Polisi wawajibike uharibifu U/Taifa

17Oct 2016
Sanula Athanas
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Polisi wawajibike uharibifu U/Taifa

WIKI iliyopita gazeti hili lilieleza jinsi serikali ilitakavyokosa takribani Sh. milioni 750 msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na klabu za Simba na Yanga kuzuiwa kuutumia Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, ndiye aliyetangaza uamuzi wa kuzipiga marufuku klabu hizo kongwe kucheza kwenye uwanja huo mkubwa zaidi nchini baada ya mashabiki wake kuvunja mageti manne na kung'oa viti 1,781.

Tukio hilo la fedheha kwa soka la Tanzania, lilitokea wakati wa mechi ya kwanza ya watani wa jadi msimu huu iliyomalizika kwa sare ya bao moja (1-1) kwenye uwanja huo.

Uharibifu wa miundombinu ya uwanja huo ulianza kabla ya kipenga cha kwanza cha refa Martin Saanya, mashabiki wa pande zote walipovunja mageti na kuingia uwanjani kwa nguvu kutokana na kile kilichoelezwa kuwa changamoto za matumizi ya tiketi za kisasa za kielektroniki.

Mashabiki wa Simba walikumbushia tabia yao iliyoibuka miaka ya hivi karibuni ya kung'oa viti baada ya mshambuliaji wao wa zamani, Mrundi Amissi Tambwe, kuwazidi ujanja marefa wa mechi hiyo kwa kujipasia kwa mkono na kuipatia Yanga goli la kuongoza dakika nne kabla ya nusu saa ya mchezo.

Tabia hii haipaswi kuungwa mkono na inapaswa kukemewa na kila anayelitakia mema soka la Tanzania. Hata kama Saanya na wasaidizi wake walifanya makosa katika uamuzi wao, bado haikuwa sababu kuntu kwa mashabiki wa Simba 'kuviadhibu' viti vya Uwanja wa Taifa.

Mashabiki hao pia hawakuwa na haki ya kufanya vurugu za aina yoyote uwanjani na hata nje ya uwanja kwa kuwa makosa ya marefa ni sehemu ya mchezo ndiyo maana kumekuwa na marekebisho ya mara kwa mara Sheria 17 za Soka.

Ni vyema pia Jeshi la Polisi likalitumia tukio lililojitokeza siku hiyo kujipima kiutendaji maana zaidi ya viti 1,700 kung'olewa na kutupwa mbele ya mboni za askari wake ni changamoto.

Ikumbukwe kuwa kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kutokana na wengi wao kuonekana kama huwa wanakwenda uwanjani kutazama mechi badala ya kutekeleza wajibu wao.

Simba inatakiwa kulipa Sh. milioni 391.82 kutokana na uharibifu wa viti 1,781 (kila kiti Sh. 220,000). Klabu hiyo inatakiwa kulipa kiasi hicho cha fedha ilhali kuna watu (polisi) wamekuwa wakilipwa mamilioni ya shilingi na Shirikisho la Soka (TFF) kwa ajili ya kuimarisha ulinzi uwanjani.

Polisi wanatakiwa kulinda usalama wa watu na mali zao. Na wanapokuwa kwenye mechi ya soka, wanakuwa wanatekeleza majukumu ya ziada ndiyo maana wanalipwa.

Kwa mujibu wa Jonas Mahanga, aliyekuwa Ofisa Usalama wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) nchini, kwenye gharama za mechi ambazo mapato ya timu hukatwa, kunakuwa na fungu kwa ajili ya ulinzi ambalo kila askari hulipwa posho ya Sh. 15,000 (Sh. 5,000 ya chakula) kwa kila mechi.

Ni kutokana na malipo haya, ndiyo maana nafikiri Jeshi la Polisi linapaswa kuwajibika kwa uharibifu uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa siku ya kwanza ya mwezi huu.