Ni somo ambalo mwanafunzi yeyote anayelimudu vema, anatazamwa si tu shuleni na familia, hata na jamii kama si mtu wa kawaida anakuwa wa kuheshimika.
Kuna baadhi ya wanafunzi hawapendi kuliona wala kulisikia. Wanaamini ni somo linalowasumbua ubongo tu, kwani kwenye maisha hawaendi kukutana nalo, japo ukweli wanajidanganya.
Wanaamini safari yao ya maisha wanaenda kukutana na mambo mengine tu, kama kuajiriwa na kufanya kazi, biashara, mapenzi, mambo ya kijamii na yanayofanana na hayo.
Wanaamini somo la hesabu linawafaa wanafunzi watakaoenda kufanya kazi za fedha, urubani, ukandarasi na zinazohitaji zaidi mahesabu, kuliko masomo mengine.
Kitu ambacho wengi hawaelewi ni kwamba, kwa binadamu, chochote anachofanya ni mahesabu. Kuanzia anapoamka asubuhi, anapotembea hadi anaporudi tena nyumbani kulala.
Kupanda kulala saa sita na kutakiwa kuamka saa 11:00 alfajiri ni hesabu tosha. Kuamka asubuhi, kupanga muda wa kunywa chai, hadi kufika ofisini kwa muda unaotakiwa, pia ni mahesabu.
Barabara inabidi uvuke kwa mahesabu, hata ukiangalia jengo lilivyojengwa, nazo ni kwa hesabu kali.
Nijumuishe, muundo wa maghorofa, nyumba tunazoishi, vyoo, vifaa vya teknolojia, nazo ni zao la hisabati na vimetengenezwa kwa mahesabu.
Nitoe mfano mdogo tu, mvua zikinyesha, maji huwa hayatuami pale barabarani na inapokuwa imejengwa kwa mahesabu bora, athari hazitokuwapo.
Ni kwamba hujengwa ikiwa upande mmoja umeinama na mmoja umeinuka, maji ya mvua yatatiririka kwenda upande mmoja.
Hesabu zingine kwa watengenezaji ni kwamba, baadhi ya barabara kati kuna mgongo, yaani pameinuka, halafu kwenda kushoto na kulia kunakuwa na mteremko ili kufanya maji kutiririka pande zote.
Kwa macho ya kawaida, inatajwa ni ngumu kuliona hilo. Hata wanaojenga vyooni, hufanya hivyo ili maji yanayomwagika pande zote yaende kwenye shimo.
Hapa nimetoa mfano wa vitu hai tunavyoishi navyo, kuhusu mahesabu. Mjenzi wa nyumba ana kitu kinaitwa 'pima maji'. Ni kifaa cha kimahesabu kinachomuongoza mjenzi asipindishe ukuta.
Kwa maana hiyo hesabu hazikimbiwi sehemu yoyote kwenye maisha. Hata bajeti ya nyumba, nini kinunuliwe kwanza cha umuhimu na nini kisubiri ni hesabu zinatumika.
Pamoja na kwamba hesabu si somo pendwa, lakini kwa miaka ya karibuni watahiniwa wameonekana kufanya vibaya zaidi, tofauti na zamani. Hapa kuna tatizo lazima lifanyiwe kazi haraka sana.
Kuna sehemu wazazi na serikali lazima wakae chini, ikiwamo kuwashirikisha wataalamu, ili kuangalia tatizo liliko.
Mwishoni mwa wiki Baraza la Mitihani (NECTA) lilitangaza matokeo ya mitihani ya kidato cha nne. Pamoja na kwamba ufaulu umeongezeka, lakini kwa somo la hesabu umeshuka na hali ni mbaya.
Takwimu walizotupa, kati ya watahiniwa 520,558 wa somo hilo, 415,844 hawakufaulu, hivyo kuwa na asilimia 79.92 ya wanafunzi ambao hawakufanya vema kwenye somo hilo.
Najua hakuna kitu chochote kinachotolewa kama fasheni tu au kuonyesha jinsi gani wanafunzi walivyofeli. Ila NECTA hesabu hapa wamemaliza kazi yao na hesabu hizi zimetolewa ili wanaohusika wafanye kazi zao.
Tukianza kwa serikali, yenyewe ina wataalam wengi, hivyo sasa wasikae maofisini tu, waanze kuzunguka na kufanya utafiti kwanini ‘madenti’ wanaonekana kufeli somo hilo kila kukicha, halafu waje na majibu kama uwezo mdogo wa walimu wa eneo hilo au kuna mengine zaidi?
Kwa wazazi, mimi ni mmoja kati yao. Naweza kuainisha baadhi, nikianza na ukweli kwamba, siku hizi wazazi wanawalea watoto 'kimayai' sana, kiasi kwamba wanashindwa kukabiliana na changamoto za kutenda na kufikiri.
Malezi ya wazazi zamani yalionekana kuwatesa watoto au kuwapa baadhi ya mambo wayafanye wenyewe; kufua nguo, kupika na kazi nyingi nyumbani, kwenda sehemu ya umbali mrefu, na mengine yanayofanana na hayo yaliwafanya wawe na uwezo mkubwa wa kufikiri na kutenda.
Hesabu zinamtaka mtoto mtulivu, mwenye uwezo wa kufikiri na kutenda kwa haraka. Mtoto yeyote ambaye hapati changamoto hata nyumbani, hesabu kwake lazima ziwe ngumu.
Nadhani wazazi tuanzie hapo. Tusiwadekeze sana watoto wetu kiasi kwamba wakikutana na changamoto ndogo tu ya kutumia akili, au kutenda inakuwa tatizo.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








