Hifadhi ya mazingira idumishwe kutunza uoto wa asili

18Feb 2016
Gwamaka Alipipi
Nipashe
Mjadala
Hifadhi ya mazingira idumishwe kutunza uoto wa asili

UNAPOSAFIRI kuelekea mikoa ya Kaskazini, baadhi yetu siku hizi tunaamua kutumia barabara mpya ya Bagamoyo-Msata.

Kwa wale ambao wamekuwa wakiitumia kwa muda mrefu watakubaliana nami kuwa kwa kipindi hicho chote, tangu wasafiri waanze, kuitumia kumekuweko na mabadiliko tele ya muonekano kando kando ya hiyo barabara.

Awali barabara ilizingirwa na misitu midogo kwa mikubwa na maeneo machache yalikuwa ni makazi ya watu. Lakini sasa ni maeneo machache sana utashuhudia misitu ya asili mingi imefyekwa, kwa kigezo cha uendelezaji maeneo. Huku sehemu nyingine kunaonekana kweupe kabisa kwa umbali wa upeo wa macho.

Huu ni mfano mmoja tu, kati ya mifano mingi ambayo nimeiona katika mikoa mbalimbali nchini iliyokuwa na maeneo mengi ambayo miaka ya nyuma yalikuwa bado “hayajaendelezwa”.

Imekuwa ni kawaida kwa serikali za vijiji na sasa serikali kuu kusisitiza kuhusu uendelezaji mashamba, tujiulize maswali machache, kwanza hii dhana ya kuendeleza mashamba ni mpya au ni ya muda mrefu? Dhana hii inatokana na nini hasa?

Mwongozo wa kuendeleza mashamba ukoje? Nani anatakiwa kusimamia dhana hii? Nini matokeo yake kwetu na kwa vizazi vijavyo?

Nikianza na dhana ya umiliki wa mashamba, utaona mashamba mengi ya maeneo ya vijijini yana umiliki wa aina nyingi.

Hapa tutaangalia umiliki wa aina tatu tu. Umiliki wa kwanza ni ule wa wanakijiji mmoja mmoja, ambao hulima kufuatana na misimu, aina ya mazao na mahitaji ya masoko.

Mashamba haya kimsingi umiliki wake ni ule wa kiasili wa kurithi na wakati mwingine kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu, basi watu wanahamia mahali wanaanza kulima.

Umiliki wa pili ni ule wa watu wanaojulikana kama wageni ambao sio wakazi wa kijiji kile, kununua mashamba madogo madogo. Hawa makazi yao wengi ni mijini, huenda kununua sehemu katika vijiji na wanavijiji wenyewe na kuwepo na idhini ya uongozi wa kijiji.

Umiliki huu una matatizo matatu, la kwanza ni ununuzi usio na malengo ambao kutokana na wimbi la watu kutaka tu kumiliki ardhi. Wengine wananunua sehemu hizi ili pindi wanapostaafu iwe ni kama sehemu ya kianzio cha uwekezaji.

Umiliki wa tatu ni ule wa uwekezaji. Umiliki huu maeneo yake ni makubwa na hufuata ngazi mbali mbali hadi mwekezaji kumiliki. Umiliki huu huwa na malengo yaliyo wazi na wanakijiji hujua tangu mapema . Umiliki huu mara nyingi hufuata sheria zilizopo ikiwemo sheria ya kumiliki eneo, kupata hati na wakati mwingine kibali cha uwekezaji.

Maeneo haya mara nyingi huanza kazi kwa kufanya upembuzi yakinifu na pia kupata vibali toka Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) ili kuona athari za kimazingira za mradi husika na hatua zitakazochukuliwa na mwekezaji kupunguza athari hizo.

Pia wamo wale ambao wanaanza kama wawekezaji, lakini uwekezaji unakwama kwa sababu mbalimbali. Pia wamo wale ambao kwa malengo mabaya wanachukua mashamba ili kupata mikopo mikubwa kisha kuyatelekeza.

Kila umiliki una changamoto zake na namna ya kuzishughulikia. Lakini changamoto naiona ni kubwa, ni ile ya kutunza maeneo yetu ili yawe mazuri ya kutosha kurithiwa na vizazi vijavyo.

Umiliki wa mwanakijiji mmoja mmoja, athari hizi hazionekani maana aidha wanafundishwa au wanajua namna ya kuweka mazingira kuwa endelevu kwa kupanda miti na kuzuia mmomonyoko wa udongo. Pia wanajua mahitaji yao ya miti kwa ajili ya matunda na shughuli nyingine za kimaisha.

Kwa uwekezaji mkubwa, kazi hiyo imerahishwa maana lazima uwe na kibali kutoka NEMC ndipo uanze kufanyia kazi eneo lako. Kwa uwekezaji mdogo hasa huu wa umiliki wa wageni, hakuna usimamizi makini katika kuhakikisha mazingira yanatunzwa.

Imefanyika kampeni kubwa ya kusafisha mashamba pori. Kampeni hii inalenga kuweka mashamba katika hali ya usafi.

Lakini utekelezaji wa kampeni hii, unaonekana kuwa na changamoto nyingi, kubwa kabisa ni ile ya kuharibu mazingira ambayo usimamizi wake haujaangalia athari za kimazingira. Miti inakatwa ovyo, misitu inateketea, na uoto wa asili unaangamia.

Kampeni hii inasimamiwa bila kuwepo miongozo bayana ya maana halisi ya kuendeleza mashamba. na wale wanaoitekeleza, hususan ambao wengi wao ni wageni, wanatumia nguvu kubwa kusafisha, wakiacha ardhi nyeupe kabisa isiyokuwa na miti ambayo huleta mvua, uoto utakaozuia momonyoko na vivuli na chakula ambavyo vitatunza viumbe hai rafiki wa mazingira.

Matokeo yake ni kama yanavyoonekana pembezoni mwa barabara kutoka Bagamoyo hadi Msata na nyinginezo ambazo misitu imekatwa, mashamba yamesafishwa kwa kisingizio cha uendelezaji mashamba huku yakiacha ardhi tupu yenye rutuba ikiharibika.

Ni vema mamlaka husika zikatoa maelekezo maalum kwa viongozi wa vijiji na wasimamizi wa undelezaji huu kuhusu namna bora ya “kuendeleza” mashamba bila kuathiri mazingira.

Maelekezo haya yalenge katika kutunza miti ya asili, kupanda miti mipya, kupanda miche na mimea itakayozuia mmomonyoko wa udongo.

Pia kuhakikisha viumbe hai rafiki wa mazingira vinatunzwa. Visingizio kuwa mashamba pori yana athari kwa vijiji husika inaweza kuwa kweli, lakini kisiwe ndicho chanzo cha kuanzisha majangwa yasiyotarajiwa.