Hili la Wajiki kupigania kunusuru mabinti, linapaswa kuungwa mkono

29Sep 2022
Halfani Chusi
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hili la Wajiki kupigania kunusuru mabinti, linapaswa kuungwa mkono

HONGERA Taasisi ya Wanawake Katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI), kwa kuzindua tena awamu ya tano ya kampeni itwayo ‘Safari Salama Bila Rushwa ya Ngono Inawezekana’,...

...yenye lengo mahususi la kupambana na rushwa ya ngono, utetezi wa haki za kinamama na watoto, pamoja na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Si hivyo tu. Bali mmekuwa bega kwa bega na jamii pale mnapo baini kuwapo kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na, unyanyasaji kwa wanawake, pamoja na vitendo vinavyoashiria rushwa ya ngono. Hii ni hatua kubwa yenye azma ya kupata kizazi chenye usawa na kisicho na dosari ya vitendo hivyo.

Lakini mbali na vyote hivyo, makusudio ya kutumia kampeni hiyo, ni kupaza sauti kwa jamii juu ya kupiga vita rushwa ya ngono na ukatili wa kijinsia, jambo ambalo linapaswa kuungwa mkono na wengi, kwa sababu suala la kumlinda mtoto wa kike ni jukumu letu sote.

Jambo lililovutia zaidi, ni pale waliposoma tathimini ya utoaji wa elimu kwa awamu zilizopita na kubainisha kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia pamoja na rushwa ya ngono vimepungua hizi ni habari njema na inaonyesha ni kwa jinsi gani jamii inapata uelewa kupitia taasisi hiyo.

Katika uzinduzi wa awamu hiyo ya tano, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Janeth Mawinza, alisema kampeni  itajikita zaidi katika kuwapa elimu waendesha bodaboda, bajaji, na daladala, akibainisha kuwa kundi hilo ndio linaloongoza kwa kuwaharibu watoto wengi, kwa kuwashawishi kufanya vitendo viovu kupitia madhaifu yao ya kuhitaji lifti .

Akatamka: “Kampeni hii italenga zaidi kuwapa elimu madereva wa bodaboda, bajaji, daladala, na mabasi ya abiria kwa kupita kila kituo kutoa elimu juu ya masuala ya rushwa ya ngono, pamoja na kutoa vibandiko ambavyo vimebeba ujumbe unaokemea vitendo hivyo.

“Sisi tunashughulika zaidi na watu wanaohusika na usafirishaji, hasa madereva. Mwanzoni kabla ya kuanza kwa kampeni hii, tulibaini madereva daladala, bodaboda, na bajaji ndio sehemu kubwa ambako watoto wanaharibikia ni mahali ambako vitendo vya rushwa ya ngono vimekithiri kwa hiyo sisi tukaona tuanzie huko.”

Alisema katika mazingira hayo wamepata mabalozi wanawapatia elimu juu ya masuala ya rushwa ya ngono na wao wanaenda kuwapatia wenzao kwenye vituo wanavyopaki, pia wamefika hadi shuleni  na kuunda vilabu mbalimbali vya kufundisha namna ya watoto hao wanavyoweza kujiepusha na vitendo hivyo

“Naweza kusema, kwa awamu nne zilizopita wamefanikiwa kufikisha elimu hii kwa ukubwa na baadhi yao wameelimika na wamejua maana ya rushwa ya ngono na ukatili wa kijinsia, anaendelea kuwa ofisini kwetu tunapokea kesi nyingi na tunawasaidia wengi kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria ili kuapata haki zao” anasema mkurugenzi huyo.

Pamoja na mambo mazuri ambayo taasisi hiyo imeyafanya kwa awamu nne zilizopita, lakni bado mkurugenzi huyo anaangusha kilio chake kwa wadau mbalimbali kujitokeza kufadhili mradi huo.

“Sisi tunafadhiliwa na Women Fund Tanzania (WFT), kwa miaka yote hiyo minne na huu wa tano. Kwa hiyo, tunaomba wadau wengine wajitokeze kwa sababu bado tunahitaji kufika mikoani, lakini uwezo wa kifedha kwetu ni mdogo

“Lengo ni kukomboa kizazi chetu wenyewe inauma na inasikitisha unapoona mtoto wa kike amebakwa au ameshindwa kupata ajira kwa sababu amegoma kutoa tendo la ndoa, kwa hiyo tunaomba wafadhili wengi zaidi ili tuifikishe elimu hii mbali zaidi,” anasistiza.

Katika uzinduzi wa kampeni hiyo taasisi hiyo iliambatana na Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma Takukuru Mkoa wa Kitakukuru Kinondoni, Bibie Msumi, ambaye mbali na kuunga mkono jitihada hizo, pia anakemea watu kujihusisha na rushwa yoyote ile akitolea angalizo kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.

“Rushwa ya ngono inaua, inasababisha mimba zisizo na mpangilio, inasababisha magonjwa ya zinaa, inadhalilisha utu, na inaharibu saikolojia ya mtu, kwa hiyo niwaombe watanzania wote kutoa taarifa takukuru pale unapobaini viashiria vya rushwa ya ngono

“Ukishindwa zaidi, fika ofisi zetu zilizopo Magomeni, Dar es Salaam unaweza kuja pale ukatoa taarifa na tukalifuatilia suala hilo bega kwa bega mpaka kuhakikisha linashughulikiwa,” anasema.

Pia katika kuzindua kampeni hiyo, Mratibu Msaidizi Jeshi La Polisi Dawati la Jinsia Mkoa wa Kipolisi Ilala, Joyce Kajiru, alisema kazi ya dawati hilo ni kushughulikia kesi hizo na kuwapeleka mahakamani wote wanaokutwa na hatia ya rushwa ya ngono na ukatili wa kijinsia.