Simba, wanahabari, hawakumtendea haki Makelele

11Jul 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Simba, wanahabari, hawakumtendea haki Makelele

MIAKA ya nyuma kulikuwa na makala na mijadala mingi ya watangazaji na wachambuzi kuzilaumu klabu hasa kubwa za Simba na Yanga, hasa pale wachezaji na makocha wao wa zamani wanapougua.

Klabu za Simba na Yanga zilikuwa zinabebeshwa mizigo isiyokuwa yao, kwa kuelezwa kuwa zimewatelekeza wachezaji au makocha wao wa zamani wanapoumwa.

Utashangaa kusikia eti mchezaji wa miaka ya nyuma wa Simba au Yanga ambaye baada ya hapo alikwenda kucheza soka kwenye klabu nyingine, lakini akianza kuumwa, au amelezwa hospitali, basi inaelezwa kuwa ametelekezwa na kwa nini haimhudumii.

Nakumbuka wakati kocha wa zamani wa Simba, James Siang'a akiwa mgonjwa, baadhi ya wachambuzi waandishi wa makala waliandika kuishutumu Simba kwa kumtelekeza.

Huyo nimetolea mfano tu, wapo wachezaji wengi na makocha ambao wanapatwa matatizo, lakini vidole zinaonyeshwa Simba au Yanga.

Nilishangaa, kwani Siang'a, baada ya Simba alikwenda klabu ya Express ya Uganda. Yenyewe haikunyooshewa vidole.

Nami nikafanya uchunguzi wangu mdogo tu, nikaibuka na makala iliyozima tabia hiyo.

Nikaandika Simba na Yanga ni Taasisi au Kampuni kama zingine na haziwezi kumhudumia mfanyakazi ambaye hayupo kazini kwa muda huo, au amestaafu. Kama kampuni zimekuwa zinawatibua wafanyakazi waliopo na walioacha kazi kwa sababu mbalimbali, zingekuwa zimeshafilisika.

Mfanyakazi huwa anawekewa akiba yake au mafao na kampuni yake, basi. Akistaafu au kuondoka kampuni haihusiki kumhudumia akiumwa.

Sikukataa kama wafanyakazi wenzake wa zamani akimchangia, iwe kwenye magrupu au vyovyote vile, lakini kampuni huwa haihusiki.

Hata klabu hizi nazo zina mamia ya wachezaji waliozichezea tangu miaka ya 1960, hadi leo hii na hawapo kwenye timu. Na makocha pia. Kwa vyovyote haiwezi kuwahudumia.

Pia hawa wachezaji waliokuwa wanalipwa, hawakucheza bure, hivyo hawana cha kuzidai klabu hizo. Somo likaeleweka. Lakini hivi majuzi klabu ya Simba imefanya jambo ambalo hili sasa inabidi lipigiwe kelele.

Aliyekuwa mchezaji wao, John Makelele 'Zigzag' alifariki dunia Jumamosi ya Julai 2, hatukuona angalau kupewa heshima tu ya kupotiwa kwenye akaunti ya klabu hiyo.

Ndiyo, si wote, au wachezaji wote wa klabu hiyo wapostiwe, lakini wale waliofanya makubwa ilibidi wafanyiwe hivyo, ikiwezekana na zaidi, kwani sikusikia hata kutuma salamu za rambirambi.

Sijui kilitokea nini, kwani viongozi wa zamani wa Simba bado wapo na wala hatukuwasikia kusema lolote, achilia mbali hawa wa sasa.

Sikutegemea mchezaji kama Makelele ambaye ana rekodi ya kuinusuru Simba kushuka daraja kifo chake kupita hivi hivi tu kama aliyefariki ni mtu wa kawaida.

Nilipongeze Shirikisho la Soka Nchini (TFF) ambalo lilituma salamu za rambirambi na kaposti kifo cha mchezaji huyo aliyeitumikia pia timu ya taifa, Taifa Stars.

Niseme tu hapa nchini kuna tatizo la kutojali historia, au rekodi zilizowekwa na wachezaji waliopita. Hata hawa wa sasa walimaliza na yao yatamalizika tu. Ingekuwa Ulaya kifo chake kingekuwa ni habari kubwa. Fikiria mchezaji aliyefunga goli ambalo limeinusuru Manchester United, Chelsea, Real Madrid, yaani hadi wachambuzi wetu hapa wangemchambua, lakini huyu Mbongo wameshindwa kumpa thamani.

Japo wengi wana umri mdogo, lakini maana ya uchambuzi na uandishi ikiwemo wa michezo ni kufukua rekodi za nyuma. Soka ni mchezo wa rekodi, historia na takwimu

Mtu ambaye Julai 23, 1988, alifunga bao la pili dhidi ya Yanga, lililoinusuru Simba kushuka hakupewa stahiki yake hata na klabu yake.

Leo hii wanachama na mashabiki wa Yanga wangekuwa wanaitania Simba kuwa ingewahi kushuka daraja kama isingekuwa mtu huyu, Makelele. Na sijui kama ingekuwa imeshapanda au bado. Inawezekana ingekuwa imependa, lakini ingekuwa na rekodi ya kushuka ambayo watani zao wangeitumia kama fimbo. Huyu mtu ilitakiwa mashabiki wa kizazi cha sasa cha Simba wamfahamu.

Ilikuwa ni mechi ya mwisho wa ligi, Simba ilitakiwa lazima ishinde isishuke daraja na Yanga ilitakiwa sare tu ili itwae ubingwa.

Edward Chumila akaipatia Simba bao dakika ya 21, Issa Athumani akawasazisha dakika ya 36. Makelele alifunga bao la pili dakika ya 58, akiiwezesha timu yake kushinda mabao 2-1, akainusuru Simba kushuka daraja na Yanga ikakosa ubingwa, ambao ulienda kwa Coastal Union. Lakini si wachambuzi wala klabu yake iliyomuenzi. Rekodi aliyoiacha duniani haitofutika milele, ila hakutendewa haki.