Tambo, ubishi mwisho leo

20Feb 2016
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tambo, ubishi mwisho leo

“KINYWA ni jumba la maneno.” Ni methali ya kutukumbusha kuwa binadamu ana uwezo wa kusema maneno yoyote, yawe mazuri au mabaya. Kwa hiyo tusishangae kusikia maneno yanayosemwa na watu.

Makocha wa Simba na Yanga, viongozi, wanachama na mashabiki wamekuwa wakitamba (tembea kila mahali kwa kujifaragua), kila upande ukijigamba kushinda mechi ya leo Jumamosi. Ni mechi inayowakutanisha watani wa jadi yenye hisia na msisimko wa aina yake nchini.

Kutakuwa na mashahidi wa aina tatu watakaojua mbivu na mbichi leo baada ya tambo nyingi. Filimbi ya mwamuzi Jonesia Rukyaa wa Kagera baada ya dakika 90 za mchezo, dimba la Uwanja wa Taifa na watazamaji wa pande zote mbili.

Ni vema ijulikane kuwa “maneno ni daraja, hayazuii maji kuteremka.” Maana yake daraja haliwezi kuyazuia maji ya mto yasiteremke. Maneno nayo hayawezi kumzuia mtu kufanya jambo aliloazimia.

Mbali ya upinzani mkali kati ya Hamis Kiiza wa Simba na Amissi Tambwe wa Yanga kutaka kuonyeshana nani mkali kwa ufungaji, pia watazamaji wanataka kuona mpira ‘uliokwenda shule.’

Kiiza aliyetemwa na Yanga akielezwa kiwango chake kimeshuka, ndiye anayeongoza kwa ufungaji akiwa Simba na mabao 16 akifuatiwa kwa karibu na Tambwe ambaye naye aliachwa na Wekundu wa Msimbazi kwa sababu kama za kinara wa kupachika mabao na sasa ndiye anayefuatia kwa ufungaji akiwa amezifumania nyavu mara 14.

Kati yao ni nani atakayetoka kifua mbele leo baada ya mechi kwa kuongeza mabao ya kufunga?

Watazamaji wasiandikie mate na wino ungalipo. Mwenye kisu kikali ndiye alaye nyama. Maana yake aliyejiandaa vizuri ndiye anayeweza kufanikiwa katika jambo. Tunatakiwa tujiandae ipasavyo kabla ya kuliingilia jambo.

Wakati Simba wakipiga kambi ‘mji kasoro bahari,’ Yanga waliambaa kando kando ya bahari ya Hindi wakitokea Mauritius walikoshinda mechi ya mabingwa wa Afrika dhidi ya wenyeji, mpaka Pemba walipopiga kambi. Ni mji gani wenye futahi (bahati njema; ushindi) kati ya Morogoro na Pemba?

Mengi yamesemwa kuhusu mchezo huo ila watazamaji wanataka kuona mchezo wa kiungwana na ufundi. Atakayeshindwa akubali matokeo bila visingizio visivyo na msingi kwani kwenye ligi kuna matokeo ya aina tatu.

Nimefurahishwa na onyo alilotoa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa wanachama na mashabiki wa Yanga na Simba kutofanya uharibifu wa miundombinu kwenye Uwanja wa Taifa.

Aliwaasa watazamaji kukubaliana na matokeo yoyote kwani tabia ya kuharibu miundombinu, hasa timu moja inaposhindwa haitavumiliwa kwani serikali imetumia fedha nyingi kujenga uwanja huo.

Waziri Mkuu Majaliwa ameeleza masikitiko yake kuona viti vingi vya uwanja huo ama vimekwanguliwa au kuharibiwa na mashabiki wanaoshindwa kuvumilia timu zao zinapofungwa.

Hao wanaoharibu viti baada ya timu zao kushindwa hufanya hivyo ili kubadilisha matokeo na timu zao kushinda? Mambo mengine ni ya (ashaakum) kipumbavu, kiwenda wazimu na kihuni.

Onyo kama alilotoa Waziri Mkuu pia limetolewa na mkuu wa kanda maalumu ya polisi jijini Dar es Salaam. Amesema yeyote atakayeharibu kitu chochote uwanjani atachukuliwa hatua.

Pia ameonya dhidi ya tabia za mashabiki wanaotukana matusi na kurusha vitu uwanjani kwamba atakayehusika atakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.

Tabia ya kuharibu vifaa vya uwanjani, kutukanana matusi ya nguoni na kurusha chupa zenye mikojo uwanjani ni mambo yanayofanywa wazi lakini hakuna hatua wanazochukuliwa wakorofi hao ili kukomesha upuuzi huo.

Nimeandika mara nyingi kuhusu tabia zisizopendeza za askari wanapokuwa viwanjani. Wote husahau wajibu unaowafanya wawe viwanjani. Badala ya kufanya kazi iliyowapeleka huko, huangalia mechi kuliko kuangalia usalama wa wachezaji, waamuzi na watazamaji.

Kama wangekuwa wanaangalia runinga za wenzetu huko ughaibuni wangegundua kuwa askari wenzao huwa wanawaangalia watazamaji migongo yao ikielekezwa uwanjani. Huwa makini kuwaangalia wakorofi wanaoleta rabsha na mara moja huwakamata.

Huku kwetu mambo ni tofauti kwani hata wasiokuwa kwenye zamu, huvaa sare ili waingie bure uwanjani. Baadhi huonekana wakishirikiana na ‘makomandoo’ wa vilabu kuuza tiketi za bandia!

Kuna mengi ya kueleza kuhusu mashabiki wa Simba na Yanga lakini nafasi si rafiki kwangu. Yaniacha na dukuduku (joto la moyo linalosababishwa na kuudhika) kwa ukosefu wa nafasi ya kutosha gazetini.

marobarnabas@yahoo.com
0715/0784 33 40 96