Ligi itakuwa ngumu kuliko msimu uliopita, ambao wachambuzi wa masuala ya michezo wanasema ulikuwa mgumu pia.
Inavyoonekana ni kila msimu unaofuata kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, unakuwa mgumu zaidi kuliko uliopita.
Hii ni kutokana na klabu zinavyojipanga, kuanzia kwenye usajili hadi maandalizi.
Ukitaka kujua klabu zimejipanga kwa ajili ya msimu ujao, anza kwa kuziangalia timu ambazo hapo awali zilikuwa hazisajili wachezaji kutoka nje ya nchi.
Awali ilikuwamo Mtibwa Sugar, lakini kwa misimu miwili iliyopita iliondoka huko, ikaanza kusajili wageni, japo haikufanya vyema sana.
Klabu za majeshi kama Tanzania Prisons na Polisi Tanzania, lakini safari hii zimeamua kuingia huko huko. Zinaona kama zinaachwa nyuma na zinabaki kuhangaika tu kwenye ligi.
Kwa mara ya kwanza Polisi Tanzania imemsajili mchezaji raia wa Uganda, Ambose Awio, katika kile kinachoonyesha hali imeshakuwa ngumu ni lazima sasa zishindane na klabu nyingine, vinginevyo zinaweza kuachwa mbali.
Prisons nayo katika usajili wake pia imesema itasajili wachezaji watatu kutoka Kenya. Hii si hali ya kawaida kwa klabu za Tanzania, si ndogo tu, bali hata za Taasisi za Majeshi.
Hii inaonyesha timu hizo nazo zinataka wachezaji wenye viwango vya juu zaidi ili kukabiliana na ushindani mkubwa kutoka kwa vigogo wa soka nchini, Simba, Yanga na Azam, ambazo zenyewe ni jambo la kawaida tu kushusha wachezaji zaidi ya 10 kutoka nje ya nchi.
Kwa ujumla ni kwamba zinataka kuleta ushindani kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara. Kwa maana hiyo ni lazima kuwa na uwiano mzuri kwenye uamuzi.
Kwa miaka kadhaa tumeona klabu za Simba na Yanga ambazo zinakuwa na wachezaji wenye viwango vya hali ya juu kuliko timu nyingine, lakini pamoja na hayo zinanufaika sana na makosa yanayoitwa ya kibinadamu ya waamuzi wetu nchini.
Ni makosa ambayo yanaziadhibu timu ambazo zinajikongoja kusajili wachezaji kwa gharama ndogo na uwezo wa kawaida, lakini pamoja na kujitutumua na kuleta ushindani wa kweli, wanajikuta wanaangushwa na maamuzi hayo.
Hivi karibuni, tumeona kwenye Uwanja wa Azam Complex, waamuzi wakitumia mfumo wa uamuzi wa video (VAR), kwenye Ligi ya Vijana chini ya miaka 20.
Mashabiki wengi walifurahishwa sana na jinsi ilivyotumiwa kwa ufanisi kiasi cha kupendekeza itumike pia kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Wakati wa kutangaza ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Ofisa Mtendaji Mkuu, Almasi Kasongo, pamoja na mambo mengine alisema kwa msimu huu haitowezekana kwa sababu ni lazima kwanza jambo hilo liingie kwenye mchakato.
"Kwenye mashindano ya U20 tulianza na mfumo huo wa VAR uliokuwa umefungwa na wamiliki wa Uwanja wa Azam Complex na kuwa wa mafanikio makubwa, lakini mimi kama Mtendaji Mkuu ni lazima niseme jambo hilo bado linahitaji mchakato mrefu. Tumefanya majaribio kwa vijana, tumewasiliana na wataalamu wa CAF na FIFA, tumewaambia kama tuna kitu kama hiki, wao baadaye wamesema watatuletea wataalamu ili kuja kutazama na kuthibitisha, kama ukikamilika na kuthibitishwa basi hatutosita kuuingiza kwenye mpango wa waamuzi wetu kuwasaidia kwenye kutafsiri sheria," alisema Kasongo.
Kwanza kabisa niwapongeze Bodi ya Ligi kwa kuwasiliana na CAF na FIFA kuwaambia Tanzania tumefikia hatua hii ya kutengeneza VAR yetu.
Inaonyesha ilikuwa na nia ya dhati itumike msimu huu, lakini sasa itabidi tusubiri wakubwa CAF na FIFA waje kuthibitisha.
Nawashauri tu Bodi ya Ligi wawe wanawakumbusha mara kwa mara ili waje kuitazama, angalau msimu ujao tuanze kuwa na VAR.
Inawezekana ikianza kutumika, yale mambo ya makosa ya kibinadamu yatapungua sana kwa sababu refa atakuwa na fursa ya kwenda tena kuangalia nini kimetokea, kabla ya kurekebisha au kuendelea na uamuzi wake.
Kwa jinsi timu zilivyosajili imefikia wakati sasa zishinde kwa uwezo wao na si uamuzi mbovu wa waamuzi.
Klabu zinatumia gharama kubwa sana kusajili na kuweka wachezaji kambini, lakini zinakuja kukatishwa tamaa na maamuzi yasiyo sahihi.
Mchakato wa VAR unahitajika uharakishwe ili kila timu ishinde kwa uwezo wake, na mashine hiyo ndiyo mwarobaini wa yote.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







