Asiyeuliza hana ajifunzalo

18Oct 2016
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Asiyeuliza hana ajifunzalo

HUKO twendako maneno mengi ya Kiswahili yatapoteza maana kwani yatakayotumika ni maneno ya mitaani yasiyo kwenye msamiati wa Kiswahili.

Kwa mujibu wa Kamusi la Kiswahili fasaha, ‘majeruhi’ pia ‘majuruhi’ ni mtu aliyeumia kama vile katika ajali. ‘Jeruhi’ ni kitendo cha kumuumiza au kumtia mtu kidonda. ‘Jeraha’ pia ‘jaraha’ ni kidonda kipya.

Kamusi ya Karne ya 21, ‘majeruhi’ ni mtu aliyepata jeraha, mtu aliyeumia katika ajali na kupata majeraha. ‘Jeraha’ ni kidonda au mchubuko ulio katika mwili. ‘Jeruhi’ ni piga mtu kwa silaha au kitu kingine chochote na kumsababishia jeraha.

“Katika mchezo wa jana Yanga iliwakosa mastaa wake ghali ambao wengi wanakabiliwa na majeruhi …”

‘Staa’ limetoholewa (kubadilisha matamshi au tahajia ya neno la lugha moja ili lilingane na matamshi au tahajia ya lugha nyingine) kutoka Kiingereza (‘star’) lenye maana ya ‘nyota.’

Watu hawakabiliwi na ‘majeruhi’ bali huwa majeruhi kutokana na ‘majeraha’ wanayopata. Kwa hiyo wanaojeruhiwa huitwa ‘majeruhi.’

‘Kabili’ (i) sogelea au pambana na jambo ama mtu; chegama; (ii) kitendo cha mtu kumwendea mwingine kutaka haja; (iii) mwenye uwezo wa kufanya jambo na (iv) mpiga zumari kwenye ngoma.

Ingeandikwa: “Yanga jana iliwakosa nyota wake walio majeruhi,” Ni kosa kusema/kuandika “wanaokabiliwa na majeruhi.”

“Kwa African Lyon hiyo ilikuwa ni mechi yao ya pili baada ya mechi ya ufunguzi kulazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam FC, mechi iliyopigwa Chamazi nje kidogo ya jijini la Dar es Salaam.”

Mechi ‘haipigwi’ bali huchezwa. Pia si sahihi kuandika “nje kidogo ya ‘jijini’ la Dar es Salaam.” Ingeandikwa “…Ilikuwa mechi ya pili kwa African Lyon baada ya kutoka sare ya 1-1 na Azam kwenye mechi ya ufunguzi kule Chamazi n-nje ya jiji la Dar es Salaam.”

Swali: Anayelazimisha sare ni anayetangulia kufunga au anayesawazisha? African Lyon ilikuwa ya kwanza kufunga wakati Azam FC ilisawazisha dakika za nyongeza. Iliyolazimisha sare ni Lyon au Azam?

“Kaseke ndiye aliyeanza kutikisa nyavu za African Lyon ikiwa ni dakika ya 18 tangu mchezo uanze …” Katika makala zilizotangulia nilieleza kuwa ‘nyavu’ ni wingi wa ‘wavu’ lakini bado waandishi wanashikilia neno ‘nyavu’ kana kwamba golini kuna wavu zaidi ya mmoja!

‘Wavu’ ni nyuzi au nyaya zilizosukwa na kufanya utandu wenye tundu ndogondogo unaotumiwa kwa shughuli mbalimbali kama uvuvi, kutegea wanyama, kufunga kwenye magoli n.k. kimia.

Ingeandikwa “Kaseke ndiye aliyeanza kutikisa wavu wa African Lyon dakika ya 18 kipindi cha kwanza.”

“…Yanga walikimbilia langoni mwa wapinzani wao na kufanya shambulizi lingine muda huo huo baada ya Mwinyi Haji kupiga krosi iliyomkuta Tambwe aliyepiga kwa kichwa kilichotoka nje ya goli.”

Ilivyo hapa ni kwamba kichwa cha Tambwe kilitoka n-nje ya goli! Maana yake kiwiliwili cha Tambwe ndicho kilichobaki baada ya kichwa chake kumeguka (kukatika na kutoka sehemu yake)!

“…Tambwe naye akikosa nafasi nyingine ya kufunga kwani mpira wa kichwa aliopiga uligonga besela na kurudi uwanjani akipokea krosi ya Kaseke.”

‘Besela’ si Kiswahili. Neno sahihi ni ‘besera’ yaani milingoti inayozuia samadari ya kitanda kwa mujibu wa Kamusi la Kiswahili Fasaha.

Kamusi ya Karne ya 21 yaeleza maana ya ‘besera’ kuwa papi zinazopigiliwa kwenye vitakizo (sehemu za mbele au nyuma za kitanda zinazounganishwa na mifumbati) vya kitanda au kuning’inizwa juu ya kitanda ambapo hufungiwa chandarua.

“Dante anapiga vichwa hadi aibu” ni kichwa cha habari inayoeleza kuwa “Beki wa Yanga amecheza dakika 90 za kwanza katika Ligi Kuu Bara lakini kocha wake Hans Pluijm akatamka kwamba amekubali kila kitu hususani jinsi anavyoruka vichwa.”

Sijui mwandishi anakusudia nini kuandika “ … Dante anapiga vichwa hadi aibu.” ‘Aibu’ ni jambo la kumtia mtu fedheha, kumvunjia mtu heshima; tahayuri, soni. He! Dante anapiga vichwa hadi anajiaibisha? Kwa lipi? Pili, huandikwa hususan au hususa si ‘hususani!’

“Simba yamkwida Mbaraka.” Chini ya kichwa hiki imeelezwa kuwa klabu ya Simba ilimwekea pingamizi straika wao Mbaraka Yusuph kwa kosa la kusaini mkataba mpya na Kagera Sugar …”

Ah! Simba yamkwida Mbaraka? Mwandishi ajua maana ya neno ‘kwida’? Ni shika kwa nguvu shati au gauni na kulibanisha na mwili.
Minya mtu kwa nguvu kama njia ya kumlazimisha atende utakalo. Pia ni mdudu mdogo mweusi jamii ya sisimizi anayetafuna.

Je, ni kweli Simba walimkwida (mminya) Mbaraka kumlazimisha atende watakalo? Pia badala ya ‘straika’ lingetumiwa neno ‘mshambuliaji.’

Methali: Asiyeuliza hana ajifunzalo.
marobarnabas@yahoo.com
0715/0784 33 40 96