Mathalani, imezuka tabia ya ajabu sana kwa baadhi ya watendaji wa serikali mkoani kwamba, mwandishi wa habari hawezi kupata habari kwa Mkuu yeyote wa Idara hadi Katibu Tawala wa mkoa husika au Mkurugenzi aidhinishe hata kwa masuala ya kawaida kabisa yanayohusu utaalamu aliosomea mtendaji husika kama atatakiwa kutoa maoni yake kwa manufaa ya wananchi.
Kwa kufanya hivyo, mnatupa kazi ngumu ya kuwaeleza Watanzania wanavyongozwa na watu wasioaminiana kiutendaji. Mkuu wa Idara naamini ndiye mhusika namba moja katika eneo lake anapaswa kujibu au kuuelezea umma kuhusu utendaji wa shughuli zake kupitia vyombo vya habari.
Katika mazingira kama hayo, ikiwa Mkurugenzi au Katibu Tawala akitaka kila maelezo ayatoe yeye kwa hofu kwamba mhusika ataeleza anachokiona yeye, basi ni uamuzi ambao unafaa kutazamwa kwa umakini sana faida na hasara zake.
Kuna nini kinachofichwa ambacho mwandishi wa habari hapaswi kukihoji kwa watendaji wa chini hadi viongozi wa juu mkoani waidhinishe?
Kumbe kwa kufanya hivyo, wamekuwa wakiwanyima haki Watanzania ya kupata habari sahihi kwa wakati muafaka.
Inasikitisha kwamba, mwandishi wa habari anakwenda kutafuta habari, ambazo zipo kwenye ngazi husika, lakini anaanza kupewa mlolongo wa kujaza fomu na kuandika barua kana kwamba anakwenda kuomba mkopo.
Naamini kila mmoja ana mipaka yake, katika kazi na hiyo inatambulika na kuheshimika, lakini busara pia inapaswa kutumika hasa kwa kuona kwamba habari zinazotafutwa si kwa maslahi ya waandishi au vyombo vyao vya habari, ni kwa maslahi ya umma wa watanzania wanaolindwa na haki ya msingi ya Kikatiba katika kupata habari.
Katibu Tawala ni mtendaji wa ngazi ya juu mkoani, kimsingi muda mwingi anakuwa na shughuli mbalimbali, hivyo sio muda wote ataweza kutoa habari kwa waandishi.
Halikadhalika, Mkurugenzi, sasa huu urasimu wa kuminya uhuru wa kupata habari ni kwa maslahi ya nani? Silazimishi kila habari ipatikane la hasha.
Kuna habari kutokana na unyeti wake ziendelee kusubiri vibali ili zitolewe, lakini zile za kawaida ziachwe kutolewa na watendaji wenye dhamana na maeneo yao.
Kwa nini hamuwaachi wanaohusika wakajiwajibisha wenyewe kwenye nafasi zao, kwa sababu nyakati nyingine kutokana na kubanwa na maswali ya waandishi, na ili kuficha madudu wanayofanya, wanapata sababu ya kusema au kujibu kwa haraka kwamba wao si wasemaji. Kumbe hiyo ni namna mojawapo ya kukwepa maswali au kuhojiwa.
Ieleweke kwamba, waandishi wa habari si adui wa serikali. Wapo kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yao kama watu wengine ndani ya jamii. Hivyo viongozi na watendaji wa serikali, wana kila sababu ya kuwapa ushirikiano wakitambua wazi kwamba, macho ya Watanzania na masikio yao ni kwa vyombo vya habari.
Tabia ya kutaka kuwakweza waandishi wa habari kwamba ni watu muhimu nyakati za uchaguzi tu ni mbaya na haina tija hata kidogo. Kwenye uchaguzi wagombea wanafunguka kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa waandishi na vyombo vya habari kwa ujumla, baada ya hapo wanajitenga na waandishi na vyombo vya habari tuwaeleweje?
Vyombo vya habari vipo kwa mujibu wa sheria. Na vinatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia taratibu zote za kisheria.
Tunamwomba Waziri mwenye dhamana alione hili na kulichambua kwa kina, kwani linaleta maswali kwa waandishi na Watanzania kuhoji kuna nini ndani ya serikali ambacho umma haupaswi kukijua? .


.jpg?itok=nfwjwDzv)








