Licha ya kuwa na maadhimisho kitaifa yanafanyika jijini Mbeya, kila kanda maadhimisho yanaendelea kwa taasisi, mashirika, watu binafsi na wakulima mmoja mmoja kuonyesha kazi zao ambazo ni muhimu kwa taifa.
Unapotembelea maonyesho hayo utaona kazi nzuri za shambani ambazo unatamani mavuno yangekuwa hivyo siku zote.
Kama haitoshi kuna mashamba darasa ambayo kila halmashauri ina shamba lake imepanda zao la mfano ambalo ni kwa ajili ya kuwafundisha watu wanaotembelea maonyesho hayo.
Aidha, watafiti hubainisha utafiti waliofanya na kwa namna gani zinaweza kuleta matokeo chanya ikiwa zitafika kwa wakulima na hivyo kuboresha au kuongeza uzalishaji.
Pia wabunifu mbalimbali huonyesha kazi walizozifanya ambazo zina nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko kwenye jamii, kutoa suluhisho la mambo mbalimbali kwa kutumia gharama ndogo kuliko kuagiza teknolojia kutoka nje.
Kwa ujumla, maadhimisho ya Nanenane ni muhimu sana kwa maendeleo yetu, ikiwa yatatumiwa vyema itasaidia sana elimu kuwafikia wengi kwa urahisi.
Mathalani, Aprili, mwaka huu, serikali iligawa pikipiki kwa maofisa ugani nchi nzima, lengo ni kuhakikisha wanawafikia wakulima kwa haraka na kutoa elimu sahihi ya ugani ambayo itaboresha kazi zao.
Pia, kwenye bajeti ya Wizara ya Kilimo, vimewekwa vipaumbele kwa mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya kuleta mapinduzi kwenye kilimo, kuimarisha utafiti na ubunifu utakaotoa suluhisho kwenye matatizo ya jamii.
Naamini vipaumbele hivyo vikitekelezwa kwa dhati nchi itapiga hatua kubwa kwenye uzalishaji wa chakula na kuyafikia masoko kwa urahisi zaidi, hali itakayobadili maisha ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Nawaza kwa kiasi gani mashamba ya kwenye maonyesho yanasaidia kubadili kilimo. Mara nyingi utaona mashamba ya halmashauri yana mazao mazuri sana lakini ukitembelea maeneo yao halisi hawana hayo mazao na uzalishaji ni wa chini.
Unapotembelea maonyesho hayo utaona mazao mazuri sana kiasi kwamba unapokwenda kwenye mashamba ya wakulima huyakuti huwa najiuliza yanaandaliwa kwa ajili ya maonyesho tu au ni uzalishaji endelevu.?
Natambua gharama kubwa sana hutumika kuandaa maonyesho hayo kuanzia watumishi wanaosafiri kulipwa posho, mafuta ya magari, nauli na gharama zingine za uendeshaji.
Ni muhimu ubora wa mazao unaoonekana ukawafikia wakulima kwamba mbinu za kuboresha mazao katika eneo dogo zikaelekezwa kwenye mashamba ya wakulima, naomba 'waambukizane' elimu hiyo muhimu ambayo itawawezesha kuboresha kilimo.
Tuko katika wakati wa mabadiliko ya tabia nchi, mvua hazitabiriki na wakati mwingine hazinyeshi kabisa, kiasi cha maji kimepungua hali ambayo ni ngumu kwa wazalishaji wote yaani wanaotegemea mvua na umwagiliaji.
Lazima wakulima waelimishwe mara kwa mara ili kujua namna ya kuishi na mabadiliko ya tabia nchi, ambayo hayatarajiwi kuisha leo wala kesho ni suala la dunia ambalo litapunguza uzalishaji wa chakula kwa kiasi kikubwa.
Bila hivyo wengi wataendelea na kilimo cha mazoea ambacho hawatazalisha na kukata tamaa, lazima kuboresha uzalishaji ili watu wawe na uhakika wa chakula wakati wote.
Kilimo ni uti wa mgongo kinapaswa kuendelezwa ili zaidi ya asilimia 70 wanapotegemea shughuli hiyo wazalishe kwa tija na kibiashara, kwa kuwa mahitaji ya chakula ni ya kila siku.
Mungu ibariki Tanzania



.jpg?itok=nfwjwDzv)








