Kanuni hii ya 'play off' mbili Bara ibadilishwe

09Jul 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kanuni hii ya 'play off' mbili Bara ibadilishwe

KESHO ndiyo mwisho kwa wadau wa mpira wa miguu nchini kutuma mapendekezo ya maboresho ya kanuni za msimu ujao wa mashindano yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka Nchini (TFF).

TFF ilishatangaza huko nyuma kwa wadau wote na wapenzi wa soka kutuma mapendekezo, kitu chochote ambacho anataka kiongezeke katika kanuni za msimu ujao ili kuiboresha ligi hiyo.

Kuna kanuni kandamizi ambayo nataka iondolewe, lakini pia kuna wanaotaka kanuni hizo hizo ziwepo, lakini zifanyiwe marekebisho.

Kinachofanyika ni kuchukuliwa maoni hayo na kuchakatwa, kabla ya kutolewa rasmi na kuanza kutumika kwa msimu husika.

Ili kusiwe na malalamiko yoyote, TFF imetoa anwani yake ikitaka maoni au mapendekezo yatumwe kupitia email yao, maoni@tff.or.tz.

Kwa wadau wa soka bado hawajachelewa, wanatakiwa watume ili baadaye kusiwe na malalamiko kwa TFF wakati watakapozitumia.

Tumekuwa tukiona viongozi, waandishi wa habari na wachambuzi wa masuala ya michezo wakilalamikia baadhi ya maamuzi yanayotolewa na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi kwa madai kuwa hayakutenda haki, au yamepitwa na wakati.

Lakini kwenye nyakati kama hizi huwa hatuwasikii wakipeleka maoni mapya, au kuhitaji marekebisho ya kanuni zilizopita.

Hiki ndiyo kipindi ambacho husikii wachambuzi au mashabiki wa soka wakihamasishana kupeleka maoni, lakini ngoja siku maamuzi ya adhabu yatoke kwa mujibu na kanuni ambazo zimeletwa, kuchakatwa na kupitishwa na kamati husika, ndipo mapovu yanapoanza kuwatoka.

Uzuri ni kwamba maoni anapeleka mtu yoyote, shabiki, mpenzi, mwandishi, mchambuzi, mdau, kiongozi wa soka na yoyote yule anayeguswa na mchezo huo. Hayabagui.

Huwa nashangaa sana wanavyokurupuka na kulalamika mtu anayefungiwa kujihusisha na soka miaka mitano kuwa ni mingi na imepitwa na wakati.

Huu ni wakati sasa wa kupeleka maoni mfano kusiwe na kufungiwa maisha, bali kifungo kirefu kiwe miaka mitano na kifupi mwaka mmoja. Labda kufungiwa maisha iwe tuhuma za kupanga matokeo.

Zipo nyingi kama vile timu za nyumbani ziendelee kuchukua mapato, irekebishwe zigawane nusu kwa nusu, au wa nyumbani achukue asilimia nyingi kidogo, lakini mgeni naye apate.

Nilimsikia kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi akilalamika kuhusu kukatazwa kuchezesha wachezaji wote 12 wa kigeni waliosajiliwa kwenye Ligi Kuu, badala yake wanatakiwa kucheza nane kwa mechi moja.

Si yeye tu, mashabiki wengi wanaipinga kanuni hiyo, huu sasa ndiyo wakati wake wa kwenda kupeleka maoni kuwa irekebishwe, wachezaji wote wanatakiwa waanze iwe wa Kigeni au Kibongo bila ubaguzi. Wanataka mwenye uwezo aachwe acheze.

Kuna faini za timu kupitia milango isiyohusika. Wengi wanalalamika, wanasema ni ndogo sana na ndiyo maana timu hazijali, zinaendelea tu na tabia hiyo.

Kinachotakiwa sasa ni kupeleka maoni ya kutaka faini iongezwe, ili timu ikipigwa, basi isijifikirie tena kurudia kosa.

Leo mimi pendelezo langu ni mechi za mchujo ambazo kwa sasa zinaendelea. Hazitendi haki. Prisons ambayo imefungwa na Mtibwa Sugar, eti inakwenda kucheza 'play off'  ya pili.

Haya ni matumizi mabaya ya rasilimali na muda. Pia kutozitendea haki timu za Champioship.

Ikumbukwe JKT Tanzania ilishika nafasi ya tatu, ikaifunga Kitayosce iliyoshika nafasi ya nne, leo hii ikija kufungwa na Prisons  na kukosa kurejea Ligi Kuu ni jambo linalokatisha tamaa.

Haiwezekani timu iliyofungwa kwenye Ligi Kuu iende kucheza na timu iliyoshinda Championship halafu aliyefanya vibaya kwenye Ligi Kuu anarejea tena kwa sababu kashinda mechi ya pili ya mchujo.

Kanuni hii haina mashiko, inabidi ibadilishwe kwa mustakabali wa soka la Tanzania. Tangu kanuni ya 'paly off' ianze imeonekana kuzinufaisha zaidi timu za Ligi Kuu zaidi kuliko za chini ambazo inabidi ndiyo ziandaliwe mazingira ya kutengenezewa kanuni ya kuwathamini zaidi.

Mawazo au maoni yangu ni kwamba kuanzia msimu ujao ni kwamba kila timu zicheze 'play off' moja zenyewe. Za Ligi Kuu zicheze yao na za Champioship zicheze ya kwao na timu itakayoshinda inapanda na itakayofungwa inateremka moja kwa moja ili kurahisisha kazi na kuweka usawa pia.

Mfano kwenye ushindi wa jumla Mtibwa Sugar ilishinda, hivyo ilibidi ibaki Ligi Kuu na Prisons ishuke. Na Champioship, JKT Tanzania ilitakiwa iwe tayari nayo imepanda Ligi Kuu.

Nadhani hapa tutakuwa tunatenda haki zaidi, hivyo ushauri wangu msimu ujao kanuni hii ibadilishwe kwa sababu inaleta ukakasi na ni kandamizi kwa timu za madaraja ya chini.