Hata alipotoka, alikuwa mchezaji mzuri tu, ila nadhani anaonekana kuongezeka kiwango kwa sababu amejiunga na timu kubwa na kongwe nchini, Simba.
Lakini pia amekutana na wachezaji waliokomaa, wazoefu na wenye vipaji zaidi kuliko alikotoka.
Hii pia inaweza kumfanya mchezaji kuonekana kiwango chake kimepanda. Alimaliza ligi msimu uliopita akiwa na Mtibwa, akiwa amefunga mabao manane.
Hivi leo, tayari ana mabao saba kwa mechi tisa tu ambazo timu yake imecheza mpaka sasa.
Awali, pamoja na kufunga mabao, licha kwamba ni mcheza mwenye kipaji, alionekana kwa wapenzi na mashabiki wa Simba ni mchezaji wa kawaida. Lakini hali ilibadilika mara baada ya kufunga bao pekee dhidi ya Azam FC.
Hapo hata wale ambao si wafuatiliaji sana wa masuala la soka, walianza kufahamu jina lake.
Bao la kusawazisha dhidi ya Yanga ndilo kwa kiasi kikubwa lililomuweka winga huyo kwenye chati ya juu zaidi.
Kila mmoja sasa mwenye kufuatilia michezo hata kwa mbali, anamfahamu Kichuya. Katika kuonyesha kuwa hakubahatisha, alifunga tena mechi zilizofuata dhidi ya Mbeya City na Kagera Sugar.
Kwa sasa ukipita mitaani na hata kwenye mitandao ya kijamii ambayo watu wanajadili masuala ya soka, ndiyo jina linalotajwa zaidi.
Inawezekana kabisa ikawa ni hazina ya baadaye ya Tanzania kwenye soka kama hatolewa sifa.
Nilichoona kwa sasa tayari kuna kile kinachoonekana kumpa sifa za hali ya juu zaidi kwenye baadhi ya vyombo vya habari kiasi cha kumshauri aachane na soka la Tanzania na kwenda kucheza nje ya nchi.
Kwangu mimi naona kwa sasa bado mapema sana kumshawishi mchezaji huyo kwenda kucheza soka la kulipwa.
Ni kwamba amecheza mechi chache sana za Ligi Kuu na bado haijulikani kama mwendelezo kama huu atakuwa nao hadi mwisho wa msimu.
Wapo wachezaji ambao wanatamba kwa kipindi fulani halafu wanazimika, na wengine wanatamba kwa msimu mmoja na wanatoweka kwenye ulimwengu wa soka, au viwango vinashuka na kwenda kuchezea timu nyingine ndogo.
Wanaotaka Kichuya kwenda kucheza soka nje ya nchi wakati huu, wanafananisha na jinsi Mbwana Samatta alivyoondoka Simba akiwa na miezi sita tu baada ya kujiunga.
Ukiangalia kwa undani mazingira ni tofauti. Samatta alikuwa na bahati kidogo.
Alijiunga na Simba wakati ikiwa inashiriki mechi za kimataifa. Alicheza mechi za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu msimu wa 2010/11 akifunga mabao saba na wakati timu yake ikicheza mechi ya Ligi ya Mabingwa aling'ara kwenye mechi ya awali na zile mbili dhidi ya TP Mazembe nyumbani na ugenini.
Hiyo ilifanya benchi la ufundi ya TP Mazembe liamue kuchukua kipaji hicho na kwenda kumtengeneza tena upya ili afikie kiwango walichokuwa wakikihitaji wao.
Kwa upande wa Kichuya ana bahati mbaya. Simba haitocheza mechi yoyote ya kimataifa mwakani. Lakini pia hata kwenye Ligi Kuu bado haijafika mwisho.
Anachotakiwa kukifanya ni kuwa kwenye kiwango alichokuwa nacho hivi sasa au zaidi na si cha kushuka na kupanda kama homa za vipindi.
Akiichezea timu kubwa kama ya Simba kwa msimu mzima, tayari atakuwa amekomaa na msimu wa pili ndipo sasa aanze kuangalia maisha mengine nje ya nchi.
Na inaweza ikawa vizuri zaidi akawa ameipa mafanikio klabu yake kuiwezesha kucheza mechi za kimataifa, hapo ndipo anaweza kujiuliza kwa urahisi zaidi na kwa gharama na thamani kubwa tofauti na hivi sasa.
Mchezaji anapochukuliwa na timu nyingine nje ya nchi, akiwa ameonekana kwenye Ligi ya Mabingwa au Shirikisho anakuwa na thamani zaidi, hivyo ataiingizia Simba pesa nyingi, pamoja na yeye mwenyewe kupata mshahara mnono.
Uzuri ni kwamba hata yeye mwenyewe amelitambua hilo na kusema kuwa akili yake kwa sasa ni kutaka kuisaidia klabu yake kutwaa taji lolote kubwa litakaloifanya kucheza mechi za kimataifa ili aondokee akiwa kwenye ngazi hiyo na si katika mechi chache tu za ligi.
Ndiyo. Kwa sababu kwanza tunachotaka kwake ni kujidhihirisha kama kiwango alichonacho ni endelevu? Isije ikawa ni kama baadhi ya wachezaji tuliowaona huko nyuma tuliotegemea kama hawatocheza soka nchini kwa muda mrefu kabla ya kutimkia nje ya nchi kutokana na kuonyesha uwezo mkubwa kwa muda mfupi kama kina Edward Christopha, Geofrey Mwashiuya na wengineo.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








