Ukifanyika mwaka 2020 katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, unabini kuwa takribani asilimia 60 ya wanafunzi ambao hawajui kusoma na kuandika wana changamoto ya kutoona kikamilifu.
Utafiti huo unaeleza kuwa walimu hawana ujuzi wa kuwawezesha kubaini changamoto hizo, hivyo hushindwa kuwapatia watoto hao afua (njia) wanazostahiki ili wamudu masomo yao, hali inayosababisha kumaliza darasa la saba bila kujua kusoma na kuandika.
Mkurugenzi Mkuu wa TET, Aneth Komba, akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, anasema kuwa hali hiyo inachangia baadhi ya wanafunzi kumaliza darasa la saba hawafahamu kusoma, kuandika majina yao, wala kuhesabu.
Anasema, kutokana na matokeo hayo serikali imetenga Shilingi milioni 82.64 kuandaa moduli za kuwafundisha walimu ili waongeze umahiri wa kuwabaini wanafunzi wenye changamoto zinazowarudisha nyuma wakati wa kujifunza katika ngazi ya elimu ya msingi hadi sekondari.
Ukiacha changamoto ya umahiri waliokuwa nayo walimu, wazazi na walezi kuna jambo la kujifunza kufuatia taarifa hii ya utafiti kwa kuwa hata wao wana nafasi kubwa ya kuchangia tatizo hili kutokea.
Wazazi na walezi, wafahamu kuwa zipo changamoto nyingi zinazomrudisha nyuma mtoto katika kujifunza si shuleni tu hata nyumbani, ikiwamo kukoseshwa raha na wanafunzi wenzie na hata kutengwa na kunyanyapaliwa kutokana na kasoro za maumbile walizo nazo.
Lakini, mtoto anashindwa kuzitolea taarifa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kutokuwa na mazingira rafiki kati yake na mzazi, mlezi au mwalimu hasa ukali uliopitiliza hivyo anaamua kuvumilia huku akirudi nyuma kimasomo.
Kuna haja ya wazazi na walezi kuongeza ukaribu, urafiki na upendo na watoto wao ili wawe huru kuwaambia pale wanapopitia changamoto au matatizo mbalimbali.
Mtoto akiwa huru kumwambia chochote hata kama atarudi usiku atahakikisha anasubiri ili aseme jambo lake.
Haiwezekani mzazi au mlezi unalea mtoto huyo tangu akiwa mdogo hadi anamaliza darasa la saba unashindwa kutambua kama anachangamoto ya uoni hafifu au kusikia.
Vilevile wazazi na walezi ni wakati wa kutenga muda wa kucheza na kushirikiana na watoto wenu ili kutambua matatizo yao na wanayoyapitia, itasaidia kwa wale wenye watoto wasioweza kujieleza kwa kuwa utaona kwa vitendo.
Suala la kumsaidia mtoto linahusisha pia kugundua changamoto zinazomkabili katika kujifunza na kuzitafutia ufumbuzi ni jukumu la mzazi na mwalimu.
Kwa maana hiyo, ikiwa mzazi umetambua mtoto anachangamoto ya uoni utakuwa umemsaidia mwalimu kulifahamu tatizo na namna gani ya kumsaidia mtoto huyo darasani.
Wazazi wengi wana dhana kuwa suala la elimu ni jukumu la mwalimu jambo ambalo si wakati ni la ukweli kwa sababu mtoto hasomi shuleni tu hata nyumbani ndiyo maana walimu wanawapa kazi za kufanya nyumbani ili kumpa nafasi mzazi kujua uwezo wa mtoto wake na kumsaidia.
Ni rahisi kumgundua mtoto mwenye uoni hafifu kupitia mwandiko wake na hata jinsi anavyotazama vitu vinavyomzunguka jambo linalohitaji wazazi na walezi kuongeza ukaribu kwa watoto wao ili kulibaini.
Ni wakati wa wazazi na walezi kuamka na kubeba jukumu hili muhimu la kumsaidia mtoto kupambana na changamoto zinazomrudisha nyuma kimasomo ili kutokomeza tatizo la watoto kumaliza darasa la saba bila kujua kusoma na kuandika.


.jpg?itok=nfwjwDzv)








