Katika uwanja huo, kutafanyika mkutano wa hadhara utakaohutubiwa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, Lissu, ambaye anatarajiwa kurejea nchini saa 7:35 mchana wa leo.Lissu ambaye ni mwanasheria, alipata hifadhi ya kisiasa nchini Ubelgiji baada ya kunusurika kifo tangu mwaka 2017 na sasa anarudi nyumbani kutokana na kile anachoeleza kuwa ni kuwapo kwa mazingira mazuri ya kuendesha siasa.Mazingira hayo yanatajwa kuwekwa na serikali ya awamu ya sita kwa lengo la kujenga taifa lenye maridhiano, ustahimilivu, mabadiliko na ukuaji wa demokrasia, ambapo katika eneo la maridhiano ya kisiasa, ndipo suala la mikutano ya vyama vya upinzani linapoingia.Ratiba ya ujio wake inaonyesha kuwa baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Dar, atakwenda Mwembe Yanga Temeke kuhutubia mkutano huo wa hadhara.Wakati wanachama na wafuasi wa CHADEMA wakisubiri kwa hamu ujio wa kiongozi wao huyo, si vibaya kukumbushana mambo kadhaa yenye lengo la kusaidia kuendesha siasa zenye manufaa kwa umma.Kiongozi huyo ni mwanaharakati, lakini ni vyema asije akayumbishwa na wanachama wanaotamani kusikia siasa za uanaharakati ambazo hufikia 'kuwashambulia' wengine kwa maneno.Kwa kutumia ushawishi wake wa kisiasa, awasaidie wanachama wenye mihemko ya kisiasa kubadilika ili wajielekeze katika siasa za kistaarabu zinazosaidia kuwaunganisha Watanzania.Wakati mwingine siasa za aina hiyo hugeuka kuwa za majitaka, hasa kutokana na kuwatukana wanasiasa wengine au kurushia wengine maneno makali, jambo ambalo linaweza kuleta sintofahamu katika siasa za sasa.Ikumbukwe kuwa marufuku ya mikutano ya hadhara ya kisiasa imeondolewa, na sasa Watanzania wanatamani kusikia hoja zenye majibu ya kutatua changamoto zinazowakabili badala ya kulalamika tu.Tayari Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe ameshaonyesha njia katika uzinduzi wa mikutano ya hadhara kwa kujikita katika hoja badala ya mashambulizi kwa wengine.Hivyo, wanasiasa wengine akiwamo Lissu ni vyema wakaiga mfano huo, ili mikutano ya vyama vya siasa iweze kujaa watu wengi wanaosikiliza hoja za viongozi wa vyama hivyo na si kuwakatisha tamaa.Kwa kuwa Lissu naye anasubiriwa kwa hamu kuhutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Mwembe Yanga, ni vyema akafuata nyayo za mwenyekiti wake, kwa kujikita zaidi katika hoja za chama hicho.Mwanasiasa huyo ni miongoni mwa wana CHADEMA wenye uwezo mkubwa wa kujenga hoja, ninaamini kwa njia hiyo ataweza kuteka watu wengi na kuondoa dhana kuwa viongozi wa chama hicho wamezoea kutukana.Ameitikia wito wa Rais Samia Suluhu Hassan na kunaonyesha utayari kurudi nyumbani kuendeleza siasa na pia kushiriki katika mchakato wa katiba mpya, ni muhimu hayo yakafanyika na kuleta matokeo chanya.Tangu awali wakati anaingia madarakani, Rais ameonyesha utayari wa kukutana na viongozi karibu wote wa vyama vya upinzani na kutoa ruhusa ya mikutano ya hadhara, ilikuwa mojawapo ya mambo aliyoshauriwa kufanya na wadau mbalimbali wa siasa akakubaliana nao.Kilichobaki sasa ni wanasiasa wenyewe akiwamo Lissu, kutumia nafasi hiyo kunadi sera za chama chake kwa umma wa Watanzania na kufanya maandalizi ya kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa.Hata Rais anasubiri kuona kile ambacho anatamani kukisikia nacho ni kutamalaki kwa siasa za kistaarabu, huku wanasiasa wakitumia nafasi hiyo kujadili masuala muhimu pasipo kufanya mambo yatakayoharibu amani, utulivu na maadili ya Watanzania.
Karibu Lissu, leo Mwembe Yanga
25Jan 2023
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Karibu Lissu, leo Mwembe Yanga

MACHO na masikio ya wanachama na wapenzi wa CHADEMA wa Dar es Salaam na vitongoji vyake, leo yatakuwa yameelekezwa katika Uwanja wa Mwembe Yanga Temeke, kumsikiliza Tundu Lissu, baada ya kurejea nyumbani.


.jpg?itok=nfwjwDzv)







