Sekta ya uvuvi iwezeshwe kikamilifu

18Feb 2016
Lulu George
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Sekta ya uvuvi iwezeshwe kikamilifu

SEKTA ya Uvuvi ni miongoni mwa sekta nyeti sana nchini ambazo kwa undani wake zimekosa kisemeo, licha ya mchango wake mkubwa kwa Serikali,Taifa na jamii kwa ujumla.

Sekta hii kimsingi ilipaswa kuwa na muundo wa wizara yake maalum . imekuwa ikitegemea kurudishiwa makombo badala kula vitu stahiki yake, ambavyo serikali imekuwa ikikusanya kupitia uvuvi na wavuvi.

Ni ukweli usiopingika kwamba, bajeti ya serikali inayotengwa kwa ajili ya sekta ya uvuvi haitoshelezi. Ni keki ndogo sana inayopelekwa kwenye Halmashauri ambayo pengine huishia katika mafungu ya wakurugenzi wa halmashauri husika na ambao fedha hizo huzipangia shughuli nyingine tofauti na malengo yaliyotakiwa kutekelezwa .

Ukiangalia mfumo wa serikali kwenye Halmashauri, wakuu wengi wa idara kwa upande wa kilimo na mifugo.

Aidha wataalamu wa kilimo au mtaalamu wa mifugo jambo ambalo linaleta mkanganyiko mkubwa wa kimaslahi na utendaji kwani hata pale Ofisa uvuvi anapotaka kumshauri Mkuu wake wa idara kuhusiana na mahitaji yake ya wavuvi, hawezi kueleweka huku ikikumbukwa bayana kabisa kwamba, hata wanaoingia kwenye vikao vya bajeti katika ngazi za halmashauri ni wakuu wa idara ambao baadhi yao wanaenda kusema ya kwao na si kuwasilisha mahitaji halisi ya wavuvi.

Tunafahamu kwamba, mahitaji ya wavuvi na ili kuufanya uvuvi uwe endelevu, ni lazima changamoto mbalimbali zitatuliwe ikiwemo kuwawezesha maofisa uvuvi kufanya kazi zao kwa uhuru kulingana na mahitaji ya sekta hiyo alimradi wanazingatia sheria.

Inasikitisha kuona kwamba, Ofisa uvuvi katika halmashauri zinazoguswa moja kwa moja na sekta hiyo, anakosa boti hata ya kufanya doria kila wakati, matokeo yake wanasubiri msukumo wa oparesheni maalum za Kitaifa.

Kimsingi serikali ilifanya vizuri kuanzisha Kamati za Uhifadhi wa Mazingira na Rasilimali za Uvuvi (BMU ) ambazo kwa kiasi kikubwa, katika maeneo ambayo zimewezeshwa zimeweza kuokoa fedha nyingi zilizokuwa zikipotea kutokana na kukithiri kwa vitendo vya uvuvi haramu hata kwa wavuvi waliokuwa wakikwepa kulipa kodi ya serikali .

BMU zilianzishwa kwa Mujibu wa Katiba ya Nchi, Sera ya Taifa ya Uvuvi ya Mwaka 1997 na Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya Mwaka 2003, ambayo ilitamka kwamba, Usimamizi wa uvuvi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Shirikishi na kuwa Ulinzi wa raslimali za Taifa zikiwemo za uvuvi ni jukumu la wananchi wote na si jukumu la Serikali pekee, lakini cha ajabu zimetekelezwa kana kwamba hazitambuliki.

Niseme tu katika hili kuwa, iwapo serikali itaweka mikakati madhubuti na kuongeza rasilimali fedha kwenye sekta hiyo, ni dhahiri kuwa uvuvi utakuwa na tija katika kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla, hatua ambayo itafanya zao hilo kuwa endelevu.

Inashangaza kuona, licha ya kuwepo kwa kamati hizo kisheria lakini zimekuwa zikikabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo serikali haina budi kuzifanyia kazi, ili kuzipa uhai kamati hizo, ikiwemo suala la kuongeza bajeti zake ili hata wale wanaofanya shughuli za doria wapate kuhamasika katika ushiriki wa ulinzi wa rasilimali zao.

Serikali haina budi kuongeza nguvu ya hali na mali katika kamati hizo, hasa kwa kuzingatia kuwa, wananchi wameanza kuzitambua hivyo kufanikiwa kuwa, washirika wakuu wa masuala ya ulinzi na uhifadhi wa mazingira ya pwani na baharini, hali ambayo imesaidia kuwakusanya vijana na kufanya ulinzi shirikishi ambao lengo kuu ni kudhibiti vitendo vya uharibifu na uchafuzi wa mazingira.