Wakulima ni tegemeo kubwa kwa nchi mbalimbali kwa kuwa ndiyo wazalishaji wa mazao kuanzia ya chakula na biashara, wanyama na rasilimali za viwandani, hata hivyo kwa sababu mbalimbali hasa wakulima nchini wanajikuta kwenye nyakati ngumu kipindi cha kuvuna na kuuza mazao yao.
Ni tatizo linalowakumba kutokana na shinikizo ambalo wamekuwa wakilipata kutoka kwa wafanyabiashara wakiwamo madalali wa mazao wanaotajwa kuwa huwalazimisha kuwauzia bidhaa kweye ujazo zaidi au kwa uwingi zaidi na huo ndiyo mwanzo wa lumbesa.
Lumbesa ni kujaza mazao zaidi ya kipimo kilichowekwa kwenye gunia, kiroba na ndoo ni kujaza na kushindilia hadi kumwagika, jambo linalofanywa kwa makusudi ili mnunuzi apate zaidi tena kwa kulazimisha na kumuumiza mkulima, anayepata kiduchu tofauti na mavuno ya mazao wanayouza.
Serikali kwa muda mrefu imeliona hilo ambapo viongozi kadhaa wa ngazi tofauti wamejitokeza kulikemea na limeripotiwa kwenye vyombo vya habari mbalimbali na kupigwa marufuku lakini bado mkulima anaumizwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Agosti mwaka jana akiwa katika kijiji cha Ilolo kilichoko kata ya Kiwira mkoani Mbeya alizungumza na wananchi katika eneo hilo ambao miongoni mwa mazao wanayolima ni viazi mviringo ambavyo pia vinafungashwa kwa utaratibu wa lumbesa.
Katika mazungumzo hayo Waziri Mkuu hakusita kuzungumzia lumbesa na kukemea kuwa ni wizi kwa wakulima, hivyo akatoa maagizo kwa Wizara ya Kilimo kusimamia matumizi ya mizani hasa kwenye masoko ya vijijini .
Jambo hilo limezungumzwa na Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, akiwa kwenye maonyesho ya Nane Nane wiki hii mkoani Morogoro, akisema ununuzi wa mazao kwa lumbesa, uishe na mazao yote yanunuliwe kwa vipimo vya mizani na si vinginevyo.
Ni wazi kuwa serikali imesikia kilio cha wakulima kuhusu kipimo hicho, ambacho ni wazi ukitafakari kinawasababishia mateso na umasikini kwa kuwa hawanufaiki ipasavyo ikilinganishwa na nguvu walizotumia kuandaa, kupanda hadi kuvuna mazao hayo.
Ni jambo la kusikitisha kuona kwamba licha ya viongozi kupiga marufuku bado magunia ya lumbesa ya aina mbalimbali yamejaa sokoni, hapo ndipo kuna zua maswali je viongozi wa masoko hawatambui hilo na kushiriki kudhibiti? Je Wizara ya Kilimo na Biashara zinafanya juhudi gani kukomesha jambo hilo ili kumkomboa mkulima dhidi ya wizi huu wa wazi?
Ifike wakati wahusika wawajibishwe ili mkulima apate haki yake kwa kuwa hadi lini viongozi wataendelea kupaza sauti jambo hili lidhibitiwe lakini kumekuwa na hali ya kusuasua katika kulikomesha, kilio cha wakulima siyo cha samaki kwamba machozi yanaondoka na maji, kwa kuwa wao ni miongoni mwa watu tegemeo kwa afya na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Sasa isisubiriwe kusikia Rais Samia Suluhu Hassan, naye anapiga marufuku jambo hilo, hatua zinazostahili zichukuliwe, watendaji waone umuhimu, kulikomesha na kumaliza tatizo hilo sasa.
Sheria ya kupiga marufuku upakiaji wa mazao na bidhaa kupita ujazo au uzito katika magunia ipo tangu mwaka 2016, je haina ‘meno’? Inahitajika kuona umuhimu wa uwepo wake katika nchi kwa kusaidia wakulima. Ni vyema sheria hiyo itumike ipasavyo kukomesha lumbesa.


.jpg?itok=nfwjwDzv)







