Hiyo, inatokana na ukweli kwamba, wanafunzi ambao wamewahi kukaa makambini kwenye baadhi ya mikoa, walifanya vizuri na hivyo kuwawezesha kuendelea na masomo.
Wanafunzi hao ni wale wa shule za msingi na sekondari, ambao wamewahi kuwekwa katika kambi hizo lengo likiwa ni kuhakikisha ufaulu unaongezeka, ambapo kambi hizo zilisaidia kuleta matokeo chanya.
Hata hivyo, kwa sasa kampeni za kuhamasisha kambi hizo ni kama zimefifia, kwani hamasa zilizokuwapo katika mikoa mbalimbali miaka michache iliyopita hazisikiki tena, hali inaonyesha huenda wahamasishaji wamerudi nyuma.
Mkoa wa Simiyu chini ya Mkuu wa Mkoa, Anthony Mtaka, uliasisi kambi hizo kwa kushirikiana na wadau wengine wa elimu wa mkoa huo na kuibua kambi hizo za kitaaluma, hatua ambayo ilielezwa kuongeza ufaulu.
Kambi hizo ziliandaliwa kwa ushirikiano kati ya shule na wadau mbalimbali wa elimu wakiwamo wazazi na walezi, ambao walikuwa wakichangia vyakula na fedha ili kuhakikisha zinaimarika.
Mkoa huo uliwahi kushika nafasi ya 10 kitaifa katika matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha sita mwaka 2018, kutoka nafasi ya 26 mwaka 2017 ambapo mkoa uliendelea kuimarisha kambi hizo.
Ni wazi kwamba, wanafunzi kuwekwa kambini wanapata muda mwingi wa kujifunza na kujisomea, hali ambayo kwa namna moja au nyingine imasaidia kuongeza ari ya kupenda elimu na kuongeza ufaulu.
Ipo mikoa mingine ilioiga mfumo huo wa kambi za kitaaluma, lakini ninadhani kwamba zimeanza kufifia, kwani hazisikiki kama zamani, hali inayoonyesha kuwa huenda zimeachwa.
Ninaamini kuwa katika mazingira ya nyumbani kwa baadhi ya wanafunzi, hayawapi nafasi ya kujisomea wanaporudi nyumbani au siku za mwisho wa wiki, hivyo kambi hizo zilikuwa njia mojawapo ya kuwawezesha kusoma.
Wakati mwingine, kwa wanafunzi wa shule za vijijini, wanaweza kujikuta mwisho wa wiki wanapewa jukumu la kwenda kuchunga ng'ombe, kulima na shughuli nyingine za nyumbani, ambazo nazo ni muhimu, lakini ni vyema wakawa na muda wa kujisomea.
Njia mojawapo ya kuwafanya wawe na muda wa kujisoemea, ni hiyo ya kambi za kitaaluma, lakini nazo ni kama zimeanza kufifia, hivyo si vibaya waanzilishi wakaangalia ni wapi walikosea ili kuziwezesha kuwa na nguvu.
Ninaamini kwamba, mzazi au mlezi anayejua umuhimu wa elimu atakuwa tayari kuchangia kwa ajili ya kusaidia kuinua kiwango cha elimu cha mtoto wake ili aweze kusonga mbele katika masomo ya juu.
Elimu ni ufunguo maisha, elimu ni mali, dhana hizi na nyingine nyingi zinaonyesha jinsi elimu ilivyo ya muhimu kwa mwanadamu na ndiyo maana wale wanaowakatiza wanafunzi masomo huchulikuwa hatua za kisheria.
Kwa maana hiyo, ninadhani ipo haja ya kufufua kambi hizo, hasa kwa kuzingatia kwamba kule zilizoanzia zilisaidia kuwafanya wanafunzi kupata matokeo chanya katika mitihani ya taifa.
Uwapo wa kambi hizo mkoani Simiyu, ulichagizwa na zawadi kwa wanafunzi waliokuwa wakipata matokeo mazuri, hali ambayo iliwafanya wawe na hamasa katika masomo shuleni.
Hata baadhi ya wanafunzi walikuwa wakikiri kwamba, kambi hizo zilikuwa msaada mkubwa kwao hasa wale waliokuwa wakitoka katika mazingira magumu ambayo yaliyowafanya wasiwe huru kujisomea.
Aidha, kambi hizo pia zilikuwa msaada kwa wanafunzi wa kike kuepukana na vishawishi hasa wale waliokuwa wakitembea umbali mrefu kwenda shule na kurudi nyumbani ambapo kukaa sehemu moja kulikuwa ni nafuu kwao.
Kambi za kitaaluma zimeishia wapi? Kwa nini hazisikiki kama zamani? Kama zimekumbwa na changamoto, kwa nini changamoto hizo zisitafutiwe ufumbuzi ili ziendelee kusaidia wanafunzi?
Mbinu za ufaulu zipo nyingi, mojawapo ikiwa ni hiyo ya wanafunzi kuwekwa katika kambi ambazo kimsingi zilisaidia wanafunzi kufanya vizuri. Nadhani matarajio yangekuwa ni kuenea kwa kambi hizo nchi nzima.