Kijana mmoja aitwaye Selestine, msomaji mzuri wa gazeti hili na pia safu hii, alinisimulia kisa kimoja cha kusisimua kuhusu shangazi yake aliyejifungua boga badala ya mtoto miaka kadhaa iliyopita. Akasema hivi Shangazi yake aitwaye Chrisanta alijifungua boga hospitalini jambo ambalo lilishangaza wengi. Na kisa cha mkasa huo ni kwamba alipora mume wa rafiki yake. MwanaMume huyo aliitwa Eliezeri Msafiri.
Baada ya rafiki yake huyo kugundua kuwa yule aliyekuwa karibu naye wakicheka na kushirikishana mambo mengi ana uhusiano na mumewe na anammiliki jumla, akatamka maneno yafuatayo: “Ikiwa wewe rafiki yangu umenitendea hivi, sitamwamini tena mtu yoyote, na utaona yatakayokupata.”
Shangazi akaendelea kuishi na mwanamume huyo akapata ujauzito. Alipokwenda hospitali kujifungua, badala ya kuzaa mtoto akazaa boga! Baada ya tukio hilo, babu wa kijana huyu akawaita wajukuu zake kuwapa taarifa hizo, kisha akawauliza, je, mnasemaje kiumbe hicho cha ajabu kiletwe nyumbani au kitupwe huko huko? Wakajibu, kiletwe tukione!
Wakati hayo yanaendelea, mume wa shangazi alishaongea na mfanyabiashara wa madini wa Mwadui, Shinyanga kuhusu hilo boga na kukubaliana atampa Sh. 500,000 kisha yeye atalipeleka mgodini. Hata hivyo, mama mzazi wa Eliezeri akashauri atafutwe mganga kufumbua hicho kitendawili, akapatikana mganga kutoka Burundi aliyetafutwa na Eliezeri.
Alipofika mganga huyo akatoa masharti yafuatayo; yatafutwe maziwa freshi lita 60 na ulezi usiopungua kilo tano kwa ajili ya kuchanganywa pamoja ili familia yote iogeshwe. Wakati huo, wazazi wa Selestine walikuwa wanaishi Tanga walikotafuta makazi mapya kwa kukimbia mauzauza ya kijijini.
Mchanganyiko huo kila aliyekuwapo aliogeshwa kuanzia kichwani hadi miguuni. Baada ya hapo mganga akasema litafutwe kaburi la mtoto mchanga kuanzia miezi sifuri hadi sita, lifukuliwe kisha kuchukuliwa sanda yake kwa ajili ya kwenda kulivisha lile boga! Baada ya sanda kuletwa ikaagizwa ifuliwe kwanza kisha shangazi na mumewe wapewe maji yaliyofulia hiyo sanda kila mmoja anywe nusu lita na maji mengine wayaoge usiku, jambo ambalo lilifanyika!
Ndipo ile sanda ikavishwa lile boga tayari kwenda kulizika kule kwenye makaburi ilikochukuliwa ile sanda. Waliokwenda kwa shughuli hiyo walikuwa mama yake shangazi, bibi wa Selestine, Eliezeri mume wa shangazi na shangazi mwenyewe aliyezaa boga hilo. Wote waliokwenda kuzika waliambiwa wasivae nguo yoyote mwilini. Waliporejea toka kuzika yule mganga akawauliza kama walikutana na kitu chochote njiani wakasema hakuna walichoona.
Akatoa masharti tena kwamba achinjwe ng’ombe jike tasa ili kipikwe chakula watu wale. Alipoletwa na kuchinjwa, akachukua damu ya ng’ombe akawapaka wote kwenye paji la uso na kuwatamkia kwamba mikosi na nuksi vyote vimekwisha!
Mpenzi msomaji wangu, kisa hiki kina mafunzo mengi kwa maisha yetu tunayoishi leo. Labda nitaje maeneo kadhaa ya msingi niliyokazia macho. Awali ya yote, Mwenyezi Mungu katika moja ya maandiko yake anasema watu wangu wanaangamia kwa sababu ya kukosa maarifa. Bado watu wengi wako gizani fahamu zao zimefungwa kutambua madhara ya kile wakifanyacho.
Mungu ameweka amri zake akasisitiza kuwa tusiabudu miungu mingine ila yeye. Lakini bado watu wanaendekeza ushirikina wakiamini kuwa ndiyo njia sahihi kuwafanikisha kimaisha.
Familia ya shangazi hawakuwa washirikina lakini walijikuta wanaangukia kwenye boma linaloamini mambo ya uganga kuwa kinga yao. Angalia mume aliyempora ndiye aliyetaka kuuza lile boga, ndiye aliyetafuta mganga. Mungu anasema kwenye moja ya maneno yake, na alaaniwe anayemtumainia mwanadamu kuwa kinga yake. Pia akasema mwanamke mchawi asiishi. Wote waliokwenda makaburini kwa kisa hiki walishatangulia mbele za haki.
Jambo lingine la kujifunza ni kuhusu nguvu ya maneno. Maneno aliyotamkiwa shangazi ndiyo yaliyoharibu hatma ya maisha yake. Maneno aliyotamkiwa na rafiki yake kwamba “utaona kitakachokupata’ yalikuwa ni mwiba mkali uliozima ndoto ya shangazi yule. Tumtafute sana Mungu ambaye anaweza yote.
Msomaji wangu, tuishie hapa. Wiki ijayo nitakuletea kisa kingine cha kijana huyu huyu kuhusu maisha yake. Je, una maoni, kisa? Ujumbe mfupi 0715268581.

.jpg?itok=nfwjwDzv)









