Fanya hivi ili usitapeliwe ardhi yako inauzwa kwa watu wawili

08Jul 2022
Halfani Chusi
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Fanya hivi ili usitapeliwe ardhi yako inauzwa kwa watu wawili

UKINUNUA ardhi kwa maana ya nyumba, kiwanja, au shamba hakikisha unafanya uhamisho wa miliki kutoka kwa aliyekuuzia na kusomeka kwa jina lako mara moja kadri iwezekanavyo, ili kujiepusha na mambo mengi, ikiwamo kutapeliwa au kuuziwa kiwanja kimoja mara mbili.

Wengi tukinunua viwanja kwa sababu hakuna anayetuuliza wala kutulazimisha kufanya uhamisho kwa haraka basi tukishakabidhiwa hati na mikataba ya mauziano tunakaa nazo hata miaka miwili au mitatu, huku tukisema nikipata pesa nitaenda kubadilisha umiliki hilo ni kosa kubwa.

Inapaswa kutambua kuwa, kama haujabadilisha jina kutoka kwa mmiliki wa ardhi aliyekuuzia, kuna uwezekano mkubwa aliyekuuzia akakuzunguka na kukiuza kwa mtu mwingine na hata kukuchezea anakuwa na uwezo mkubwa.

Nilipopiga stori na Wakili wa Kujitegemea, Bashiru Yakubu, alinieleza mengi ikiwamo namna watu wanavyodhulumika na kukosa haki kwa kutokujua umuhimu wa kufanyia uhamisho.

Akanidokeza kwa darasa: “Mfano ni kwamba, kuwa aliyekuuzia anaweza kutoa taarifa ya kupotelewa kwa hati kituo cha polisi kisha akapewa kibali kinachoonyesha kupotea kwa hati (loss report) anaendelea

“Baada ya hapo akafanya tangazo kwenye radio, tv, na kwenye magazeti ya serikali na binafsi halafu akafanya maombi ya kupatiwa hati mpya kupitia Fomu namna Tatu chini ya Kifungu cha 38 cha Serikali ya Usajili wa Ardhi Sura ya 334.”

Kisha hapo mtu anapatiwa hati nyingine mpya, hiyo inafanya kutakuwapo hati mbili katika ardhi moja. Huo tayari unakuwa kiashiria cha mgogoro, kwako mnunuzi usiye na hati.

Akishakuwa na hati, hayo mengine anaweza kuyakataa kirahisi na pengine watu wa namna hii hata zile saini anazokuwa amekuwekea kwenye nyaraka nyingine, zinaweza kuwa sio zake.

Mbaya zaidi, ni kwamba mtu usipofanya uhamisho na wakati umeshanunua shughuli zote zinazohusu ardhi hiyo mfano kulipa kodi za ardhi, vibali vya ujenzi, tathmini, tozo na kila kitu kinaendelea kusoma jina la aliyekuuzia na malipo yataendelea fanyika kwa jina la aliyekuuzia.

Maana yake ni kwamba, ushahidi wote wa risiti na nyaraka nyinginezo unaendelea kumtambua aliyekuuzia kuwa mmiliki halali wa ardhi hiyo ambapo anaweza kutumia ushahidi huo dhidi yako na ukakosa haki.

Hiyo ni kwa sababu, ataonyesha risiti znazosoma jina lake na atasema nilikuwa nalipia atachukua hata kibali cha ujenzi bila wewe kujua na atakioonyesha kinasoma yeye.

Ndugu yangu, katika mazingira hayo kushinda kesi hiyo kunahitaji muujiza wa Mwenyezi Mungu, kama utabahatika kuzipata, lakini kama umefanya uhamisho mchezo huo ni mgumu sana na pengine haitawezekana kabisa.

Nasema, hata ikiwezekana kwa nguvu ya rushwa au utumiaji wa mamlaka,  bado mnunuzi utakuwa salama kwa sababu ya mfumo utaonyesha umiliki ulivyokuwa ukihamishwa kutoka kwa mmiliki mmoja kwenda kwa mwingine.

Ninachotaka kushauri, unaponunua kiwanja au ardhi kwa lengo fulani inatakiwa kufanya uhamisho wa umiliki mapema najua wengi wetu tunaogopa gharama ambayo ni asilimia 10, lakini hiyo huwa inazungumzika na kupungua.

Pia, wakati wa kununua ardhi hakikisheni mikataba yenu inashuhudiwa na wanasheria (mawakili) wakili kwa cheo chake ni ofisa wa viapo na mthibitishaji wa umma, pia ni ofisa wa mahakama.

Wakili akiwa kwenye makataba wako wa manunuzi, ni mtu muhimu sana na ushahidi wa hakimu unaaminiwa sana na mahakma.

Waswahili wnasema heri nusu shari kuliko shari kamili katika andiko. Hili ni bora utekeleze ushauri huo ukawa salama katika ardhi yako, kuliko kupuuzia ukaingia hasara ya eneo lako kabisa na ukalikosa mjini wajanja wajanja ni wengi sana.