Sasa ni karibu kila mkoa umetangaza msako wa wanafunzi watoro wanaotakiwa kuanza kidato cha kwanza mwaka huu, hali inayoonyesha kuwa tatizo hilo linazidi kuwa kubwa.
Mfano, wiki iliyopita, madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe waliazimia kufanya msako wa wiki moja wa nyumba kwa nyumba, ili kuwarejesha wanafunzi watoro zaidi ya 1,000 madarasani.Wakati hao wakiazimia kufanya msakao huo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila naye amewaagiza viongozi na watendaji wote kuanzia ngazi ya mtaa kuanzisha msako kama huo.
Kwa mujibu wa Chalamila, wanafunzi 59,324 walichaguliwa kuingia kidato cha kwanza mwaka huu, lakini walioripiti shuleni ni 35, 594, na kwamba 23,730 wapo mitaani.
Licha ya kuwapo jitihada mbalimbali zinazofanywa ili kukomesha utoro shuleni, ikiwamo msako dhidi ya wanafunzi watoro, inaonekana utoro bado ni miongoni mwa vikwazo vinavyozikabili shule za umma.
Kwa hali hiyo, ni vyema wakati msako wa wanafunzi wa kidato cha kwanza ambao hawajaripoti shuleni ukiendelea, ninadhamini kuna haja pia kutafuta uliko mzizi wa utoro huo na kupatia ufumbuzi wa kudumu.
Ninashauri hivyo, kwa sababu ni karibu kila mkoa umekuwa na matukio ya utoro ambayo yamewafanya viongozi wa mikoa husika kutangaza msako dhidi ya watoto watoro na hata kwa wazazi na walezi wao.
Serikali inatoa elimu bure, wazazi na walezi wanawajibika kuwatafutia watoto wao sare, madaftari na vitu vingine muhimu vya shule, lakini ajabu ni kwamba, pamoja na kuwapo kwa unafuu huo, utoro umeshika kasi.
Ninadhani badala ya kuendelea kutumia nguvu kuwarejesha shuleni, zitumike mbinu ambazo zinaweza kubaini chanzo cha utoro, kisha mbinu zitumiwe kuwarejesha wanafunzi wapende shule.
Lakini kuweka malengo ya kutokomeza utoro na kuweka mbinu ambazo zinawashawishi na kuwavutia wanafunzi kupenda kuhudhuria masomo shuleni, huku wenye tabia ya utoro wakipewa uongozi shuleni.
Kwa ujumla, vivutio vingi kama chakula cha mchana na vipindi vya michezo na hata kuwasaidia wanafunzi wanaofanya utoro kwa sababu ya hali ngumu ya maisha, vinaweza kuwarejesha shuleni.
Baadhi ya wanafunzi watoro wanaweza kuwa ni yatima wanaoishi katika mazingira magumu, wengine ni tabia zao au kwa sababu wanazozijua wenyewe, lakini suala la msingi ni kutafuta mzizi wa utoro ni la muhimu.
Si vibaya vikaanzisshwa vikosi maalum vya kuwatembelea wanafunzi watoro nyumbani, ili kujua kinachosababisha wawe watoro na kama sababu zitakuwa ndani ya uwezo wa vikosi hivyo, basi vizitatue.
Inasikitisha kuona kila mwaka wanafunzi wanaochaguliwa kuingia kidato cha kwanza hawaendi shuleni kwa wakati au wanaingia mitini moja kwa moja na kusababisha kuwapo kwa msako dhidi yao.
Lakini katika kundi hilo la hao wanaoitwa watoro, ninaamini wapo wapo wale ambao wazazi wao wanawahamisha na kuwapeleka katika shule binafsi, bila kutoa taarifa, ingawa idadi yao haiwezi kuwa kubwa.
Pamoja na hayo, ni vyema kuwapo kwa kampeni ya kuhamasisha jamii kuelewa umuhimu wa elimu, kuwaelekeza wazazi na walezi ambao watoto wao ni watoro kutambua manufaa ya elimu.
Katika vita dhidi ya utoro, ni muhumu jamii kutambua umuhimu wa elimu na kuungana ili kutofautisha muda wa masomo na muda wa kazi na kuwapunguzia majukumu ya nyumbani, wasiwe watoro.
Inawezekana idadi ya wanafunzi watoro wanaosakwa, wengi wao ni wakike, hivyo kutambua umuhimu wa elimu kunaweza kusaidia kuondoa mtazamo hasi kuhusu kumsomesha binti ni kupoteza pesa.