Hongera maofisa elimu kwa hatua hii kabambe

28Sep 2022
Beatrice Moses
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hongera maofisa elimu kwa hatua hii kabambe

MAOFISA elimu kuanzia ngazi ya kata hadi mkoa jijini Dar es Salaam, badala ya kutembelea na kukagua shule pekee, kuanzia sasa wataingia darasani kufundisha masomo waliyobobea iwe sayansi, sanaa  na hesabu, badala ya kufanya ukaguzi  kama walivyokuwa wanafanya miaka ya nyuma.

Hatua hiyo imetajwa kuwa ni mojawapo ya mipango iliyowekwa katika kutekeleza miongozo na mikakati ya uendeshaji na usimamizi bora wa elimu katika tawala za mikoa na serikali za mitaa.

Katika mazungumzo na Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam (REO), Abdul Maulid, anabainisha kuwa wanaamini hatua hiyo itasaidia kuboresha au kubaini changamoto wanazokutana nazo wanafunzi au walimu katika masomo mbalimbali kwenye shule hivyo kushirikiana kutafuta ufumbuzi.

Awali, ilikuwa maofisa elimu wakifika shuleni kufanya ukaguzi  lakini bila kufundisha lakini  sasa mambo yamebadilika wanalazimika kufundisha kulingana na utaalamu wa somo ambalo wanalimudu zaidi.

Mfano, kama Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam ni mbobezi kwenye somo la English akifika shuleni ataongozana na mwalimu wa somo mwenye kipindi kwa muda huo ambapo atafundisha wanafunzi japo kwa dakika 45.

Hatua hiyo ni njema hasa ikifanyika kwa umakini ambao unaelezewa kuwa ni mbinu ambayo  kwa kiwango kikubwa itawatia moyo walimu wa somo linaloongezewa ufanisi kwani kuna baadhi ya changamoto zinazomkabili zitabainika na kiongozi wake hivyo kujenga hoja ili kupata ufumbuzi na uboreshaji zaidi.

Mapema mwaka huu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa, alitoa maagizo kwa maofisa elimu wa mkoa na wilaya nchini kuwasimamia wakuu wa shule, walimu wakuu na walimu wa masomo, kuzingatia kalenda ya utekelezaji wa mtaala, ili kuwa na ufundishaji na ujifunzaji wenye tija.

Waziri Bashungwa, anatoa maagizo hayo wakati akizindua kalenda za utekelezaji wa mitaala na mafunzo kwa maofisa elimu wa mikoa na wadhibiti wakuu wa ubora wa shule jijini Dodoma.

Anawataka maofisa elimu mikoa, kutoa mafunzo ya matumizi ya kalenda ya utekelezaji, katika halmashauri, kabla au ifikapo Februari 1, 2023 kwa hiyo hatua hiyo iliyoelezewa na  baadhi ya maofisa elimu kuwa inaonyesha ni kwa jinsi gani pia utekelezaji unavyozingatiwa.

Pamoja na mambo mengine maofisa hao wanapaswa kusimamia kikamilifu ufundishaji wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK)  kwa madarasa ya awali ili kuhakikisha wanafunzi wanaingia darasa la tatu wakiwa wanamudu kikamilifu.

Ili kutimiza azma hiyo ni lazima wanafunzi wote wasome katika mazingira rafiki kuboresha utoaji wa taaluma na ufaulu katika mitihani ya kitaifa, manispaa  zisimamie utekelezaji wa mafunzo ya walimu kazini, kupita kwenye vituo vya walimu na kubadilishana uzoefu na kujenga umahiri wa ufundishaji.

Maono haya ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ni mazuri lakini yatafanikiwa iwapo kutakuwa na ushirikiano katika ya maofisa elimu na wakurugenzi pamoja na wadau wengine wa elimu, kwa kuwa kuzitembelea shule kunahitaji bajeti ikiwamo ya usafiri wa kuwafikisha shuleni.

Maofisa elimu, ni lazima wakumbuke kuwa  uvivu na uzembe au kutojali kazi kutakwamisha kufikia malengo, hivyo wawe wa kwanza kuona umuhimu wa kutekeleza jambo hilo ipasavyo, hivyo wajitokeze kwa moyo kushiriki ili kufikia malengo.

Pia kwa kuwa ni jambo jema siyo tatizo  kwa maofisa elimu wa mikoa mingine kuiga nia  hiyo ikiwa ni kuhakikisha sekta ya elimu inakuwa na mafanikio yenye kuleta maendeleo kwa taifa.