Vilevile, ndani ya mtazano huo wa kuhakikisha jamii haikumbwi na magonjwa, viongozi wa serikali za mitaa nchini, nao wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wananchi kufanya usafi wa mazingira ndani ya maeneo yao.
Hiyo ni hatua inayoendana na kudhibiti mambo kama kufukia madimbwi ya maji, pia kuteketeza mazalia ya mbu yanayochangia kuongezeka mbu na ugonjwa wa malaria nchini.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, amesema jijini Tanga, alipozindua unyunyizaji wa viuadudu vya kibaiolojia kwenye mazalia ya mbu kwa wilaya za Tanga, Handeni na Lushoto, iliyofadhiliwa na serikali ya Uswisi, kupitia Shirika la Maendeleo la Uswisi.
Anasema licha ya kutekeleza unyunyiziaji huo wa viuadudu vya kibailojia kwenye mazalia ya mbu, bado jamii inahitajika kuboresha usafi wa mazingira, kwa kuangamiza mazalia ya mbu katika maeneo tunayoishi, hivyo viongozi wa serikali za mitaa wanawajibika kuhimiza usafi wa mazingira.
“Tukifunika madimbwi, itasaidia kuzuia magonjwa yaenezwayo na mbu, pamoja na magonjwa mengine kama dengue, matende na mabusha, homa ya bonde la ufa na chikungunya,” anasema.
Hata hivyo, Waziri Ummy anataka kutekelezwe usimamizi wa Sheria ya Afya ya Jamii ya Mwaka 2009 na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004.
Anasema, hatua hiyo ikifanyika kikamilifu, itasaidia kupunguza idadi ya mazalia, pia hata wingi wa mbu katika maeneo tunayoishi na hatimaye kupunguza maambukizi ya malaria na magonjwa mengine.
"Yeyote ambaye hatotekeleza wajibu wake katika kuharibu mazalia ya mbu achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria hizi," anasema waziri.
"Ugonjwa wa malaria bado ni tatizo katika nchi yetu. Hata hivyo, serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imefanikiwa kupunguza kiwango cha maambukizi ya malaria nchini, kati ya watu 100 wanaofika hospitali 10 wana changamoto ya malaria,"anasema.
Ufafanuzi wake unabeba maana kwamba, mradi huo utakuwa wa miaka miwili na utaweza kuleta manufaa yaliyokusudiwa, hivyo kuendelea na afua zingine za udhibiti wa malaria, ikiwemo ya kuwa na mazingira safi.
Lingine kutoka kwa waziri huyo ni kwamba, wizara hiyo kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria, unatekeleza mpango mkakati wa malaria wa miaka mitano, unaolenga kupunguza kiwango cha maambukizi ambapo mwaka 2012 kiwango cha malaria kilikuwa asimilia 14 na kupungua hadi kufikia asilimia 7.5 ilipotimu mwaka 2017.
Hapo ndipo Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Didier Chassot, mtazamo wake ni kwamba, wangependa kuiona Tanzania isiyo na malaria na ndio sababu wamefadhili fedha za kitanzania Sh. bilioni 400 kwa ajili ya kutekeleza hatua hiyo kwa kipindi cha miaka miwili, bega kwa bega na serikali nchini.
Hapo akasema, pamoja na juhudi za serikali na washirika wake, kuna ukweli unaobaki kwamba malaria ipo na inasababisha vifo, hata kufika hatua serikali ya Uswisi inaendelea kushirikiana na Tanzania katika harakati za kujikinga na kutokomeza malaria kitaifa.


.jpg?itok=nfwjwDzv)








