Yaani wote wanaotumia barabara za jiji hili ni waathirika wa foleni. Watumiaji hao wanapokwenda katika shughuli za kujipatia riziki kuanzia alfajiri na hata majira ya jioni wanaporudi ni kero kwao kiasi cha kuwalazimisha watumie saa nyingi kuwa barabarani kabla ya kufika waendako.
Hali halisi ilivyo ni kwamba, mara nyingi majira ya asubuhi magari mengi ya binafsi na ya umma, huwa na uelekeo mmoja wa katikati ya jiji, jambo linalosababisha foleni kuwa kubwa kwa karibu watu wote wanaokwenda uelekeo huo.
Hali hii hufanya watumiaji wa barabara kukumbwa na hasara, ikiwamo mafuta ya gari kutumika zaidi, kupoteza muda ambao ungetumika kufanya shughuli nyingine za uzalishaji mali.
Baadhi ya watu wanazungumzia sababu nyingi zikiwamo ongezeko kubwa la watu jijini ambalo sasa ni zaidi ya milioni huku miundo mbinu ya barabara ikibaki ileile, kasi ya ununuzi wa magari imeongezeka kwa mujibu wa takwimu za Kikosi cha Usalama barabarani, jijini Dar es Saalam, magari yapatayo milioni moja hufanya safari za kila siku jijini.
Watembea kwa miguu ambao ni sehemu ya watumiaji barabara wanafikia 300,000 kwa siku, hivyo msongamano wa watu na magari ni mkubwa hata kuathiri usafiri na usafirishaji kwa ujumla.
Wataalamu wanaeleza kuwa zaidi ya Sh. bilioni sita hupotea kupitia nishati ya mafuta na muda unaopotezwa bila ya kazi kila mwaka.
Hivi karibuni, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, aliuthibitishia umma kuwa, ujenzi wa barabara za mzunguko zitapunguza msongamano wa magari katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Ujenzi huo unatarajia kukamilika Juni mwaka huu, kwa kiwango cha lami. Barabara hizo na urefu wake katika mabano ni barabara za Tangi bovu-Goba (km 9), Goba- Mbezi Mwisho (Km 7), Kimara Baruti-Msewe- Chuo Kikuu (km 2.6), Mbezi Mwisho-Malambamawili-Kifuru-Kinyerezi ( km14 ) na Tabata Dampo-Kigogo (km 1.6).
Serikali kwa upande wake alisema kuwa, imeanza kulipa madeni ya makandarasi na kuwataka warudi kazini mara moja ili kuhakikisha kuwa malengo ya serikali ya kukamilisha barabara hizo yanafikiwa.
Alitoa wito kwa wenye nyumba zilizo pembezoni mwa barabara za mzunguko kutoa ushirikiano ili kuhakikisha mipago inakwenda kwa wakati na kwamba wameorodheshwa kwa ajili ya kulipwa fidia.
Gharama ya ujenzi huo ni Sh. bilioni 56.3 fedha ambazo ni kwa ajili ya fidia na ujenzi walioufanya katika maeneo hayo.
Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads), inasema waendesha magari katika maeneo yatakayopita barabara za mzunguko wahakikishe kuwa hawaegeshi magari katika maeneo hayo.
Hata hivyo, ujenzi huo pia uzingatie, kutengwa kwa njia maalum za watembea kwa miguu, hali ambayo itasaidia kuwa na utaratibu maalum unaofahamika ambao watu wataufuata pamoja na waendesha vyombo vya moto ili kuhakikisha kuwa suala la usalama linapatiwa uzito mkubwa na wahusika wote wanaotumia barabara.
Waathirika wakubwa wa ajali za barabarani wamekuwa ni watoto wa shule pamoja na watu walio na ulemavu kwani baadhi ya madereva hawawaangalii kila wavukapo barabarani na kuhakikisha kuwa maisha yao hayaathiriwi hata kidogo.
Kwa mfano, ujenzi wa barabara kuanzia Mwenge hadi Tegeta ni umehakikisha kuwa unazingatia maeneo ya watembea kwa miguu kwani kuna utaratibu mzuri, jambo linalohitaji kuigwa na wakandarasi wote pamoja na serikali kutoa maagizo na msisitizo kwa wakandarasi hawa kutenga maeneo ya watembea kwa miguu ambao ni wadau muhimu wa barabara.Barabara sio kwa ajili ya watumiaji wa vyombo vya moto peke yake.
Elimu ya usalama barabarani, semina iendelee kutolewa kwa watumiaji wote wa barabara, ili iwapo kutatokea kuvunjwa kwa sheria hiyo zichukuliwe hatua kali za kisheria.
Kimsingi ninachotaka kusema ni kuwa, barabara hizo zijengwe hara iwezekanavyo ili kuhakikisha kuwa zinachangia kupunguza msongamano na hivyo kuokoa muda mwingi unaoendelea kupotea kila saa ya siku jijini Dar es Salaam


.jpg?itok=nfwjwDzv)








