wanapokuwa na mpira miguuni na si wakati hawana mpira.
Ni wavivu wa kukaba, kufuata wapinzani wanapokuwa na mpira, wana tabia ya kutegeana na waoga pia kuingiza miguu mpinzani anapokuwa na mpira.
Ukiwa una kasoro kama hizo, basi huwezi kuwa kiungo mkabaji mzuri na itakuwa ni hasara tu kwa timu yako.
Hata msimu uliopita, wachezaji kama Henock Inonga na Joash Onyango walipata shida sana kukabiliana na mastraika na mawinga wasumbufu kwa sababu walikosa viungo wa aina hiyo.
Nimeshangaa pamoja na usajili wote bado haikusajili kiungo mkabaji, sehemu ambayo ni muhimu mno kwenye soka kwani unaweza ukapata bao moja tu, ukafunga duka.
Ukiangalia hata timu kubwa kama Al Ahly, wanaweza kusajili wachezaji wazuri sana, lakini huwa wana viungo wao wakabaji ambao mara nyingi ni vipande vya watu kutoka Afrika Magharibi. Kazi yao hao ni kufanya uchafuzi tu pale kati. Hata TP Mazembe wanaye mtu huyo. Kwa sasa timu za Afrika Kaskazini maarufu kama 'Waarabu' huwa wanawachukua sana nchini Nigeria, Cameroon, Burkina Faso, Mali ambako wachezaji wa aina hiyo wamejaa mno.
Sina wasiwasi sana kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, kama Simba inakwenda na viungo wakabaji hawa waliopo, basi inaweza kutolewa mapema kwenye michuano hiyo na mashabiki wakaanza kupiga kelele kuwa usajili mbovu.
Kumbe haina watu kama Gerson Fraga, au Thadeo Lwanga yule wa mwanzo wakati anawasili.
Miaka ya nyuma ilikuwa na kina Abbas Kuka, Ramadhani Lenny, Idd Selemani 'nyigu' aliyefariki wiki hii na kuzikwa Manzese, Nico Nyagawa, Matola mwenyewe na wengineo.
Naamini Simba ikimpata kiungo mwenye akili ya kuzuia zaidi hata kama Zawadi Mauya tu, wala siyo Yannick Bangala mwenye uwezo mkubwa zaidi, basi inaweza kufika mbali.
Kwa hawa waliopo kina Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Sadio Kanoute, ama Victor Akpan ambaye naye si mkabaji halisi, bali ni namba nane, Simba itahenyeka sana kimataifa, hasa ikikutana na timu zenye kasi na zinazoshambulia mfululizo.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







