Wingi huo wa vyama, ulisababisha serikali kufikiria kuvipunguza, lakini Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere akasema hata vikiwa vingi kama utitiri ni sawa na kutaka viachwe, huku akiamini kwamba vingeweza kujifia vyenyewe.
Kwa sasa ni wazi utabiri wa Baba wa Taifa ulishatumia, kutokana na ukweli kwamba vipo ambavyo vilifutika vyenyewe bila kuguswa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, vipo vilivyofutwa na vingine vinaendelea kusuasua.
Ukweli ni kwamba umri wa miaka 30 tangu kurejeshwa kwa mfumo huo, ni mkubwa vilitakuwa kuwa vimeshakomaa na kuwa na uwezo wa kujiendesha, kwa kuwa miradi mingi na ofisi zake.
Lakini bahati mbaya, vingi ni kama havipo na vimebaki kusubiri kuibuka wakati wa uchaguzi na kukodi vyumba na kuvifanya kuwa ofisi za muda uchaguzi ukiisha, navyo vinarudi 'mafichoni'.
Kwa utaratibu kama huo, haviwezi kufika mbali, kwa sababu si rahisi viongozi wake kushawishi watu wakajiunga navyo na badala yake vinakuwa vinasindikiza vingine kana kwamba havina malengo.
Pengine ni wakati wa kutafakari walikojikwaa na kusababisha kuyumba ili kuchukua hatua.
Kuna sababu mbalimbali ambazo zimekuwa zikitajwa na wadau wa siasa kuwa zinachangia vyama kuyumba, kubwa ikiwa ni wanachama na viongozi wake kutofautiana kimawazo, kimtazamo na hatimaye kuzusha migogoro.
NCCR-Mageuzi ni miongoni mwa vyama vinavyokabiliwa na mzozo wa uongozi kwa sasa, ambao haujapata ufumbuzi.
Hatima ya migogoro hiyo huwa ni kufukuzana bila kujali kwamba, kila mtu ana mapungufu yake na pia suala la kutofautiana kimtazamo au kimawazo ni la kawaida na linaweza kusaidia kujenga chama.
Sidhani katika wingi wa watu wanaweza kuwa na mawazo au mtazamo wa kufanana, lakini utofauti ndizo ambazo zinaweza kusaidia kuimarisha chama iwapo kila mmoja atapewa nafasi ya kuelezea mtazamo au mawazo yake.
Ikitokea katika wingi huo watu kila jambo linakuwa ni ndiyo kila wakati bila kuhoji, ni wazi kutakuwa na sehemu ambayo haiko sawa, aidha kwa wanachama au kwa viongozi wa chama husika.
Hivyo, ni nafasi kwa viongozi wa vyama kutafakari kwa kina wakitambua kuwa miaka 30 ambayo vimekuwapo ni mingi, inatosha kuvifanya viwe imara badala ya kuonekana kama vilianzishwa juzi.
Ikumbukwe kuwa, chama ni wanachama, bila wanachama hakuna chama, hivyo, ni muhimu viwe na mpango mkakati wa kuhakikisha vinakuwa na wanachama wa kutosha watakaoviwezesha kushika dola.
Si vyema kuendekeza migogoro na kufurahia kufukuzwa kwa baadhi ya wanachama, kwani mtindo huo unachangia kudhoofisha vyama na kubaki vimedumaa kwa kukosa wanachama na wafuasi.
Uimara wa chama unategemea ukomavu wa kisiasa walionao viongozi na jinsi ya uendeshaji wa chama katika katika dhana na misingi ya demokrasia, uwazi katika ushiriki wa wanachama kukitumikia na kufanya maamuzi muhimu.
Kutofautiana kimtazamo, kimawazo ni jambo la kawaida, hivyo lisingefaa kuchukuliwa kama usaliti na kufikia kuzusha migogoro katika vyama, badala yake iwe ni fursa ya kujirekebisha.
Tanzania na vyama imara vya siasa visivyo na migogoro na vyenye malengo ya kushika dola inawezekana, iwapo kutakuwa na dhamira ya kweli, ni viongozi wenyewe wa vyama kutafakari na kuchukua hatua sahihi.



.jpg?itok=nfwjwDzv)






